Afisa mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Kakamega amekamatwa na kuwekwa kizuizini baada ya kutuhumiwa kumuingilia kingono msichana mwenye umri wa miaka 16.
Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, OCS wa Kituo cha Polisi cha Lumakanda, Wycliff Kwendo, alidaiwa kuwaambia Wazazi wa msichana huyo kuwa kulikuwa na operesheni ya usalama iliyokuwa ikiendelea katika eneo hilo, na kuwashauri kuondoka nyumbani.
Wazazi hao walidaiwa kurudi nyumbani mapema na kumkuta afisa huyo ndani ya nyumba pamoja na binti yao. Polisi pia wanachunguza madai kwamba afisa huyo aliwapa wazazi KSh20,000 ili wasiripoti tukio hilo.
Msichana huyo alipelekwa katika Hospitali ya Lumakanda kwa matibabu na uchunguzi wa kitabibu, huku maafisa wa DCI wakichunguza eneo la tukio. Afisa huyo anaendelea kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kakamega huku uchunguzi ukiendelea.
Kumbuka: Haya ni madai yanayochunguzwa na mamlaka; afisa huyo hajapatikana na hatia mahakamani
Source: NTV