Tahariri ya Tanzania Daima
WIKI chache zilizopita Rais Jakaya Kikwete alisaini Sheria ya Matumizi ya Gharama za Uchaguzi katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam. Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo mawaziri, mabalozi, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania iliandika historia katika nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kusaini sheria hiyo ambayo imelenga kudhibiti vitendo viovu wakati wa uchaguzi.
Tulifurahishwa na uamuzi wa ujio wa sheria hii, tukiamini itapunguza mianya ya rushwa, hasa kwa kurubuni wapiga kura katika maeneo ya vijijini, ambako wananchi wengi haki zao hununuliwa.
Jambo la kusikitisha ambalo sasa limeanza kuibua hisia miongoni mwa jamii ni hatua ya Rais Kikwete kusaini sheria ambayo baadhi ya vipengele vyake havikupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Tunaamini kitu chochote ambacho kinafikia hatua ya kusainiwa na rais huwa kimekamilika, sasa tumeshtushwa kusikia kuna baadhi ya vipengele vimechomekwa kinyamela.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alibaini kuchomekwa kipengele kinyamela katika mjadala uliopelekwa bungeni na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, aliyetaka mabadiliko ya pendekezo la serikali kwa kifungu 7 (2).
Alisema katika kifungu hicho, Chenge alitaka makundi ya sanaa yaingizwe badala ya neno ‘voters'.
Tunasema kilio cha Dk. Slaa kinaweza kuwa na ukweli kama wahusika wataamua kuchukua uamuzi wa kina wa kupitia kipengele kimoja baada ya kingine.
Kipengele kinachodaiwa kuchomekwa kwenye sheria iliyosainiwa na Rais Kikwete ni cha 7 (3), ambacho hakikuwamo kabisa kwenye muswada huo bungeni.
Tukiwa chombo huru, tunasema kama kweli kuna watu waliojaribu kuchomeka kipengele hicho kwa manufaa yao binafsi wanapaswa kusakwa kwa udi na uvumba ili kufuta aibu hii.
Aibu hii ya kumgeuza mkuu wa nchi kuwa mtoto, haikubaliki. Tunatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuwawajibisha wale ambao wametia mikono yao kwenye kipengele hicho.
Tunachukua fursa hii kuwataka Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Spika wa Bunge kuwaomba radhi rais na umma wa Watanzania kutokana na aibu hii ambayo haikubaliki.
Tunatumia fursa hii kuzitaka ofisi hizo mbili kurudisha sheria hiyo bungeni itenguliwe, ili iweze kujadiliwa upya kwa manufaa ya taifa na si kikundi cha watu wachache.
Kama imefikia hatua rais kuchomekewa vipengele kama hivi, Watanzania tutegemee nini katika sheria nyingine ambazo husaini ndani ya ofisi yake?
Sisi Tanzania Daima tunasema umefika wakati sasa wa kuhakikisha wale wote waliohusika kumdanganya rais wanaondolewa kwenye nafasi za kazi wanazoshikilia ili kujenga nidhamu kwa watu wengine.
Tunamalizia kwa kusema rais ana majukumu mengi, lakini wasaidizi wake wanapofikia hatua ya kumdangaya, inatia shaka na kuondoa imani mbele ya jamii.