Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 04




Kikao kilikwisha kwa pande zote mbili kuelewana, mwenye nyumba alisema baada ya siku tatu mafundi watakuja kwaajili ya kuanza ujenzi lakini pia hapohapo kabla kikao hakijaisha akasisitizia kuhusu kodi yake, hili nililijua tu litakuja, alisema na yeye atapata nguvu zaidi ya kuboresha miundombinu endapo sisi tutatoa pesa zake kwa wakati, baada ya kikao kuisha aliaga na kwenda zake na kila mtu akaendelea na shughuli zake, angalau sasa na mimi nikapumzika na macho ya yule shemeji, macho ambayo sikuelewa yanamaanisha nini zaidi ya kunitisha.

Zikapita siku mbili, mafundi hawakuja kama tulivyoambiwa, ikapita siku ya tatu na ya nne, hola, mpaka wiki nzima iliyoyoma si fundi wala mhandisi aliyekuja, mwenye nyumba anatupiga tu kalenda.

Siku moja nikiwa niko nyumbani, sikumbuki haswa zilipita siku ngapi tangu tufanye kile kikao, katika majira ya saa saba usiku nikasikia mtu anafungua mlango wake, sikujua ni nani maana mimi nilikuwa ndani sebuleni lakini ni bayana alikuwa ni jirani mmojawapo katika milango ile miwili, kidogo mlango wa grill ulifunguliwa kakaaa-kakaaaa kisha kukawa kimya, nami nikawa kimya nikiwaza huenda mtu anaenda maliwatoni hivyo nikaendelea na mambo yangu ya kutazama runinga.

Nilikaa kama nusu saa lakini sikusikia mlango ule wa grill ukifungwa, na kwa namna yoyote ile mlango ule usingeweza kufungwa bila kutoa sauti, hapo nikapata shaka. Nilitoka sebuleni nikaenda chumbani ili nipate kuchungulia nje kuna nini kinaendelea, nilipofungua pazia la dirisha kwanza nikatazama pikipiki yangu, nikaona kuna usalama, nikaangaza huku na kule lakini sikumwona mtu, nje kulikuwa kimya sana.

Nilitulia kusikiliza labda kuna mtu bafuni, napo sikusikia kitu, kila pembe ilikuwa kimya sana. Hapo nikapata wasiwasi. Niliufungua mlango nikaenda nje kutazama maana ule mlango wa grill kuwa wazi kwa muda wote huo haikuwa salama kabisa ukizingatia tulinusurika kupigwa tukio mara ya mwisho, huko nje nikatazama upande wa magharibi, hamna mtu, nikatazama upande wa mashariki nao hamna mtu, kabla ya kurudi ndani nikaenda kule bafuni, bafu zote zilikuwa zimezimwa taa hivyo nikahitimisha hamna mtu humo, basi nikarejea mlangoni na kuurejeshea ule mlango wa grill pasipo kuufunga na ufunguo ili kama kuna mtu huko nje basi ataingia na kuufunga mwenyewe, mimi nikareja sebuleni nikaendelea kutazama televisheni.

Nilitazama mpaka nilipohisi naelemewa na usingizi ndipo nikaenda zangu chumbani, huko nikajilaza na kuskilizia lakini muda wote huo sikusikia mlango wa grill ukifunguliwa, kulikuwa ni kimya tu kama hapo awali, nikajiuliza nini kinaendelea au ni mimi ndo' mwenye matatizo? Mpaka napitiwa na usingizi sikupata kusikia kitu, asubuhi palipokucha wakati naenda kuoga niende kazini, pale bombani, nilikutana na jirani yangu wa mlango mwingine ndani ya ile nyumba kubwa, mwanamke huyo alikuwa anafua nguo zake hapo nje, wanawake hawa huwa wana utaratibu wa kuamka mapema kufua kwaajili ya kuwahi kamba, baada ya kunisalimu aliniuliza,

"Shemeji, ni wewe ndo' uliacha mlango wa grill ukiwa wazi jana usiku?"

Nikamweleza namna mambo yalivyotokea kuwa mimi sikuuacha wazi bali niliurejeshea tu baada ya kusikia mtu alitoka, ajabu akaniambia kuwa mumewe asubuhi ya mapema sana alipotoka aliukuta mlango ukiwa wazi kabisa, umeachama kama mdomo! Nikastaajabu kusikia hayo, nilijiuliza ni muda gani mlango ulifunguliwa lakini sikupata majibu, nikaenda zangu kuoga nikilenga kuwa siku n'takayokutana na BIGI nimuulize kuhusu jambo hilo, sikuwa najua ni lini ila nilitumai ndani ya wiki hiyo basi nitambahatisha.

Ikapita siku mbili, sikumwona BIGI wala mkewe, siku ya tatu yake nikiwa sebuleni majira yangu ya usiku mtulivu, siku hiyo sikuwa natazama televisheni bali namalizia kazi fulani kwenye laptop, nikasikia mtu akiufungua mlango na kisha akaufungua mlango wa grill kakakaaa-kaaakaa, nikakaa tenge, mara hiyo sikutaka kupuuzia nilinyanyuka upesi nikaenda chumbani kutazama, ile kufungua tu pazia nikamwona mtu akiishia kwa kulifunga geti dogo, sikumjua mtu huyo ni nani kwani nilichoambulia kukiona ni mkono tu tena kwa muda mchache mno, basi nikabaki hapo nikiendelea kutazama pengine nitaona kitu.

Ngoja lakini wapi! Nilitumia kama nusu saa hapo lakini sikuona kitu nami nilikuwa nina hamu sana ya kumwona mtu huyo kwani niliamini yeye ndiye yule aliyeacha geti wazi siku ile, nilitamani kujua anafanya nini muda huo na kwanini anaacha geti wazi?

Nilikaa hapo dirishani kwa muda mrefu pasipo kuona kitu nikakata shauri kwenda nje, nilipoufungua mlango wangu kudaka korido nilisikia sauti ya watu wakizungumza, nikasita nikiskiliza. Sauti hiyo ilikuwa inatokea kwenye chumba cha BIGI na nilipoisikiliza kwa kitambo kidogo tu nilibaini sauti hiyo haikuwa ngeni masikioni mwangu, nilishawahi kuisikia mahali, ila ni wapi?

Kidogo kuwaza nikaikumbuka, sauti hii ilikuwa ni ileile niliyoisikia siku ile kwenye mlango huuhuu nikajua ni ya televisheni, ina maana imejirudia au ni masikio yangu? Nilistaajabu, lakini kadiri nilivyoisikia sauti hiyo tena na tena, tena kwa umakini, nikaamini kabisa haikuwa sauti ya televisheni, sauti hiyo ilikuwa ya watu wanaozoza na kunong'ona kitu ambacho sikuwasikia vema nikaelewa.

Nikiwa naendelea kuskiza hapo, mara nikasikia kishindo cha hatua za mtu kibarazani alafu mlango wa grill ukafunguliwa kakaaa kaakaaa! Nikashtuka kweli kweli, ni kama vile moyo wangu uliruka pigo moja kwa fujo!

Upesi nilirejea karibu na mlango wangu nikayatupa macho kule langoni, punde nikamshuhudia BIGI akiingia ndani huku amebebelea kiroba kitupu mkononi, huku juu amevalia 'vest' yake ileile aliyokuja nayo wakati mke wake anaumwa, aliponiona alisimama akan'tazama, nahisi na yeye alishtushwa na uwepo wangu pale, alinitazama pasipo kusema kitu chochote ila mimi nikamsalimu, hakujibu, alisimama tu akiendelea kun'tazama, sijui alikuwa anawaza kitu gani, mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanapiga kwa kasi sana, niliona ni busara kuingia ndani kwangu upesi nikaufunga mlango kwa funguo kisha nikasimama hapo kusikiliza, kimya, nlidhani nitasikia vishindo vya miguu vikijongea lakini sikusikia chochote zaidi ya sauti ya mlango ukifungwa kisha kukawa kimya tena.

Nilizima kila kitu changu nikaenda chumbani moja kwa moja mpaka dirishani. Nilitazama pale kibarazani nikaona mlango wa grill ukiwa wazi. Nilitamani kwenda kuufunga lakini nikawaza vipi kama bwana yule akawa bado hajamaliza shughuli zake? Nikaona ni stara nikitulia lakini niendelee kungoja kama atatoka tena.

