Kikundi cha Mawaziri cha Jumuiya ya Madola (CMAG) kimeihimiza Serikali ya Tanzania kuongeza juhudi na kasi katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari, kuendesha mashauri ya kisheria kwa uwazi, na kuweka mifumo inayowajibika ya kutoa fidia kwa walioathirika na migogoro ya kisiasa.
Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Dharura wa 74 wa CMAG (CMAG74) uliofanyika tarehe 20 Septemba 2026 jijini New York, Marekani, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa.Ikiwasilisha msimamo wake rasmi, CMAG ilirejelea masharti manne yaliyowekwa katika Mkutano wake wa 71 wa Desemba 2025 na matarajio yenye muda maalum wa utekelezaji ya Mkutano wa 73 wa Julai 2026.
Ingawa kamati hiyo ilipongeza hatua zilizopigwa katika baadhi ya maeneo, ilibainisha kuwa mambo muhimu ya kikatiba, haki za binadamu, na demokrasia bado yanahitaji kufanyiwa kazi kwa kina zaidi.
"Huku ikikiri maendeleo katika maeneo fulani, CMAG imesisitiza haja ya kazi zaidi ili kuendeleza mchakato jumuishi na unaoaminika wa vyama vya siasa; ulinzi wa uhuru wa kiraia, kisiasa na vyombo vya habari; taratibu za haki, za wakati na za uwazi za kisheria katika kesi zinazoendelea; pamoja na taratibu zinazoaminika za uwajibikaji, urekebishaji na fidia stahiki kwa walioadhirika", imeeleza CMAG.
Ikumbukwe kuwa Julai 10, 2026, Serikali ya Tanzania ilipewa siku 30 CMAG kutatua suala la kuzuiliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Tundu Lissu kupitia njia za kisiasa na kisheria, na kuwaachia huru watu wengine wanaoshikiliwa kwa sababu ya kutumia kile kilichotajwa na Jumuiya hiyo kama haki zao kwa amani.
Aidha, CMAG ilitaka pia kufanyika kwa jukwaa la mashauriano linaloshirikisha vyama vyote vya siasa Tanzania ndani ya siku 90 ili kujadili mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ushindani wa kisiasa, masuala ya mahabusu na uwajibikaji, na ndani ya siku 60 irejeshe uhuru kamili wa matumizi ya mitandao ya kijamii.
CMAG ilitaka pia kuondolewa kwa vikwazo vinavyohusu uhuru wa kukusanyika, kujieleza, shughuli za asasi za kiraia na vyombo vya habari, kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa kati ya vyama, pamoja na kuwepo kwa uwajibikaji kwa wahusika wa matukio ya vurugu na fidia kwa waathirika pale inapostahili.
Mkutano wa karibuni wa CMAG uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulaya wa Malta, Chris Fearne, ukihudhuriwa pia na Makamu wa Waziri Mkuu wa Samoa, Mulipola Anarosa Ale Molioʻo, pamoja na mawaziri na wawakilishi kutoka nchi za Antigua na Barbuda, Botswana, Canada, Grenada, Malaysia, Mauritius, na ZambiaKatika mkutano huo, CMAG ilikuwa na majadiliano na Ujumbe wa Tanzania uliowakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa John Palamagaba Kabudi.
CMAG ilitambua na kupongeza ushirikiano wa Tanzania na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu, mashauriano ya hivi karibuni na vyama vya siasa, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuelekea maridhiano ya kisiasa visiwani Zanzibar kama msingi mzuri wa ujenzi wa maendeleo zaidi.
Ili kuendeleza mchakato huo wa mashauriano, CMAG imeihimiza Serikali ya Tanzania kuweka tarehe ya mapema kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola ili kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wadau wengine wa kisiasa.
Kutokana na tathmini ya jumla, Kamati hiyo imekubaliana kuendelea kuibakiza Tanzania kwenye Agenda yake Rasmi. Hatua hiyo inamaanisha kuwa Tanzania itaendelea kufuatiliwa na CMAG, huku kundi hilo likitarajia maendeleo zaidi katika maeneo yaliyotajwa.
Kabla ya kuanza kwa ajenda za mkutano huo, wajumbe wa CMAG walikaa kimya kwa dakika moja ili kutoa heshima zao kufuatia kifo cha Hafidh Ameir Hassan, aliyekuwa mume wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyefariki dunia tarehe 7 Septemba 2026.
Kamati hiyo ilisisitiza tena utayari wake wa kulinda na kukuza misingi mikuu ya kisiasa ya Jumuiya ya Madola kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Jumuiya hiyo (Commonwealth Charter) kupitia Mfumo wa Huduma Njema wa Katibu Mkuu.
Kikao kijacho cha kawaida cha CMAG kinatarajiwa kufanyika Novemba 2026 nchini Antigua na Barbuda, pembeni ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), ambapo kundi hilo pia litawasilisha taarifa yake ya kila baada ya miaka miwili kwa wakuu wa Serikali.