Pia sikufahamu kwamba ni Sokoine ndio alituletea Dala Dala. Ni kitendo cha kijasiri mno kuruhusu ubinafsishaji wa nyanja za Uchumi za Usafirishaji wakati wa Nyerere. Ni kama vile alimwambia Nyerere, Mzee haya makampuni yako ya Ujamaa na Kujitegemea ya UDA na KAMATA yanafeli. Ruhusu watu wamiliki vyombo vya uchumi. Alichapa kibao kwenye uso wa Nyerere, na Azimio la Arusha.
Hata hivyo, kama ambavyo tunaungana mkono pale tukikubaliana, tukikosea pia tutakosoana.
Uchambuzi wako wa Adolf Hitler una mushkeli. Hakuna wachambuzi wanaoheshimika wanaosema Ujerumani ya leo ni kazi ya Hitler. Hitler aliua wasomi, isipokuwa watengeneza mabomu. Mabomu yakazaa vita, vita vyenyewe wakashindwa, na li nchi likabomolewa na washindi wa vita. Wasomi wa Kiyahudi wakaanza mbele. Ujerumani ikaanza kujengwa upya baada ya Hitler kuondoka.
Ujerumani ilijengwa tena na mifumo mipya ya Ujamaa wa Masoko ya Kiuchumi (Social Market Economy) kuanzia katikati miaka ya 40 mpaka mwishoni wa miaka ya 50. Tofauti na mifumo ya Kidekta chini ya mawazo ya Hitler, mifumo hii mipya ilihurisha uchumi wa Ujerumani, ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya mashindano, kuruhusu masoko huria, pamoja na biashara ya nje. Hilter hasifiki kwa hayo. Kile anachosifika kwa kukijenga wakati wa utawala wake alikivunja kwa mawazo na mwamko wake wa kivita vita.
Ahsante.