BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Uongozi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) umetoa ufafanuzi wa changamoto iliyojitokeza katika mfumo wa maegesho ya magari katika jengo la tatu la abiria na kusababisha msongamano wa magari katika uwanja huo.
Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Mhandisi Rehema Myeye changamoto hiyo iliyotokea Novemba 24 mwaka huu saa sita mchana katika njia ya kuingia kiwanjani kupitia geti la Kipawa, ilitokana na kuisha kwa kadi katika mashine ya geti hilo zinazoruhusu kufunguka kwa kizuizi katika mfumo.
Mhandisi Myeye amesema kuwa changamoto hiyo ilirekebishwa ndani ya dakika 30.
“Baada ya hapo magari yaliingia na kutoka uwanjani bila usumbufu wowote, menejimenti ya uwanja inaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza,”amesema.
Myeye ameeleza kwamba hatua stahiki zimeshachukuliwa kwa wahusika waliosababisha kadhia hiyo.
“Tunapenda kuujulisha umma, shughuli katika kiwanja hiki ikiwa ni pamoja na kuingia na kutoka katika jengo la tatu la abiria zinaendelea kama ilivyo kuwa mwanzo,”amesema.
Hata hivyo Myeye alibainisha kuwa kutokana na changamoto hiyo hakukuwa na ucheleweshwaji wa abiria kuingia kwenye ndege wala ucheleweshwaji wa ndege kuondoka.
MWANANCHI