Nilingoja hapo kitandani kwangu mpaka usingizi ukanibeba, sikusikia kitu abadani. Kesho yake niliporejea tu kazini nikaelezwa kulitokea mjadala mkubwa hapo nyumbani juu ya swala la mlango wa grill kuachwa wazi kwa mara nyingine tena usiku ulopita, siku hiyo majira ya saa tatu hivi usiku kama sijakosea, nilikutana na jirani yangu yule wa dukani tukaongea mambo kadhaa kuhusu hapo nyumbani, moja kuhusu swala la ujenzi wa uzio na namna ambavyo mwenye nyumba haeleweki, na pili kuhusu swala la mlango wa grill kuachwa wazi nyakati za usiku. Bwana huyo alikuwa ndo' mtu wa kwanza kutoka asubuhi hivyo yeye ndiye aliyekuwa anaukuta mlango huo ukiwa wazi.

Kwa upande wangu nilimweleza yale niliyoyajua ya kuwa bwana BIGI ndiye anayeacha mlango huo wazi na basi kwa pamoja tukaazimia kumwambia endapo yeyote akipata nafasi hiyo. Siku zikapita, sijui kama yeye alifanikiwa kuonana na jamaa lakini mimi sikufanikiwa na uzuri mlango haukuachwa wazi tena.

Nakumbuka siku ambayo mafundi walikuja kwaajili ya ujenzi ndo siku ambayo nilipata kumwona bwana BIGI. Siku hiyo ilikuwa ni usiku kama wa saa nane hivi kama niko sawa, nilikuwa sebuleni kama kawaida yangu kabla ya kwenda kulala, televisheni inaongea lakini akili yangu yote ipo kwenye simu naperuzi mitandaoni, naingia instagram, whatsapp na JamiiForums.

Nilisikia mlango unafunguliwa na kisha mlango wa grill, nikanyanyuka kwenda kutazama dirishani. Hapo nilimwona BIGI akiwa amebebelea kiroba begani mwake anatoka kwenda geti dogo.

Kwasababu za ujenzi, geti hilo lilikuwa wazi tena limeegeshwa pembeni kabisa hivyo unaweza kuona mpaka nje. Nikamwona mtu huyo akitokomea huko mpaka kiza kikammeza!

Niliendelea kukaa hapo kwa muda kidogo lakini sikumwona akirudi, nikajua ni kama kawaida sitamshuhudia mpaka nitakapolala, lakini siku hiyo hali ilikuwa tofauti, baada ya kurudi kule sebuleni na kukaa kwa dakika kadhaa nilisikia kishindo cha mtu akikatiza koridoni alafu sauti ya mlango ikaita, nikawaza moja kwa moja atakuwa BIGI ndo amerejea lakini kwanini haufungi mlango wa grill? Nikaazimia ningoje kidogo hapo na nikiona kimya basi nitatoka nikaufunge mlango huo mwenyewe.

Kweli nilikaa hapo kwa kama nusu saa hivi, kimya, nilienda chumbani kutazama dirishani, hali ilikuwa shwari, nikauendea mlango wangu kuufungua lakini nilipotekenya tu funguo nikasikia mlango mwingine unafunguliwa, nikatulia kuskiza.

Vishindo vilipita koridoni nikahisi na kuamini kabisa alikuwa ni BIGI, vishindo hivyo vilipofifia nikaufungua mlango na kuchungulia nje, kweli alikuwa BIGI, nilimwona anatoka nje ya uzio akiwa na kiroba chake begani. Sikujua alikuwa anabebelea kitu gani humo lakini kilichonitatiza zaidi ni kwanini alikuwa anafanya zoezi hilo usiku wa manane?

Nilitoka nikatembea kwa upesi lakini pia kwa uangalifu mpaka kwenye geti dogo. Hapo nilirusha macho yangu kule kutazama, kwa mbali kwa msaada wa mataa mengine ya kule nje, nikamwona BIGI akiwa anayoyomea kuelekea kule korongoni, kule ambapo ndiyo wezi wanapokimbilia. Mwendo wake ulikuwa wa haraka sana na kwasababu ya uweusi wake basi kiroba ndo kilikuwa kinaonekana kikikata upepo, kile kinapepea, kilee kinapepea!

