mkoa wa njombe ni♨️♨️♨️♨️♨️👇👇👇ALIYEKUWA MKUU WA MKOA WA IRINGA ATEMBELEA NJOMBE PAMOJA NA WAWEKEZAJI WA MADINI
Njombe, 13 Februari 2025 – Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa enzi ambazo mkoa wa Njombe na Iringa ulikuwa mmoja, na ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mhe. Mohamed AbdulAziz, amefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe akiwa ameambatana na wageni kutoka Kampuni ya Hongji Mining Co. Ltd.
Akiwa ofisini hapo, Mhe. AbdulAziz na watumishi wa kampuni hiyo walisaini kitabu cha wageni na baadaye walifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ambapo walieleza dhamira ya kampuni hiyo kuwekeza katika sekta ya madini mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa wawakilishi wa Hongji Mining Co. Ltd, kampuni hiyo inapanga kuanzisha uwekezaji wa kisasa katika eneo la Mkiu, Wilayani Ludewa, kwa kujenga kiwanda cha kuchakata madini. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 500 kwa wakazi wa eneo hilo na mkoa kwa ujumla.
Aidha, imeelezwa kuwa taratibu zote za upatikanaji wa vibali vya uwekezaji kwenye eneo hilo zimekamilika, na kwa sasa hatua inayofuata ni kuanza kwa utafiti wa kina kabla ya shughuli rasmi za uchimbaji na uchakataji wa madini kuanza.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amepongeza jitihada za kampuni hiyo na kusisitiza kuwa serikali ya mkoa ipo tayari kushirikiana nao ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa kwa wananchi wa Njombe.