Date::11/10/2008
Mfanyabiashara atoa Sh400milioni kugharimia mkutano UVCCM
Na Daniel Mjema, Dodoma
MFANYABIASHARA mashuhuri nchini, Tanil Somaiya anayemiliki Kampuni ya Shivacom ametoa Sh400 milioni kugharamia Mkutano wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Mfanyabiashara huyo alikabidhi msaada huo unaohusisha vifaa vyenye thamani ya Sh250 milioni na fedha taslimu Sh150 milioni za posho za wajumbe wanaokadiriwa kuwa 1,000, kwa Mwanyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete katika tafrija fupi iliyofanyika Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma.
Kabla ya kukabidhiwa kwa msaada huo, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Francis Issack alisema katika kufanikisha mkutano huo wa uchaguzi, Baraza Kuu la UVCCM liliamua kuteua kamati maalumu ya watu wanne ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma William Lukuvi, kutafuta fedha.
Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Lawrence Masha, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Somaiya.
Issack alisema Baraza Kuu la UVCCM liliwaagiza kutafuta vifaa 1,000 kila kimoja ambavyo ni pamoja na fulana, kofia, mabegi, kalamu na madaftari ambavyo vilitengenezwa kwa gharama ya Sh250,000 katika kiwanda kinachomilikiwa na Somaiya mwenyewe.
Kwa mujibu wa kaimu katibu huyo, ingawa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM Taifa ni 750 lakini wapo waalikwa ambao ni pamoja na Rais Kikwete na wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambao pamoja na wajumbe wengine watalipwa posho ya Sh50,000 kwa siku.
Akikabidhi msaada huo, Somaiya alisema ameamua kukisaidia chama hicho kwa kuwa yeye ni mkereketwa na mpenzi wa CCM, kauli ambayo ilipongezwa na Rais Kikwete ambaye alisema kwa kutoa msaada huo, mfanyabiashara huyo atakuwa amejitangaza kibiashara.
Tafrija hiyo fupi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo wajumbe wa NEC waliomaliza kikao chao jana mchana na kupitisha majina ya wanachama wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi UVCCM, Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Jumuiya ya Wazazi.
Katika hatua nyingine, wazee wa CCM wa wilaya ya Dodoma mjini wamemuomba Rais Kikwete kuharakisha mpango wake wa kupitisha utaratibu unaotenganisha suala la uongozi na biashara ndani ya Serikali na ndani ya chama cha Mapinduzi.
Akisoma risala kwa niaba ya wazee hao Ikulu ndogo mjini Dodoma jana, Mohamed Makbel alisema bila maadili hakuna nidhamu na kutaka linalowezekana leo lisingoje kesho.
Pamoja na hayo ili kulinda umoja wetu tunaomba viongozi wetu wa chama na serikali wanapotofautiana watumie vikao husika vya chama, ilisema sehemu ya risala hiyo.
Pia waliomba kupitiwa kwa sheria ya mwaka 1979 iliyoagiza Dodoma kuwa eneo maalumu la uwekezaji ili sheria hiyo ihuishwe kuwawezesha wawekezaji wengi kuwekeza Dodoma na kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Walimpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa ujasiri wa kuamua kujenga chuo kikuu cha Dodoma na ujenzi wa uwanja wa kisasa wa ndege wakisema uamuzi huo umeongeza shauku kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo wa Dodoma.
Akiwahutubia wazee hao, Rais Kikwete alisema azima ya serikali ya makao makuu kuhamia Dodoma iko palepale na kwamba amefarijika na hotuba ya wazee hao kwani imeonyesha namna ambavyo bado wako pamoja na serikali yao katika kupigania maendeleo ya wananchi.
Kuhusu suala la kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa eneo huru la kibiashara, Rais alisema utekelezaji wa suala hilo ulikwishaanza japo kasi yake haiendi kama ilivyotarajiwa lakini aliahidi kuwa serikali italitazama suala hilo ili shabaha iliyokusudiwa na Serikali iweze kufanikishwa.