Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi, amesema kwamba walipokea jalada la Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited inayokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT), lakini wamelirejesha kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai kwa Upelelezi (DCI) kwa uchunguzi zaidi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe jijini jana, Feleshi alisema kwamba ofisi ya DCI inatakiwa kufanya uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na kutafuta vielelezo vingine kutoka nje ya nchi kuhusu Kagoda.
Kagoda inadaiwa kujichotea kiasi cha Sh. bilioni 40 za EPA kwa njia ya kifisadi, ikiwa ni miongoni
mwa makapuni 22 yaliyojinufaisha na Sh. bilioni 133 zilizoibwa katika akaunti hiyo katika mwaka wa fedha wa 2005/06 ndani ya BoT.
Hadi sasa, ni watuhumiwa 21 tu wamefikishwa mahakamani kuhusiana na tuhuma za wizi wa fedha hizo, lakini kumekuwa na hisia miongoni mwa jamii kwamba Kagoda inayoonekana kama muasisi wa wizi wa EPA ikikingiwa kifua na wakubwa kwa sababu zao.
Kwa kauli hii mpya ya Feleshi, suala la Kagoda sasa linazidi kupanuka na kuhusisha makachero kutoka nje ya nchi, hali ambayo inaelekea kuzidi kusogeza mbele muda wa kufikishwa kortini kwa wahusika wa kampuni hii inayodaiwa kuwa na uhusiano na watu walio karibu na vigogo serikalini.
Kauli ya Feleshi, inafuatia kauli ya Wakala wa Serikali wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), kwamba jalada la Kagoda lilipelekwa kwa Timu ya watu watatu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kwa nia ya kufanyiwa uchunguzi.
Timu hiyo ilikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika.
Wajumbe wengine wa Timu hiyo walikuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah.
Awali, Mwanyika alikuwa ameieleza Nipashe kwamba hajui lolote kuhusu Kagoda kwani walikwisha kukabidhi ripoti yao kwa Rais na kwamba vyombo vya serikali viulizwe juu ya kampuni hiyo.
``Kuanzia pale, uenyekiti uliisha na kazi tulimaliza hayo mengine vyombo vinavyohusika vitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia,`` alisema Mwanyika.
Nipashe ilipowasiliana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, kutaka kujua maendeleo ya uchunguzi wa kesi ya Kagoda ambayo imezua gumzo kubwa nchini, alisema yupo likizo Mwanza na kwa sasa hajui nini kinaendelea kwani hana taarifa za hivi karibuni.
Badala yake, Manumba alisema mtu wa kuweza kujua hali halisi ya Kagoda kwa sasa ni DPP Feleshi.
``Kwa sasa nipo likizo na sijui nini kinaendelea tafadhali wasiliana na DPP ndie ataweza kukupa kinachoendelea,`` alisema.
Awali Nipashe ilipowasiliana na Feleshi alisema ofisi yake imepokea mafaili mbalimbali likiwemo la Kagoda kwa ajili ya kufanyia kazi kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika, Feleshi alisema haoni ni kwa nini watu wanakuwa na wasiwasi na kubashiri mambo kuhusu Kagoda wakati hilo ni suala linaloshughulikiwa kisheria.
Alisema majalada yakishafikia kwenye ofisi yake yanapitiwa upya mpaka ofisi yake ijiridhishe kwa ajili ya hatua zaidi, kwa maana hiyo haoni sababu ya watu kuishinikiza ofisi yake kwa kuwa ni wataalamu na kutaka waachiwe wafanye kazi yao.
Hata hivyo, alisema hakuna mpango wowote wa kuficha majalada, ila suala la kisheria huwa lina hatua zake na ni lazma zote zipitiwe.
Feleshi alisema kwa kuwa serikali kupitia Rais ilitangaza kufanya uchunguzi na baada ya uchunguzi suala hilo liliachiwa vyombo vya sheria, ni vyema basi wakapatiwa nafasi ya kufanya kazi hiyo kwa umakini ili watoe maamuzi ya uhakika.