Niliijikuta nina hamu ya kwenda zaidi kutazama.


***
Inatisha jamani
 
Yule Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida ~ 05




Tangu ujenzi wa uzio ulipoanza niliongeza zaidi umakini wangu kwenye kutazama usalama wa nje ya nyumba kwasababu geti lile dogo lililokuwa hapo sasa halikuwapo tena kwenye kingo za ukuta, badala yake lilikuwa linaegeshwa na kuondolewa, hivyo mtu asipoliegesha basi ndo tunakaa wazi kama behewa kitu ambacho kwangu kilikuwa na hatari sana maana usafiri wangu ulikuwa unakaa karibu na geti hilo. Yeye mwenye nyumba alisema anataka kuleta geti jingine, lile la zamani lisirudishwe, lakini kwa siku tatu mfululizo hakuleta geti hilo, hata mafundi wenyewe walikuwa wanalalamika hawajalipwa pesa zao, mara kadhaa walikuwa wanasaidiwa kupewa chakula na wapangaji.

Sijawahi kujua kwanini wenye nyumba wanakuwaga wagumu mno kufanya marekebisho ya mapango yao, yani mikono yao imezoea kupokea na kuchuma tu, kwenye kutoa wanaona kama vile hawastahili, yaani wanaumiaaaa.

Turudi kwenye usiku ule. Baada ya BIGI kupotelea kule kizani nilijazwa na hamu ya kwenda kutazama kule korongoni anapoenda. Nilijiuliza mara mbilimbili nikaona haitakuwa vema kwani nikitoka pale na kuacha geti dogo wazi kiasi kile nitakuwa nimejiweka matatani kiusalama, haswa wa pale nyumbani, hivyo nikaona kheri nibakie palepale kungoja lakini kwasababu sikutaka bwana yule anione kuwa namtazama nilienda zangu maeneo ya bafuni, huko kulikuwa na kiza sababu ya taa haikuwashwa, nikajibanza hapo kiubavu kutazama geti dogo.

Yani kama sekunde nne tu yule bwana akawa ametokea getini, Ilibakia kidogo tu angeniona maana ilikuwa ni upesi mno kiasi cha kunishangaza, alipoingia alitazama huku na kule, huku na kule, alafu akaufuata mlango wa grill lakini alipoufikia mlango huo, kabla hajaingia, alifanya jambo ambalo lilinifanya nihisi huenda aliniona. Alisimama hapo akitazama upande ule wa bafuni kwa kama dakika tatu pasipo kupepesa, moyo wangu ukawa unaenda mbio sana. Sikumchukulia bwana yule kama mtu wa kawaida tena bali kama dubwana lililopo mbele yangu katika mawindo yake.

Nilitulia kadiri nilivyoweza, alipotosheka akaingia ndani na kisha akaufunga mlango ule wa grill kwa funguo, kitu ambacho siku zingine huwa hakifanyi, mimi nikaachwa pale nje nisijue nini cha kufanya.

Nilikaa nikawaza niugonge mlango wa grill? Hapana, nikiugonga maana yake yule bwana atajua nilikuwa nje namfuatilia nami sikutaka kumthibitishia hilo, basi nikaona cha kufanya niendee dirisha la chumba changu, japo lipo juu, nihangaike nalo kuwaita waliomo ndani wapate kunisaidia, wakati nashuka ngazi mara nilisikia sauti ya kiume ikifoka:

"Wewe nani?"

Nilishtuka sana. Niligeuka kutazama sauti inatokea wapi nikabaini ni kwenye dirisha la yule jirani yangu mwenye duka, hapo dirishani alikuwa amesimama mtu aliyeshikilia pazia kutazama nje. Kabla sijajibu kitu, mtu huyo alinitambua akasema,

"Aah kumbe ni wewe, kaka! Vipi tena huko nje mida hii?"

Nikamdanganya nilienda maliwatoni lakini kwa bahati mbaya kurudi nikaukuta mlango umefungwa, basi kwa kunisaidia alitoka ndani kwake kuja kunifungulia.

