'Ikulu ilichukua faili la Kagoda'
Afisa Mtendaji mkuu wa Wakala wa Serikali wa Usajili wa Kampuni (Blera) Esteriano Mahigila akifafanua jambo kuhusu kadoga habari kamili soma pembeni
Leon Bahati
WAKALA wa serikali wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) jana ulifafanua utata wa faili la usajili wa kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, ukisema kuwa halikuwepo kwenye ofisi hizo kwa muda mrefu kutokana na maagizo ya rais.
Kampuni hiyo, ambayo umiliki wake umekuwa gumzo, inadaiwa kuchota Sh40 bilioni kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), lakini hadi sasa wamiliki wake hawajafikishwa mahakamani kama ilivyo kwa watu wengine 21 waliopandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kuiba jumla ya Sh133 bilioni kwenye akaunti hiyo.
Waandishi wa habari wamekuwa wakifuatilia mintaarafu ya kampuni hiyo kwenye ofisi za Brela bila ya mafanikio na hivi karibuni kuliibuka habari kuwa faili la kampuni hiyo limetoweka Brela, hali iliyozua wasiwasi kuwa huenda sakata la Kagoda litazimwa.
Lakini jana, msajili wa makampuni, Esteriano Mahingila aliwaambia waandishi wa habari akisema: "Nataka niwaambie kuwa nyaraka za Kagoda zipo. Kama kuna mtu anahitaji kuziona anaweza kuzipata, hata kama anataka kupiga 'photokopi' (kudurufu) faili zima, hakuna siri yoyote katika usajili wa kampuni."
Hata hivyo, Mahingila alisema kwa muda mrefu faili la Kagoda limekuwa halipo kwenye ofisi za Brela kwa sababu lilichukuliwa chini ya maagizo ya Rais Jakaya Kikwete tangu kampuni hiyo ilipohusishwa kwenye ufisadi wa EPA.
Alisema kuwa faili hilo pamoja na mengine ya kampuni zilizotajwa kwenye kashfa ya EPA, yalichukuliwa na kamati iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa harakati za kushughulikia tuhuma za wizi wa EPA.
Mahingila pia alitangaza wamiliki wa kampuni hiyo akiwataja kuwa ni Francis William, ambaye alisema anamiliki asilimia 60 ya hisa na Johnson Kyomhando, ambaye anamiliki asilimia 40.
Majina ya watu hao yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari, lakini upatikanaji wa wamiliki hao umekuwa ni mgumu, kiasi cha kubashiriwa kuwa hakuna watu wanaotumia majina hayo.
Kwa mujibu wa taarifa kadhaa za uchunguzi zilizoripotiwa na vyombo vya habari, mawasiliano yaliyo kwenye nyaraka za usajili wa kampuni hiyo yanaonekana kuwa ni ya kampuni za wafanyabiashara maarufu.
Kuhusu taarifa za kupotea kwa faili la usajili wa Kagoda, Mahingila alisema kuwa kuwa mpangilio wa kuhifadhi kumbukumbu za kampuni katika ofisi ya Brela hufanywa kwa njia ambayo hata kama faili likipotea, taarifa zote zinaweza kupatikana kwenye daftari la msajili bila wasiwasi wowote.
"Nashangaa hawa watu walioandika hivi bila kuja kuniona. Taarifa za kampuni hatuziweki tu kwenye faili, bali zinaweza kupatikana pia kwenye daftari la registrar (msajili)," alifafanua Mahingila kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo).
Taarifa kuhusu kumbukumbu za Kagoda zimekuwa ni gumzo kubwa kwenye vyombo vya habari kwa muda mrefu hasa baada ya kutajwa kwenye orodha ya kampuni zilizochota mabilioni ya fedha za EPA.
Baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani mara kadhaa vimeitaja kampuni hiyo ya Kagoda kuwa ilitumiwa na CCM kuchota fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005.
Hata hivyo, katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM- Itikadi na Uenezi,- John Chiligati alikanusha habari hizo, akisema kwamba chama chake hakihusiki na wala hakina uhusiano na kampuni hiyo.
Mahingila aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa anashangaa kusikia kuwa upatikanaji wa taarifa za Kagoda umekuwa ni mgumu, akisema hakuna mwandishi yeyote aliyewahi kumfuata ofisini na kumtaka aone faili ili kujua wahusika.
"Mtu yeote anaweza kuona kumbukumbu zote za mafaili kwa kulipia Sh1,500 tu na kwa waandishi wa habari, hii ni bure, hawatahitaji kulipa chochote," alibainisha Mahingila.
Alisema Kyomuhendo na William walijitambulisha kwenye kumbukumbu za usajili kuwa wanapatikana katika kitalu namba 87, eneo la viwanda Kipawa, wilayani Temeke.
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Mwananchi zinaonyesha kuwa Kagoda ilisajiliwa Septemba 29, 2005, siku moja baada ya kuomba usajili na baada ya mwezi mmoja, BoT ikaanza kuidhinisha sehemu ya malipo yaliyochotwa EPA.
KUMBE NA RAISI ANAHUSIKA LOOH!!!