Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA), John Heche amesema Wajumbe wa Sekretarieti ya zamani ya CHADEMA waliojiondoa kwenye Chama hicho hawajabaguliwa kama wanavyosema bali kilichowaondoa ni nongwa baada ya Mwenyekiti mpya Tundu Lissu kuunda Timu yake ya uongozi na kutowapa nafasi Viongozi hao wa muda mrefu.
Akiongea akiwa katika eneo la Nkwenda Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera leo May 08,2025, Heche amesema “Hawa Jamaa zangu waliozungumza jana hakuna miongoni mwao amewahi kuwa Kiongozi wa kuchaguliwa kwenye Chama chetu kwenye ngazi yoyote, wamekuwa Makao Makuu ya Chama Wazungu wanasema as long as i can remember kwa miaka zaidi ya 20, sisi tukipigana hapa ruzuku ikipatikana wao wanalipwa, hawajawahi kufanya kazi ya bure, Viongozi wote wanafanya kazi ya kujitolea lakini wao hawajawahi kufanya kazi ya bure”
“Umeingia uongozi mpya umechagua Viongozi wengine kwasababu Chama hiki ni kikubwa, hata anapoingia Rais si anaandaa Baraza lake la Mawaziri anaweka jingine, Lissu ameingia ameunda Baraza lake la Mawaziri jipya, imekuwa nongwa”
“Ooh Chama hiki kuna ubaguzi, si muliwasikia jana?, tunabaguliwa, unabaguliwaje?, hawasemi , kubaguliwa ni kwamba wao hawajapewa nafasi wamepewa Wana CHADEMA wengine huo eti ndio ubaguzi”
“Ooh Chama hiki kinasema no reforms no election kwahiyo sisi hiyo ajenda tunaipinga sio ajenda ya nchi, nani miongoni mwenu hapa Nkwenda ambaye anasema leo tukienda kwenye uchaguzi jinsi ulivyo tunaweza kupata Mbunge au Diwani nani anasema hivyo? “