Mshirika wa mtuhumiwa ufisadi
amwaga mamilioni kwa CCM
MWANDISHI WETU
Dodoma
TANIL Somaiya, mshirika wa kibiashara wa mtuhumiwa wa rushwa ya rada aliyekimbilia nje ya nchi, Shailesh Vithlani, amechanga zaidi ya milioni 400/- kugharimia uchaguzi ujao wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Somaiya alikabidhi vifaa kadhaa vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi ili vitumike kwenye uchaguzi huo wa kuwapata viongozi wa kitaifa wa umoja huo.
Vifaa hivyo vya uchaguzi vyenye thamani ya milioni 400/- vilikabidhiwa kwa CCM mjini Dodoma jana wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala cha CCM (NEC).
Taarifa za uhakika kutoka Dodoma zinaeleza kuwa mfanyabiashara huyo, Somaiya, alikabidhi msaada huo makao makuu ya CCM yaliyopo mji unaotarajiwa kuwa makao makuu ya nchi, Dodoma.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikichunguza bohari moja la kutunza bidhaa zisizolipiwa ushuru/kodi linalomilikiwa na kampuni moja iliyo chini ya kundi la kampuni za Shivacom za Dar es Salaam kwa tuhuma za kukwepa kodi. Kampuni hiyo ni mali ya Somaiya.
Somaiya pia anamiliki kampuni ya Incar (Tanzania)Limited, ambayo ndiyo inatajwa kumiliki bohari kati ya mabohari 22 ya kutunzia bidhaa zisizolipiwa ushuru/kodi yaliyofungwa na TRA hivi karibuni.
Incar (T) Limited, kampuni ambayo ni ajenti wa magari yanayotengenezwa Italia ya IVECO, pia iliwahi kufuma zabuni ya mabilioni ya shilingi ya kuliuzia magari ya kijeshi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wote wawili, Somaiya na Vithlani, wamewahi kuhojiwa chini ya kiapo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, kuhusu tuhuma za kuhusika kwao katika kashfa ya rushwa ya rada.
Wafanyabiashara hao walikiri kwamba walikuwa na hati ya kiapo ya kuwaruhusu kufanya mambo kwa niaba ya kampuni ya Envers Trading Corporation, inayodaiwa kupokea mabilioni kama rushwa ya rada.
Kulingana na uchunguzi, Envers Trading Corporation, ililipwa na kampuni nyingine ya Red Diamond Trading, dola za Marekani milioni 12 (karibu bilioni 15/-).
Red Diamond Trading ilianzishwa katika visiwa vya Uingereza vya Virgin mwaka 1998 na kampuni nyingine inayohusishwa na kampuni ya Uingereza ya kutengeneza silaha ya BAE Systems, ambayo ndiyo iliyoiuzia Tanzania rada kwa bei ya kuruka enzi za utawala wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 2002.
Alipobanwa na makachero wa Kiingereza, Somaiya alikiri kuwa alipewa haki ya kisheria kupitia hati ya kiapo iliyomruhusu kuiwakilisha kampuni ya Envers Trading Corporation kwa kipindi cha miezi 11.
Lakini, alisisitiza kwamba hakuwa na mambo mengine aliyoshiriki katika kampuni hiyo na kwamba hakujua kabisa uhalisi wa kampuni hiyo wala mahali zilipo ofisi zake.
Nyaraka rasmi kutoka Mahakama ya Kisutu zinaonyesha kachero wa Uingereza, Sajini Steve Rosenthal akiwabana kwa maswali Vithlani na Somaiya mwaka 2006 na kukiri kuhusika kwao.
Wakati wa mahojiano hayo, Somaiya alikiri kwamba yeye pamoja na mwenzake Vithlani aliyemweleza kuwa rafiki yangu mkubwa walikuwa wamiliki wa kampuni ya Jijini Dar es Salaam, Merlin International company.
Shailesh Vithlani ni rafiki yangu mkubwa sana. Yeye pia ni mkurugenzi wa Merlin International. Sijui kama yeye ni mmiliki pia wa Envers Trading
nilihamishia kwake haki ya kisheria ya kuiwakilisha Envers Trading. Sijui kama yeye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo, nyaraka za mahakama zinaonyesha ndivyo alivyosema Somaiya.
Kwa upande wake, Vithlani aliiambia mahakama chini ya kiapo kwamba alikuwa akiendesha kampuni ya Merlin International kama kampuni ya ushauri kwa kushirikiana na wamiliki wengine
mmojawapo akiwa Tanil Somaiya.
Vithlani ameshafunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Kisutu kwa kusema uongo chini ya kiapo na kuwadanganya maofisa wa upelelezi huku wapelelezi wakidai kuwa aliwadanganya kuwa yeye hakuwa mmiliki wa Envers Trading na kuhusu kupokea dola 390,000 kama rushwa ya rada. Inadaiwa kuwa kwa ujumla alilipwa dola milioni 12 kama rushwa.
Mfanyabiashara huyo aliyetorokea nje ya nchi, alifunguliwa mashtaka bila yeye kuwapo mahakamani na bado anatafutwa pamoja na kutolewa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake popote atakapopatikana duniani.
Uchunguzi umeonyesha kwamba, Somaiya aliifahamisha Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kupitia kwa mawakili wake kwamba alikoma kuwa mmiliki na mkurugenzi wa Merlin International Januari 8, 2007.
Hata hivyo, pamoja na kutolewa taarifa ya kukomeshwa uhusiano na Vithlani, Somaiya alikuwa mfanyabiashara mshirika wa Vithlani wakati wa kutendeka kosa la rushwa ya rada.
Haieleweki kama uongozi wa nchi bado unamchukulia Somaiya kama mtuhumiwa katika uchunguzi unaoendelea kuhusu rushwa ya rada.