Alinijulia hali na kidogo kwa kama dakika mbili hivi tukawa na mazungumzo mafupi. Aliniambia alisikia mtu anaufungua mlango wa grill kwenda nje, akaniuliza nilikuwa ni mimi?

Kabla sijamjibu nilitazama kwanza kwenye korido kisha nikamweleza kwa sauti yangu ya chini kuwa aliyeufungua mlango huo ni BIGI, mimi nilitoka hapo baadae kwenda maliwatoni ndipo nikaukuta tayari ameshaufunga. Sikutaka kumwambia kuhusu yale ya korongoni wala ya kujificha bafuni.

Nilipomjibu hayo naye alinieleza kuwa muda wote huo alikuwa akimshuku bwana huyo kuwa ndo' anaacha mlango wazi lakini hakuwa na uhakika, zaidi aliniambia anahisi kuna jambo haliko sawa kumhusu bwana yule kwani kuna mambo ambayo amemshuhudia yakamwacha mdomo wazi.

Hakutaka kunieleza mengi kwasababu wasaa haukuwa unaruhusu, tulikubaliana tutakapoonana na tukiwa na muda basi tutayajenga. Aliniaga akaenda zake na mimi nikaenda zangu.

Wiki iliyokuja nilipata safari ya siku tatu ya kwenda Tabora, wilaya ya Igunga, kwasababu ya msiba wa mmoja wa jamaa yetu wa kazini ambaye alifiwa na mama yake mzazi. Safari hiyo ndefu ilikomea kwenye kijiji fulani ambacho sikikumbuki jina ila ninachokumbuka nyumba ambayo tulifikia haikuwa mbali sana na shule moja ya sekondari inayoitwa Mwamashiga, huko hapakuwa na mtandao wa simu wala umeme, ni nyumba chache chache ndo' zilikuwa na taa zinazotumia nishati ya jua kwahiyo sehemu kubwa ilikuwa kizani nyakati za usiku.

Muda wote nikiwa huko sikuweza kutumia simu yangu kwaajili ya mawasiliano, simu iligeuka kuwa 'toy' la kuchezea game ama kukokotoa hesabu. Nilikuja kupata mawasiliano siku tulipotoka huko kijijini njiani kuelekea Igunga mjini, kitu kilichonifanya nikajua kuwa mtandao umerudi ni ujumbe ulioingia kwenye simu yangu; ujumbe kutoka Airtel kuwa kifurushi changu kimeisha, baada ya ujumbe huo nilipokea ujumbe mwingine toka kwenye namba ngeni ukisema (nanukuu):

"Kaka ukirudi nyumbani fanya tuonane upesi, nimejaribu kukutafuta kwa simu sikupati. Tarimo."

Nilijiuliza ujumbe huo umetokea wapi lakini baada ya punde ya kuwaza na kuunganisha matukio nilipata jibu langu, aliyetuma ujumbe ule alikuwa ni jirani yangu mwenye duka, yeye ndiye Tarimo na mara ya mwisho mimi kuonana naye alitaka tuongee tukipata nafasi.

Nilijaribu kumtafuta hewani pasipo mafanikio, si kwamba alikuwa hapatikani, lah, mimi sikuwa na salio. Nilicheki pia kwenye AirtelMoney lakini napo hola, hapakuwa na kiasi cha kunitosha kumpigia, ilinilazimu niwe mpole mpaka nitakapopata sehemu rafiki ya kununua vocha.

Wakati huo nilikuwa nawaza sana kuwa ni nini ambacho Tarimo alikuwa anataka kuniambia kwa dharura hiyo lakini pia nikajikuta nayakumbuka na kuyawaza yale ya kule nyumbani, kwa muda huo nikawa katika ulimwengu wangu wa pekee, nilikaa na watu lakini nilijihisi niko mwenyewe kabisa.

