Story ya Kijiweni: “No Reform No Election ni Scam ya Kisiasa”
Basi bwana, tulikuwa tumekaa pale kwa Mangi—mahali pa mishikaki na siasa. Unajua sehemu kama ile ukikaa dakika tano tu, lazima mjadala wa kisiasa ushike moto. Siku hiyo moto uliletwa na kauli ya Chadema: "No Reform No Election." Jamaa walikuwa wanasema eti uchaguzi hautafanyika kama hakuna marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Nikawacheki macho, nikawaambia, “Wakuu, hiyo ni scam ya kisiasa, siyo mpango wa kweli. Hii siyo njia ya kisiasa ya chama makini, ni ama utapeli au kukosa dira.”
Kutoka Katiba Mpya Hadi Minimum Reform – U-turn Isiyokatika
Hebu tukumbuke kidogo. Miaka ya 2021 hadi 2024, Chadema walikuwa wakiimba kila kona juu ya Katiba Mpya. Wakashupalia kabisa, wakaitwa wapigania haki.
Lakini ACT-Wazalendo wakaja na hoja ya busara: “Jamani, hebu tuanze na minimum reforms kwenye sheria za uchaguzi kwa sasa, maana muda hautoshi kwa katiba mpya kabla ya 2025.”
Chadema wakawadharau ACT. Wakawaita wajinga, wasaliti, na kusema eti hiyo ni kushirikiana na CCM.
Leo hii, hawa hawa Chadema wamerudi kwenye zile zile hoja za ACT, wanapigia kelele “reforms” – zile zile walizozibeza! Si ajabu hiyo?
No Reform No Election – Kauli Bila Meno
Sasa wamekuja na kauli ya “No Reform No Election”, kana kwamba wao ndio NEC au Mahakama ya Katiba. Eti hawataruhusu uchaguzi ufanyike bila marekebisho. Swali langu: Kwa nguvu ipi? Kwa wanachama gani? Kwa mtandao upi wa kitaifa?
Nikawaanikia hoja kijiweni kama mtoa mada wa BBC ya mtaa:
1. Tundu Lissu yupo jela, lakini hakuna maandamano
Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, yupo gerezani sasa hivi, lakini Chadema hawajaandamana, hawajakemea, hawajakemea kwa nguvu, wala hakuna presha yoyote kama chama kikuu cha upinzani.
Hivi kweli watu hawa wataweza kusimamisha uchaguzi nchi nzima mwezi wa kumi?
2. Mbowe alipanga maandamano, alitokea na watoto wake tu
Mbowe aliitisha maandamano, lakini waliojitokeza ni yeye, watoto wake, na mpiga picha wa chama. Wanachama wengine walichuna kama hawajasikia. Kama hawana support ya ndani, watashinikiza vipi taifa?
3. CCM wamefuta mikutano, Chadema wametii kimya kimya
Mikutano ya vyama vya siasa imepigwa marufuku na CCM. Kina Heche, Mdee, hawasikiki tena. Wametii kama wanafunzi wa shule ya kata. Hawa watu kweli wataandamana nchi nzima?
4. Ruzuku imekatwa, Chadema wamenyamaza
Ruzuku – damu ya chama – imekatwa. Hakuna kelele, hakuna malalamiko, hakuna mpango mbadala. Hivi chama kisicho na bajeti kitaendesha harakati za kitaifa?
---
Hoja Zao Zinajitupa Chini zenyewe
Wanasema eti wataamrisha wananchi wasijitokeze kupiga kura. Swali ni hili: Watanzania wote ni Chadema? Vyama vingine je? Wakisusia wao, vyama vingine vitaendelea, na CCM itajaza takwimu zake, na hamtakuwa na pa kulalamikia baada ya uchaguzi kwa sababu hamkushiriki.
Na kichekesho kingine ni hiki: wanasema eti vyombo vya kimataifa vitaingilia kati. Hivi kweli? Uliza CUF. Seif Sharif Hamad alizunguka dunia nzima kulalamikia uchaguzi wa Zanzibar. Nani alimsaidia? Nani alizuia uchaguzi? Hakuna. Vyombo vya kimataifa huamka kama damu inamwagika, siyo kwa presha ya mitandao tu.
---
Siasa ni Vita ya Pande Tatu – Ndani, Nje, na Mitaani
Nilihitimisha kwa kusema, “Kupambana na CCM siyo kususia uchaguzi. Siyo kukaa pembeni ukitumaini CCM wataacha tu madaraka. Siasa ni kama vita ya anga, ardhini na majini. Unapambana ndani ya uchaguzi, nje ya uchaguzi, na mtaani. Chadema waache siasa za kulalamika, waingie vitani.”
Mmoja pale kijiweni akaniambia, “Kaka hiyo ni lecture ya bure. Umenifumbua macho.”
Nikacheka nikasema, “Uchaguzi utakuwepo Oktoba 2025, hata Chadema wakiamua kususia kwa wiki nzima.”