Copy n pest
CC katibu tawala
Mwalimu Atupele Ephraim
Hivi ndivyo mafao ya Kiinua Mgongo na Pensheni ya kila Mwezi yatakavyokuwa Katika Sheria Mpya ya PSSSF
ippmedia.com
Nov 13, 2018 4:00 AM
SHERIA mpya ya sekta ya hifadhi ya jamii imeweka utaratibu wa kulipa mafao kwa mkupuo kwa asilimia 35 na asilimia 75 inayobaki italipwa kama mshahara kwa mstaafu kwa miaka 12.5.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, umri wa kustaafu ni miaka 55 kwa hiyari na miaka 60 kwa lazima, lakini kwa kada maalum kama vile madaktari na maprofesa, umri wa kustaafu ni miaka 60 kwa hiari na miaka 65 kwa lazima.
Sheria hiyo imeunganisha mifuko ya PPF, PSPF, LAPF na GEPF kuunda mfuko wa PSSSF unaohudumia watumishi wa umma na mfuko wa NSSF unaohudumia watumishi wa sekta binafsi.
Kanuni za sheria hiyo zinabainisha kuwa pensheni nzima inakokotolewa kwa kuangalia moja ya 580 (1/580) ikizidishwa mara miezi ya uchangiaji na mara mishahara mizuri ya miaka mitatu.
Kwa upande wa malipo ya mkupuo, kanuni hizo zinaeleza kuwa yatakuwa moja ya 580 (1/580) mara jumla ya miezi ya uchangiaji na mishahara ikizidishwa na miaka 12.5 ambayo ndiyo muda ambao mstaafu atalipwa pensheni yake ikizidishwa na asilimia 25 ambayo ndiyo malipo ya mkupuo.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, kikokotoo cha pensheni ya mwezi ni moja ya 580 mara jumla ya miezi ya uchangiaji ikizidishwa na mishahara minono ya miaka mitatu mara asilimia 75 ambayo mwanachama atalipwa kama mshahara kwa kipindi cha miaka 12.5 ikizidishwa na moja ya 12 (1/12).
Ofisa Sheria wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Innocent Kyara, katika ufafanuzi wake kwa Nipashe kuhusu kikokotoo hicho, alisema mwanachama aliyeanza kazi na mashahara wa Sh. milioni moja, akiwa na kiwango cha uchangiaji cha asilimia 20 kwa muda wa miezi 420 (miaka 35) atakuwa na jumla ya michango yenye thamani ya Sh. milioni 84.
Kwa mujibu wa kikokotoo cha zamani, malipo ya mkupuo kwa mtu mwenye mshahara wa aina hiyo, yangekuwa Sh. milioni 71.6,* lakini kwa kikokotoo kipya atalipwa Sh. milioni 35.8, huku pensheni ya mwezi kwa zamani ikiwa Sh. 371,800 na ya sasa ni Sh. 557,800, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.
Kyara alisema kwa mwanachama huyo, jumla ya pensheni ya mwezi ni Sh. milioni 69.2 kwa kikokotoo cha zamani, lakini sasa atalipwa Sh. milioni 103.7, huku mafao yote yakiwa ni Sh. milioni 140.8 kwa kikokotoo cha zamani na Sh. milioni 139.6 kwa kikokotoo kipya.
Alisema mafao yameongezwa kwa asilimia 50 ya mfumuko wa bei ambao ni kati ya asilimia moja hadi 10 na kwamba mfumuko ukizidi asilimia 10, uthaminishaji wa mafao utakuwa asilimia tano na ukiwa chini ya asilimia moja kutakuwa hakuna uthaminishaji na kwamba utafanyika kila baada ya miaka mitatu.
Sheria hiyo ilipitishwa Oktoba 20, mwaka jana ikiunganisha mifuko ya pensheni na kuunda mfuko wa PSSF na kufanya marekebisho kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili uwe mahususi kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.
Sheria hiyo ilianza kazi Agosti Mosi, mwaka huu na kanuni zake zilishatangazwa kwenye gazeti la serikali.