Jabali la Siasa
JF-Expert Member
- Jul 10, 2020
- 2,823
- 2,466
====
Uamuzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kumtunuku shahada ya udaktari wa heshima Rais Samia Suluhu Hassan ni uamuzi sahihi sana kwa vigezo vingi pamoja na kwamba umekuja kwa kuchelewa,
Kawaida huwa kunakuwa na sababu mahususi inayoongoza ambayo kimsingi huwa 'legacy' ya Kiongozi husika.
Mfano ulio wazi sana ni Jitihada za Rais katika kuinua nafasi ya mwanamke katika teuzi na utekelezaji wa sera zenye kumgusa zaidi mwanamke kwa kiwango ambacho kimevunja rekodi.
Kwamba katika muda mfupi wa uongozi wake, wanawake wamepata nafasi nyingi zaidi za kisiasa na kiutendaji ndani ya Serikali. Lakini pia katika kipindi kifupi cha uongozi wake, sera zinazogusa mwanamke kama Elimu, Maji, Afya na Kilimo zimepewa uzito mkubwa kibajeti.
Mkakati wa kuinua nafasi ya mwanamke ni mkakati wa kujenga Taifa kubwa.Tafiti zinaonesha kuwa mwanamke akipewa fursa sawa na mwanaume, itachangia zaidi ya $28trilioni kufikia mwaka 2025 kwenye uchumi wa dunia. Kiasi hiki ni karibu sawa na asilimia 30% ya uchumi wa dunia sasa( Mckinsey, September 2015).
Pia tafiti zinaonesha kwamba kumwezesha mwanamke kuna faida kubwa kwa familia kwani asilimia 90% ya kipato anachopata mwanamke kinatumika kwenye familia kulinganisha na asilimia 35% ambayo mwanaume anarudisha kwenye familia (UNAC).
Na zaidi , tafiti zinathibitisha uhusiano mkubwa wa ufanisi kitaasisi na ongezeko la nafasi ya mwanamke. Ripoti ya Women count 2020 inaonesha kwamba kati ya kampuni 350 kwenye soko kubwa la mitaji duniani la ( London stock Exchange), ni kati 14 tu zilizokuwa zikiongozwa na wanawake na kampuni ambazo walau theluthi moja ya uongozi imeshikwa na wanawake ilionekana kupata faida mara10 ya kampuni ambazo hazikuwa na wanawake.
Hivyo usawa wa kijinsia katika uongozi una nafasi muhimu sana katika ufanisi wa kitaasisi. Ndio maana ripoti ya OxfordReview , vol1- 2014, ilionesha kwamba kwenye mataifa 13 makubwa kiuchumi duniani, ufanisi wa taasisi unachangia 25% ya utajiri wa Taifa husika. Mbali na kuwawezesha kwenye nafasi, pia ameteleza agenda zinazogusa kuinua nafasi ya mwanamke kama afya, kilimo, elimu na maji. Inafahamika kwamba bajeti ya kwanza ya maji chini ya awamu ya sita 2021/22 ni kubwa kuliko bajeti yoyote katika miongo miwili na mwendelezo ni huo katika bajeti ya pili 2022/23.
Maji ni afya na unapogusa afya unagusa zaidi mama na mtoto. Ripoti ya WHO- 2014 inaonesha kwamba katika kila dola1 inayowekezwa kwenye maji inaokoa dola 4.2 zingezotumika kutibu magonjwa yatokanayo na ukosufu wa maji safi na salama.
Ripoti ya USAID 2014, ilionesha kwamba wakati mnyororo wa kilimo katika dhana pana( mazao, mifugo, uvuvi, na misitu) Tanzania kinaajili zaidi ya asilimia 65 ya watanzania, asilimia 70 yao ni wanawake.
Maamuzi ya Rais kuongeza bajeti ya kilimo kwa zaidi ya mara mbili ina mchango mkubwa sana kwenye kuongeza tija ya nguvu ya mwanamke kwenye kilimo sasa na baadae.
Uamuzi wa kimapinduzi kujenga miradi ya umwagiliaji pamoja na tafiti kwenye sekta ya kilimo kuna matokeo makubwa sasa na huko tuendako.
Ripoti ya jukwaa la kiuchumi duniani( WEF, sept 2022) inaonesha kwamba katika kila dola1 inayowekezwa kwenye tafiti za kilimo huzalisha dola 6 kama tija katika uzalishaji na zaidi matumizi ya mbolea huongeza tija katika uzalishaji kwa asilimia 61%.
Hivyo maamuzi ya Serikali kuweka bajeti kubwa katika mbolea, tafiti na umwagiliaji sambamba na Bank Kuu kutenga trilioni 1 kwajili ya Bank za Biashara kutoa mikopo kwa riba nafuu( isiyozidi 10%) kwenye sekta ya kilimo na mifugo kuna matokeo makubwa sana kwa mwanamke na uchumi wa Taifa kwa ujumla wake.
Aidha uamuzi wa kuelekeza sehemu kubwa ya pesa za UVIKO19 kwenye sekta ya elimu na Afya kwa kuongeza miundombinu yenye ubora na vitendea kazi ni mchango mkubwa sana kwenye sekta ya elimu na afya ambazo kwa ujumla wake zinagusa sana uchumi wa mwanamke.
Nikweli kama nchi tunapitia changamoto kadhaa hususan ongezeko la gharama za maisha ambazo kwa sehemu kubwa ndio hali halisi ya dunia , hali ambayo hakuna Taifa lenye kinga. Ushauri wangu kwa Rais wetu aliyetunukiwa heshima kubwa kutoka chuokikuu ambacho ni moja ya vyuo bora Afrika, kuendeleza mafanikio haya makubwa zaidi kwa kudhibiti wizi, rushwa na ufisadi ili kuhakikisha thamani ya bajeti zinazotengwa na kupitishwa zinamfikia mwananchi katika uhalisia( value for money).
Nimtakie kila la kheri Mama yetu na Rais wetu, Dr Samia Suluhu Hassan. Kazi iendelee.. David KAFULILA, Disemba ,2022.