Sera iliyotangazwa na serikali ya Marekani ya kupanua vizuizi vya kuingia nchini humo hadi nchi 40 kwa kisingizio cha "usalama wa taifa" imeanza kutekelezwa rasmi kuanzia tarehe mosi, Januari ya mwaka huu mpya wa 2026. Kati ya hizo, kuna nchi 27 kutoka Afrika. “Jino kwa Jino”, Niger na Chad zimejibu kwa kusimamisha kutoa viza mpya kwa raia wa Marekani. Wachambuzi wanasema, mgogoro huu sio tu umefichua tena asili ya sera ya serikali ya Trump kuhusu Afrika, bali pia umeashiria kuwa uhusiano kati ya Afrika na Marekani unaingia kwenye kipindi kipya.
Serikali ya Trump sasa inazidi kutumia viza kama mbinu, kuanzia "katazo la usafiri kwa Waislamu" wakati wa awamu yake ya kwanza hadi vikwazo vinavyofikia nusu ya nchi za Afrika sasa zikiwemo nchi nne ambazo zilikataa kupokea wahamiaji haramu kutoka Marekani, hatua hizo zimeonyesha umwamba wake. Zaidi ya hayo, serikali ya Trump imesimamisha miradi mbalimbali muhimu ya misaada, hata kufunga Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani, na kusababisha ushirikiano mwingi na Afrika kukatika. Katika nyanja ya biashara, serikali yake imeruhusu Sheria ya Fursa ya Ukuaji wa Afrika AGOA kuingia katika msukosuko, huku ikitafuta kupanua njia za uagizaji wa madini adimu kutoka Afrika. Hatua hii ya kuchukua rasilimali na kukandamiza ushirikiano imepunguza sana uaminifu kati ya Afrika na Marekani.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Afrika imechukua hatua za kurekebisha sera zake. Katika masuala ya nje, nchi za Afrika zimebadilika kutoka "kuvumilia" hadi "kuweka mipango mbadala" na "usawa," ikiimarisha ushirikiano wa ndani ya bara hilo, na kutumia majukwaa mbalimbali kama vile Nchi za BRICS kujenga uhusiano wa ushirika mwingi. Katika masuala ya maendeleo, zimesisitiza kanuni ya kujiamulia mambo, zikiimarisha ujenzi wa eneo la biashara huria la bara la Afrika, kutoa "Dhamana ya Kijani ya Afrika," ili kupunguza utegemezi wa nje; wakati huo huo, ikishinikiza taasisi kama Benki ya Dunia na IMF kuongeza sauti za Afrika, na kukuza mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa. Nchi za Afrika pia zimekuwa macho zaidi kuhusu "diplomasia ya biashara" ya Magharibi ambayo haina ufanisi halisi, na hazitaki tena kuacha mamlaka na maslahi ya maendeleo kwa kutoa ahadi za mdomoni tu.
Sera ya serikali ya Trump kuhusu Afrika imekwama katika sera mbaya za "kuchukua rasilimali" na "mazungumzo matupu ya ushirika," hivyo ni vigumu kujenga uhusiano endelevu kati ya pande hizo mbili. Mwaka 2026, Afrika bado inaweza kupuuzwa kwenye siasa ya nje ya Marekani, lakini bara hili linabadilisha kanuni za mawasiliano ya kimataifa kwa vitendo: kudumisha usawa kama sharti, na faida ya pande zote kama msingi. Kutoka kukubali "kanuni za Marekani" kwa kushinikizwa hadi kutafuta washirika mbalimbali kwa msimamo wa usawa, mabadiliko hayo yanabadilisha kwa kina uhusiano kati ya Marekani na Afrika. Mchakato huu hauhusu tu maendeleo ya Afrika yenyewe, bali pia unadokeza upanuzi wa nafasi ya kujiamulia mambo ya Dunia ya Kusini katika utaratibu wa kimataifa.