Habari za kugeuka Paulo akaacha kumpinga Yesu, na badala yake akawa mfuasi wake zinasimuliwa pahala patatu katika Matendo ya Mitume katika Agano Jipya la Biblia.
Na katika zote mara tatu kisa hicho kinahitalifiana katika mambo muhimu.
Kwanza tunasoma katika Sura ya 9 mstari wa 3 mpaka wa 7:
Hata (Paulo) alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, (yaani Paulo) mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.
Matendo 9.3-7
Katika maelezo hayo hapo ni mwandikaji anasimulia. Yapo mambo mane lazima tuyazingatie vizuri katika maelezo hayo:
- Mwangaza ambao Paulo ulimwangaza. Haikusemwa kuwa wengine waliuona mwangaza ule au la, lakini waliisikia sauti.
- Ni Paulo ambaye "akaanguka chini."
- Yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye waliisikia sauti, lakini hawakumwona mtu.
- Sauti ya Yesu ilimuamuru "aingie mjini, naye ataambiwa yampasayo kutenda." Hapo hakuambiwa nini la kutenda.
Katika Biblia hiyo hiyo, katika kitabu hicho hicho cha Matendo ya Mitume, sura 22, mstari wa 6 mpaka wa 10 ipo ncha ya pili ya hadithi kusimulia tukio lile lile.
Msimulizi hapa ni Paulo mwenyewe:
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka nchi (yaani chini), nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.
Matendo 22.6-10
Ncha hii yakubaliana na ile ya mwanzo katika mambo haya:
- Aliyeanguka chini ni Paulo na sio wale waliokuwa pamoja naye.
- Aliloambiwa Paulo ni kuingia mjini na huko ndiko atakoambiwa nini la kulifanya.
Ncha hii lakini inakosana na ile ya kwanza kuwa ya kwanza yasema ya kuwa wale waliokuwa naye "wakasimama kimya, wakisikia sauti, lakini haikusema kuwa waliona nuru.
Katika ncha hii ya pili twaambiwa: waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti.
Ncha ya tatu ya tukio hilo hilo muhimu kabisa katika historia ya Ukristo inaelezwa katika maneno yake mwenyewe Paulo vile vile kama inavyosimuliwa katika kitabu kile kile cha Matendo ya Mitume sura ya 26 mstari wa 12 mpaka wa 18:
Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. Tukaanguka nchi (chini) sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! mbona waniudhi? ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo (ujiti wenye ncha wa kuchokolea). Nami nikasema,Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.
Matendo 26.12-18
Sasa hapa tunaona khitilafu kubwa na zile ncha za hadithi ziliomo katika sura ya 9 na sura ya 22 katika hicho hicho kitabu kimoja cha Matendo ya Mitume. Hebu tuchungue:
- Kwa mujibu wa ncha hii si Paulo pekee aliyeona nuru - kama ilivyoelezwa pale mara ya kwanza - lakini wote waliokuwa naye waliona nuru, kama ilivyoelezwa mara ya pili.
- Hapa Paulo anasema: Tukaanguka nchi sote. Haya yanapinga ncha ya kwanza na ya pili zilizosema kuwa ni Paulo tu peke yake ndiye aliyeanguka chini.
- Katika masimulizi ya kwanza na ya pili ilisemwa wazi kuwa Paulo aliambiwa aingie mjini Demeski na huko ataambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa ayafanye. Hii mara ya tatu mambo yote ameamuriwa hapo hapo kabla ya kuingia mjini, kinyume na ilivyosimuliwa mara ya kwanza na ilivyosimuliwa mara ya pili. Tena hapo Paulo alimsikia Yesu anamuamrisha amri kinyume na alivyokuwa akiwafunza na kuwaamrisha wanafunzi wake siku zote katika uhai wake - anamuamrisha Paulo apeleke utume wa Yesu kwa mataifa mengine yasiyokuwa Mayahudi. Kadhaalika kinyume na mafunzo ya Yesu katika uhai wake anamuamrisha afunze kuhesabiwa haki kwa imani na kufutiwa dhambi.
- kwa nini Paulo aliongeza mengi aliposimulia mara hii ya tatu kuliko ilivyosimuliwa zile mara mbili za mwanzo? Ni kwa sababu hapa anasema na Mfalme Agripa. Lakini yafaa tusite na tujiulize: Nini thamani ya shahidi anayetoa ushahidi wake kwa polisi, akaubadilisha kidogo akifika kwa hakimu, na akatoa hadithi nyengine kabisa anapofika mahkama kuu kwa jaji? Hapana awezae kumueleza Paulo alivyo kama alivyojieleza mwenyewe katika barua yake aliyowapelekea Wakorintho. Amesema Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria,) ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. 1 Wakorintho 9.19-22