Tulipofika Igunga mjini gari lilisimama ili tupate mahitaji muhimu mathalani maji maana kuna watu walishindwa kunywa maji ya kule kijijini, maji yao ni ya kuchimba chini na kuyahifadhi kwenye ndoo, maji hayo ukiyatazama kwa haraka unaweza dhani ni chai nyepesi ya maziwa na ladha yake si kama maji uloyazoea, hapo ndipo na mimi nilipata mwanya wa kununua vocha nikapiga simu kwa Tarimo huku nikiomba apokee upesi maana simu yangu ilikuwa taabani kwa kuishiwa na charge, muda wote ambao nilikuwa kule sikuwahi kuicharge na kama matumizi yangekuwa makubwa basi bila shaka ingeshalizima muda mrefu sana.

Kidogo Tarimo alipokea simu nikamsalimu na kumweleza kuwa nimepata ujumbe wake na nilikuwa mbali mahali ambapo mtandao unasumbua, basi akanipa pole na kunitaka nikifika Dar Es Salaam nionane naye mara moja kwani kuna jambo alitaka kunishirikisha kabla hajachukua hatua zingine. Nakumbuka kauli yake moja akisema,

"Kaka, tufanye juu chini huyu jamaa aondoke hapa nyumbani kama tunataka kuwa salama."

Basi kwasababu tulishapangiana kuonana, nilikata simu na kuwatafuta watu wangu wengine wa karibu ili nipate kuwajulia hali maana sikuwa hewani kwa kitambo kidogo na sikutaka simu izime kabla sijateta nao, baada ya hapo haikupita muda mrefu simu ikazima nikabaki mpweke, wengi niliokuwa nao ndani ya gari sikuwa nafahamiana nao zaidi tu ya mfiwa na majamaa wawili wa kutoka kazini, nao walikuwa wameketi mbali na mimi.

Sikudumu muda mrefu nikapitiwa na usingizi mzito kwelikweli kwani kwa muda niliokuwa kule kijijini sikupata kulala vema, mahali pa kulala hapakuwapo, ni mara chache ndo' ningejibanza sebuleni majira ya mchana pale kwenye kochi nikalala huku nimeshika tama, usingizi wa mlinzi, hivyo nilivyotulia kwenye kiti cha basi na huku upepo unanipuliza sikuweza kuvumilia kabisa, macho yalinishinda vita.

Nilifika Dar majira ya jioni, kabla ya kunyookea nyumbani nilipitia kazini ili niuchukue usafiri wangu ambao niliuacha huko kwasababu ni salama zaidi kuliko kule nyumbani ambapo niliacha bado ujenzi unaendelea, baada ya hapo nilinyookea nyumbani na nilichokifanya baada ya kufika tu nilimpigia simu bwana Tarimo kumwambia kwamba nimewasili, bwana huyo akaniambia yuko mbali kidogo kuna mtu alimpelekea mzigo maeneo ya Mbweni lakini akitoka huko atanipigia na kunipa muafaka, basi nikangoja, wakati huo nikautumia kwenye mambo yangu mengine ya hapa na pale.

Mpaka inafikia saa nne usiku bwana Tarimo hakuwa amenitafuta, si kwa ujumbe wala kupiga, na mimi sikuona haja ya kumtafuta maana aliniambia atanijuza yeye hivyo nikatulia kungoja nikiamini atakuwa ametingwa na mambo yake ya kikazi, muda ukaenda na kuenda.

Kwenye majira ya saa tano ya usiku, nikiwa nimepumzika sebuleni, ndipo nilisikia watu wakiwa wanazungumzazungumza huko nje, haswa wanawake, katika mtindo wa zogo fulani hivi na mimi sikuwa nayasikia maneno yao wanayoyasema.

Lakini ghafla katika zogo hilo nilisikia ukunga uuuuuuuuuwiiiiii! Uuuuuuuuuwiii! Nikapata mshtuko. Kidogo nikiwa hapo, bado sijafanya kitu, mlango uligongwa na nilipoufungua nilikutana na mwanamke mmoja ambaye anakaa kwenye zile nyumba za nje, mwanamke huyo aliniambia kuwa amepata habari toka kwa mke wa yule jirani yangu wa dukani, yaani mke wa bwana Tarimo, ya kwamba bwana huyo amepata ajali mbaya ya pikipiki maeneo ya Kunduchi, mbuyuni, kwenye mataa.

Nikaduwaa.

Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida
 
Back
Top Bottom