Ndugu S. Mtsimbe,
Mimi kama mmoja watanzania ambao wangeweza kujiunga na TPN nina machache ambayo ningependa kushauri na kupata ufafanuzi kabla ya kujiunga.
1. Nimepitia tovuti yenu, nimekutana na makosa kadhaa ya wazi ya lugha. Nadhani ni vizuri tovuti hii kwa sababu inawakilisha Tanzanian Professionals basi iwe na utaalamu wa hali ya juu. Napendekeza TPN itafute wahariri wazuri (tunao wengi) ili kuipitia. Mfano mdogo tu (na ipo mingi) mtu akisoma vision ya TPN kwenye ukurasa wa mbele haieleweki mpaka akifungua ukurasa wa objectives, ndio anaelewa. Wageni wenu wakitaka kuijua TPN watataka kusoma Vision. Wakishindwa kuielewa vision, wameshindwa kuielewa TPN.
2. Nashauri pia muwe makini sana na matumizi ya takwimu na taarifa mnazoweka kwenye tovuti. Ikiwezekana muonyeshe vizuri wapi mmepata (vyanzo) takwimu hizo. Kwa mfano, mkisema tanzania ni nchi maskini sana yenye watu zaidi ya "50% below poverty line...", basi mueleze chanzo. Kwa sababu hatuna hakika kama hiyo ndio takwimu sahihi. Na nadhani ni muhimu pia kuzipa takwimu nguvu - zimzungumze zenyewe bila kuweka maneno yoyote yanayoweza kuleta hisia za kuongezea "chumvi".
3. Jingine ambalo yawezekana ni swala la muonjo tu (na hili linaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu) na labda sio muhimu sana ni muonekano mzima wa tovuti hiyo. Kwa mawazo yangu tovuti hii inaonekana kama ya jumuiya kibiashara au klabu zaidi kuliko kitaaluma. Ingependeza kama mngekuwa na vitu vichache sana kwenye ukurasa wa mbele na rangi chache zaidi, kwa maana nyingine kusiwe na makeke mengi sana.
4. Mwisho, ningependa pia kujua umuhimu wa lugha ya taifa katika taasisi hii. Kwa sababu hii imekuwa ni conflict kubwa kwenye taaluma zetu hapa nyumbani na kumezuka mjadala mkali sana kwa miaka mingi wa athari ya lugha ya taifa na ya taaluma mashuleni kwenye maendeleo ya taifa. Na kwa sababu TPN itawajumuisha watu mbali mbali hata wasioweza kuelewa lugha ya kiingereza (kutokana na mission ya TPN). Je, mmefikiria swala hili na je kwa sababu hii ni taasisi ya wataalamu wa kitanzania na kwa sababu moja ya matatizo ya msingi ya watanzania ni wataalamu wetu kutumia mbinu za mataifa mengine kutatua matatizo yetu "local", je si vizuri chombo hiki kikalifanya hilo kuwa moja ya maswala muhimu kwa sababu kwa mataifa mengi yaliyoendelea huko ulaya na Asia ya kusini lugha imekuwa ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi.