Meneja Wa Makampuni
JF-Expert Member
- Jul 7, 2020
- 9,397
- 12,415
Nashindwa kuelewa labda mnielimishe,
kwa ninavyojua kwenye ukristo dhambi zote zinasamehewa.
Sasa akitokea kiongozi mtekaji, muuaji, mtesaji, fisadi anaeumiza na kuwaachia majoni watu wengi pamoja na umasikini.
Je, toba hata kama ni ya kweli iliyotoka moyoni inatosha kufuta madhara ya dhambi ambazo zimeumiza watu wengi kwa kiwango cha kutisha ?
Kiongozi ameiba misaada ya afya, fedha zilizopaswa kununua dawa, vifaa vya hospitali na kulipa madaktari. Wakati anajinufaisha, wagonjwa wengi sana wamekufa kwa magonjwa yanayotibika, Kina mama walipoteza maisha wakijifungua, Anapofikia mwisho wa maisha, anasema ametubu.
Kiongozi ameuwa au kuamuru kuuawa kwa wakosoaji ambao ni baba wa familia. Watoto wameachwa bila mwelekeo. watoto wake wakitumbukia mitaani, wakiishia kuwa vibaka, mateja, au wauzaji wa miili. Baadhi yao sasa ni majambazi wanaoua wengine kwa sababu ya kosa la mtu mmoja tu. Kisha huyo kiongozi anakuja mbele ya madhabahu na kusema, “Nimetubu.”
Kiongozi amewateka watu waliokuwa wakipigania haki, kuwapiga, kuwatesa na kaamuru waingiliewe kinyume na maumbile ili kuwavunjia heshima ya utu wao, wengine hadi kufa. Familia zao hazijui walipo, watoto wanalelewa na machozi. Akija mbele ya Kanisa au Padre, anasema, “Mimi ni mtu mpya sasa.”
Ingelikua ni bora endapo kama kutubu kwa mtenda dhambi lingekua ni jambo jepesi. Lakini ukweli nikwambia, kutubu kwa mtenda dhambi ni ngumu kuliko ngamia kupenya kwenye tundu la sindano. Mtu hutubu kwa neema ya Mungu tu, si kwa nguvu zake mwenyewe.
Kwa macho ya mwanadamu, ni vigumu kuelewa namna ambavyo muuaji, mtekaji, mtesaji au fisadi anaweza kusamehewa kwa toba. Hii ni kwa sababu dhambi zake zimeacha majeraha makubwa kwa jamii na madhara kwa watu wasiokuwa na hatia. Lakini kwa Mungu, toba ya kweli ni ushindi mkubwa kuliko hukumu ya haraka. Ndiyo maana Yesu alisema: “Furaha kubwa hutokea mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye kuliko kwa wenye haki tisini na tisa wasiohitaji kutubu” (Luka 15:7).
Lakini kumbuka: toba ya kweli si maneno ya haraka mdomoni. Ni safari ya kuvunjika moyo, kukiri makosa, kuacha njia mbaya, na kumrudia Mungu kwa unyenyekevu. Ndiyo maana Biblia inasema, “Moyo uliovunjika na kunyenyekea, Ee Mungu, hutaudharau” (Zaburi 51:17). Kwa hiyo, si kila mtu anayedai ametubu kweli ametubu. Ni Mungu peke yake anayeona moyo.
Kwa hiyo, msamaha wa Mungu haupingi haki. Ikiwa mtu amekuwa fisadi au mtesaji, anaweza kusamehewa rohoni na Mungu, lakini bado akakabiliana na matokeo ya dhambi zake katika maisha haya. Musa alisamehewa kwa kumpiga mwamba badala ya kuusemesha, lakini hakuingia Kanaani (Hesabu 20:12). Hii inatufundisha kuwa msamaha hauondoi matokeo ya dhambi, bali huondoa hukumu ya milele.
Ndiyo maana nasema, ndugu yangu, tuna safari ndefu ya kuelewa msalaba. Toba si jambo la kirahisi, bali ni tendo linalowezekana kwa neema ya Mungu pekee. Na msamaha wa Mungu, ingawa ni wa bure, uligharimu damu ya Yesu msalabani. Hii ndiyo sababu kila anayetubu kwa dhati anapokelewa, kwa sababu si kwa haki yake, bali kwa haki ya Kristo.