TUJIKUMBUSHE
Januari 9, 2008
Kupitia taarifa inayotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, Rais Jakaya Kikwete anatangaza kutengua uteuzi wa Balali kuwa Gavana na kuagiza hatua zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na ubadhirifu uliogunduliwa kwenye EPA. Anamteua Beno Ndullu kuwa Gavana mpya wa BoT.
Januari 7, 2008
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anamkabidhi Rais Kikwete ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Ernst & Young.
Desemba 23, 2007
Kampuni ya Ernst & Young inakabidhi ripoti ya uchunguzi wake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, ambaye anaahidi kuifikisha kwa rais katika wiki ya kwanza ya mwaka 2008.
Desemba 20, 2007
Inaripotiwa kuwa Gavana Balali ameandika barua ya kujiuzulu akiwa nje ya nchi, Ikulu na Wizara ya Fedha zinasema kuwa hazina taarifa.
Desemba 19, 2007
Meghji anatetea kuchelewa kwa ripoti ya BoT.
Desemba 4, 2007
Freeman Mbowe anafungua Mkutano wa Baraza Kuu la CHADEMA na kueleza kushangazwa na ukimya wa serikali kuhusu ripoti ya uchunguzi wa ubadhirifu ndani ya BoT.
Desemba 01, 2007
Dk. Willibrod Slaa anaelezea kukerwa na usiri wa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za BoT.
Novemba 29, 2007
Ukaguzi wa hesabu za BoT unakamilika na inaelezwa ripoti hiyo kufika kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Septemba 22, 2007
Wafadhili wanadai ufafanuzi wa tuhuma za ufisadi zinazoihusu BoT.
Septemba 20, 2007
Hali ya Gavana Balali inaripotiwa kuendelea vizuri.
Septemba 16, 2007
Wananchi wataka msimamo wa tuhuma za BoT na nyinginezo kutoka kwa Rais Kikwete.
Septemba 15, 2007
Dk. Slaa anahutubia mkutano wa hadhara Mwembe Yanga, Temeke, kisha anataja orodha ya waliowaita mafisadi wanaotafuna nchi, akimjumuisha na Balali.
Septemba 14, 2007
Afya ya Gavana Balali inagubikwa na utata, lakini inaelezwa kuwa yuko nje ya nchi kwa matibabu.
Septemba 11, 2007
Kampuni ya Ernst & Young iliyoteuliwa kupitia hesabu za BoT katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ili kubaini ukweli kuhusu ubadhirifu wa fedha, inaanza kazi.
Septemba 09, 2007
Inaripotiwa kuwa hali ya Gavana Balali si nzuri, hivyo amepelekwa nje ya nchi kwa uchunguzi na matibabu.
Agosti 19, 2007
CHADEMA inajibu mapigo ya Spika dhidi ya Slaa na hoja ya BoT.
Agosti 18, 2007
Spika anamtuhumu Dk. Slaa kuwa ameghushi nyaraka alizotaka kuzitumia dhidi ya BoT na kutishia kumshitaki.
Agosti 16, 2007
Dk. Slaa anachomoa hoja binafsi ya BoT bungeni akidai kuwapo kwa dalili za kukosekana kwa nia njema, hasa baada ya Mbunge mwenzake, Zitto Kabwe, kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge baada ya kuwasilisha hoja yake iliyokataliwa na wabunge wa CCM. Anaahidi kuipeleka kwa wananchi na kwa wafadhili, lakini pia anadai kutishiwa maisha.
Agosti 12, 2007
Yaelezwa kupitia katika vyombo vya habari kuwa Balali anapaswa kustaafu kazi Juni mwaka 2008, kitakapokwisha kipindi chake.
Agosti 6, 2007
Dk. Slaa awasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka Bunge liunde kamati teule kuichunguza BoT.
Julai 26, 2007
Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi yapitisha mahesabu ya BoT ya mwaka 2005/2006, baada ya kuridhishwa na majibu ya Gavana Balali.
Julai 13, 2007
Wapinzani watoa hoja za kumshangaa Balali na kusisitiza hoja za kumtaka ajiuzulu.
Julai 12, 2007
Gavana Balali aitisha mkutano na wanahabari na kupinga shinikizo la kumtaka ajiuzulu kwa manufaa ya umma akisema hatajiuzulu kamwe, kwani hakufanya kosa lolote.
Julai 12, 2007
Balali anapunguziwa mzigo, rais anateua manaibu gavana watatu kumsaidia.
Julai 9, 2007
Viongozi wakuu wa vyama vinne vya upinzani vya NCCR Mageuzi, CHADEMA, TLP na CUF wazungumza na wanahabari na kueleza wasiwasi wao kuwa serikali inamlinda Gavana Balali dhidi ya kashfa anazokabiliwa nazo.
Julai 2, 2007
Waziri Mkuu ahitimisha mjadala wa ofisi yake bungeni na kukiri kuwa tuhuma za BoT ni nzito na kueleza dhamira ya serikali kutumia kampuni ya kimataifa kuzichunguza na kuzitolea majibu.
Aidha awataka wapinzani Hamad Rashid na Dk. Slaa kuachana na hoja ya kutaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge.
Juni 29, 2007
Serikali kupitia kwa Waziri wa Madini na Nishati inamsafisha mke wa Gavana Daudi Balali, aitwaye Anna Mug anda, kuhusu tuhuma za yeye kutumia nafasi ya mumewe na kisha kuwa mkurugenzi katika moja ya makampuni ya madini ya dhahabu hapa nchini.
Juni 28, 2007
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed, aliambia Bunge kuwa kiasi cha dola milioni 800 kimepotea BoT na kueleza kushangazwa na hatua ya serikali kupinga Bunge kuunda kamati teule.
Juni 27, 2007
IMF inatoa taarifa kupitia kwa Naibu Mkurugenzi wake, Murilo Portugal, ikitaka uwazi uwepo katika suala la kuichunguza BoT.
Juni 26, 2007
Mjadala unatanuka kuhusu tuhuma za ufujaji fedha BoT, na safari hii Mbunge wa CCM, Ole Sendeka, anataka iundwe tume ya kuichunguza BoT, huku Dk. Slaa akisisitiza kuhusu suala hilo katika mjadala wa hotuba ya waziri mkuu.
Juni 25, 2007
Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa anatoa tuhuma nzito za ubadhirifu ndani ya BoT bungeni na kutaka Gavana wa Benki Kuu, David Balali ajiuzulu.
Juni 15, 2007
Bunge la Bajeti linakaa na bajeti ya mwaka 2007/08 inasomwa na Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji.