Pre GE2025 Kama haukubaliani na Warioba kwenye hili jiangalie wewe ndiyo tatizo!

Pre GE2025 Kama haukubaliani na Warioba kwenye hili jiangalie wewe ndiyo tatizo!

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

Kamundu

Platinum Member
Joined
Nov 22, 2006
Posts
7,823
Reaction score
10,857


Wakati maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025 yakiendelea, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amesema makundi mawili yanayosigana juu ya uhuru na haki yanapaswa kukutana na kukubaliana kwanza kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.

Amesema yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 yamevifanya vyama vya upinzani kupoteza imani na kuzidisha hofu juu ya kauli za viongozi wa Serikali na CCM kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na haki.

"Uchaguzi uliopita zilitumika taratibu nyingine kabisa na kuuvuruga, mtu unachukua fomu unafuata taratibu, masharti yamewekwa na sifa za mtu kugombea vipo kwenye sheria, lakini havikufuatwa."

Haya ni maneno ya Jaji Warioba katika mahojiano maalumu na waandishi wa Mwananchi Digital yaliyofanyika Aprili 5, 2024 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, akigusia masuala mbalimbali yaliyojitokeza na yanayotarajiwa kujitokeza siku za usoni.

Uchaguzi anaouzungumza wa Serikali za mitaa mwaka 2019, wagombea wengi wa CCM walipita bila kupingwa kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu 2020, ambao chama hicho tawala kilinyakua viti vingi vya udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.

Mchakato huo ulilalamikiwa na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia, waliodai haukuwa huru na haki, huku wagombea wengi wa upinzani wakienguliwa bila kuwepo sababu za msingi.

Warioba ametoa ikiwa takriban umepita mwezi mmoja tangu Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana kusema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itahakikisha michakato ya uchaguzi inakuwa huru na ya haki.

Kinana alitoa kauli hiyo Machi 5, 2024 akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Samia katika mkutano wa nne wa ACT-Wazalendo, jijini Dar es Salaam. Alisema mkuu huyo wa nchi, amedhamiria kuhakikisha michakato ya uchaguzi ijayo inakuwa huru na ya haki.

“Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia, ina dhamira ya dhati kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, kuhakikisha tunakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.

“Kuna sheria na kuna dhamira; unaweza kuwa na sheria nzuri, lakini kama huna dhamira nzuri, unaweza kuikanyaga hiyo sheria ukafanya unavyotaka. Unaweza kuwa na dhamira nzuri na sheria mbaya, lakini dhamira ikitawala mambo yatakuwa mazuri,” alisema Kinana.

Katika hakikisho hilo, Kinana alieleza:‘‘Nataka niwahakikishie Rais ameamua uchaguzi wa mwaka huu na mwaka ujao unakuwa huru na wa haki.”

Kinana aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM alisema wakati anazungumza hivyo ana uhakika wako ambao wana mashaka na kauli hiyo... ‘‘Hao wenye mashaka wana sababu na sababu zao zinatokana na 2019 na 2020 huo ndio ukweli.”

Nasaha za Warioba
Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba amesema licha ya Serikali kusisitiza mara kwa mara uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki, bado kuna viashiria vya upinzani kutokuwa na imani kwenye hilo kutokana na kile kilichotokea kwenye chaguzi zilizopita.

"Tatizo tulilonalo, wale waliosimamia uchaguzi wa 2019 na ule wa 2020 huenda ndio hao hao watasimamia uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.

"Inawezekana wasifanye ya nyuma wakafuata sheria, tatizo ni imani kwamba je wanaweza kusimamia uchaguzi ukawa haki na kuridhisha kwa wananchi, yale yaliyotokea kwenye uchaguzi uliopita yasijirudie," amehoji Jaji Warioba.

Amesema kabla ya uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani, vyama vya upinzani vinahitaji kurudisha imani iliyotoweka kwenye uchaguzi uliopita na chama tawala kionyeshe ni kwa namna gani uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.

"Kwenye chaguzi hizo, zilikuja taratibu mpya kabisa, uzuri Watanzania wanaelewa, wanajua sifa za kugombea. Uchaguzi uliopita zilitumika taratibu nyingine kabisa na kuuvuruga, mtu unachukua fomu unafuata taratibu, masharti yameweka na sifa za mtu kugombea vipo kwenye sheria, lakini havikufuatwa," amesema Jaji Warioba.

Ameshauri vyama vya upinzani vikutane na chama tawala vijadiliane kabla ya chaguzi hizo kwa ajili ya kurudisha imani kutokana na sintofahamu iliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 na ule wa Serikali za mitaa wa 2019.

Amesema baadhi ya nchi zimeingia kwenye matatizo kutokana na sababu za kiuchaguzi akitolea mfano:”Mgawanyiko mkubwa Zanzibar, kuna nchi vurugu zinatokea sababu ya uchaguzi, tusije kufika mahali ikatokea fujo sababu ya uchaguzi, tumeona madhara ya 2019 na 2020, yasijirudie.”

"Sijui kuna kitu kingine katika maandalizi, ila ni lazima tuwe na uchaguzi ambao hautaleta madhara,” amesisitiza.

Katika msisitizo wa eneo hilo la uchaguzi, Jaji Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amesema uchaguzi wa mwaka huu ni mtihani mkubwa, japo hajui wamefanya utaratibu gani na kwa kuwa ni Serikali ndio inausimamia, hivyo kuna kila sababu ya kuweka mambo sawa mapema.

"Wana watumishi wao wanasimamia na kama nilivyosema watu hawana imani, mfano wewe ni DED (Mkurugenzi wa Halmashauri), kabla ulikuwa kiongozi wa chama na watu walikuona, leo hii huyo ndiye anakuja kusimamia uchaguzi, inaweza kuleta changamoto.

"Ndiyo maana nasisitiza pande zote mbili (upinzani na chama tawala) zielewane katika maandalizi, ili tukifika uchaguzi pande zote ziwe zimeridhika," amesema.

Jaji Warioba amesema:"Ukiona upande wa upinzani bado una wasiwasi, wanafikiri uchaguzi ujao unaweza kuwa kama ule uliopita, kisha tunaona Serikali imekuwa inasema kwa msisitizo maandalizi na zoezi lenyewe vitakuwa uhuru na haki kuna haja ya pande hizi kukutana, hawa ambao hawana imani waeleze ni kwanini.

"Tunao uwezo wa kurekebisha hili mapema, wakutane upinzani waseme ni kwanini hawana imani na Serikali iseme yaliyotokea huko nyuma tunayarekebisha kwa njia hii na hii na hii, ili tukienda kwenye uchaguzi kusiwe tena na malalamiko. Hili ni la muhimu sana kufanyika mapema," amesisitiza.

Akitolea mfano kwenye uchaguzi uliopita wa madiwani katika kata 23 uliofanyika Machi 22, 2024 amesema ni dalili kama hizo za mwaka 2019 na 2020 zimeanza kujitokeza katika uchaguzi mdogo wa madiwani, “Tumeanza kuona dalili.”

Amesema kwenye kampeni watu waliokwenda ni wengi na ulikuwepo mwamko, lakini kwenye kupiga kura idadi ikapungua ukilinganisha na chaguzi nyingine za nyuma.

"Japo ni kawaida hizi chaguzi ndogondogo watu kupungua, lakini kwenye huu wa madiwani kuna kata moja niliona waliojiandikisha ni watu 6000 waliojitokeza kupiga kura ni watu 1000, kwenye hili lazima uwe na wasiwasi ikifika mahali wananchi hawaamini katika utaratibu wa uchaguzi ni kwamba hawatakuwa na imani," amesema.

Amebainisha, hata wakati wa mfumo chama kimoja watu walijiandikisha na kujitokeza kwa wingi, akieleza uzoefu wake tangu alipopiga kura kwa ya kwanza mwaka 1962 na tangu wakati huo ameendelea kupiga na kufikisha mara 13.

Jaji Warioba pia aligusia, historia ya uchaguzi tangu Uhuru wa Tanganyika 1961 hadi Muungano 1964, amesema nchi ina uzoefu wa kupiga kura, kwani tangu wakati huo kila baada ya miaka mitano inafanya uchaguzi.

"Wananchi wana uzoefu na uchaguzi, tangu 1962 tulipopiga kura kumchagua Rais, wananchi wanaelewa maana ya uchaguzi na taratibu zake, hata vijana, kwa ambaye amepiga kura mara mbili tatu anaelewa.

"Katika miaka yote ya uchaguzi kulikuwa na matatizo madogomadogo na ndivyo ilivyo kwenye nchi nyingi, kila uchaguzi kuna mapungufu au matatizo madogomadogo na sisi tumekuwa nayo tangu tuanze utaratibu huu,” amesema.

Amesema kila yalipojitokeza kulikuwa na mabadiliko ya kanuni na taratibu, japo wakati ule hakukuwa na utaratibu mawakala, lakini ilipofika mahali ikaonekana kwa wanaosimamia huenda kuna udhaifu wa kupiga kura, kujumulisha, au kutangaza matokeo hivyo, ili kuwe na uhakika ikapitishwa wagombea wawe na mawakala.

"Utaratibu huu ulikuwepo hata wakati wa mfumo wa chama kimoja, haya yalifanywa kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kupiga kura, japo changamoto za uchaguzi zinaweza kutokea katika steji yoyote kuanzia kwenye maandalizi, ambayo steji ya kwanza ni kuandikisha wapiga kura," amesema.

Amesema huko nyuma, ingawa ilikuwa ni kipindi cha mfumo chama kimoja kuliweza kuwa na wagombea wawili, lakini ilionekana wakati wa kuandikisha wapiga kura akiwa sehemu fulani inampenda huyu, lakini chama hakimpendi watafanya mbinu kuharibu uandikishaji ili wasijiandikishe wengi.

"Changamoto nyingine ilikuwa ni kwenye vituo vya kupigia kura, wakiona sehemu hii ni ya mgombea fulani, basi watafanya sehemu hiyo wapiga kura kufika kwa matatizo, ili wasijitokeze wengi ama siku ya kupiga kura kwa makusudi kabisa sehemu fulani vifaa visiende kwa wakati, ili yule mwwnye mashabiki wengi pale akose kura,"

Amesema waliona hayo tangu mwanzo, hivyo ukawekwa utaratibu kuhakikisha kuanzia zoezi la kuandikisha uwe rahisi hadi upigaji kura.

Rushwa bado ipo
Jaji Warioba amebainisha msingi wa uchaguzi, unatokana na taratibu za vyama ambako nako kuna uchaguzi na wananchi wanaona malalaniko kwenye chaguzi hizo za ndani ya vyama, mengi yakihusisha kutokuwepo kwa haki.

"Nyingi zinakuwa ni chaguzi za fedha, rushwa na upendeleo, wananchi wanaona kwa kuwa mnateua watu watakaokuja kuwawakilisha, kuanzia huko mnafanya kwa maslahi yenu na sio ya wananchi, hili nalo ni tatizo.”

Amesema vyama vya kisiasa ni vyombo tu, vipo kwa ajili ya wananchi, wanapofanya tofauti wananchi wanaona, hata chaguzi zao za ndani, wananchi wanaziona na kuona yanayotendeka.

Akiendelea kujenga hoja juu ya rushwa, amesema alimfuatilia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Rais Samia ikielezea utendaji kazi yam waka 2022/23.

Jaji Warioba amesema taarifa hiyo ilikuwa nzuri, aliipenda na Kamishna Hamduni alieleza kwa ufasaha kazi wanayoifanya kwanza ni msingi ni kuzuia rushwa na kueleza hatua ambazo wamechukua kuizuia ikiwamo kutoa elimu kwa wananchi.

"Ni dhahiri huwezi kudili na rushwa bila kushirikiana na wananchi, kwenye taarifa ile kulikuwa na maeneo sikuona yamewekewa uzito, la kwanza alipozungumzia hali ya sasa ya rushwa alichosema kwa macho ya kitaifa ni kuwa Tanzania inafanya vizuri na ya kimataifa inaonekana rushwa imepungua, jambo ambalo naona sio kweli,” amesema.

Amesema yeye anaamini hali ya rushwa sasa ni mbaya, akisisitiza hakuna haja ya kwenda mbali zaidi katika maeneo yaliyo na rushwa, kwani ukiwauliza wananchi wa kawaida hivi siku hizi kwenye huduma za afya, Polisi, Mahakama hakuna rushwa.

"Au Tanesco, ardhi, hakuna rushwa? Pamoja na taarifa ya CAG, tunaona upotevu wa fedha katika Serikali ni mkubwa, mimi nadhani tusiwe tunasema Tanzania rushwa imepungua hapana, ukienda kwa wananchi matatizo yao ni makubwa, nafikiri bado Takukuru hawajafanya kazi ya kutosha kuelimisha wananchi kwenye hili,” amesema.

Amesema wakati wa Rais Benjamin Mkapa, yeye (Jaji Warioba) alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kupambana na Rushwa, baada ya kutoa taarifa kuna hatua fulani fulani zilichukuliwa.

"Pia kwenye elimu kwa wananchi tulifanya kitu, ilikwenda mbali zaidi, waliweza kuhoji," amesema akitolea mfano walipokwenda zahanati na kukuta bango limeandikwa huduma zifuatazo hakuna malipo, mgonjwa akiambiwa atoe fedha atauliza.

"Sasa hii ni hali halisi kwa wananchi, inabidi Takukuru ifanye jitihada zaidi ya kuelimisha wananchi kuhusu rushwa sababu ndiyo wanaoumia," amesema Jaji Warioba

Amekwenda mbali zaidi na kusema Takukuru ni chombo kinachofanya kazi bila kuingiliwa, sio kutumiwa na viongozi kama ni jeshi, kwa kutoa maagizo nenda uchunguze pale, halafu lile linalohusu viongozi hajasikia viongozi hao wanasema waende wachunguzwe.

"Pamoja na taarifa (waliyokabidhi kwa Rais) kuwa nzuri kuna maeneo ambayo Takururu inabidi iimarishe juhudi zake na kuna maeneo ambayo inapaswa isiingiliwe," amesema.
 
Watu hawatakua na imani na Pori jipya Nyani wale wale.
 
Back
Top Bottom