Karai na ndoto: Vijana wa Tanzania wakumbatia sanaa ya mapishi ya Kichina

Karai na ndoto: Vijana wa Tanzania wakumbatia sanaa ya mapishi ya Kichina

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
微信图片_20260209100658_1_14.png


Katika jiko lenye shughuli nyingi katikati mwa jiji la Dar es Salaam, milio ya visu vigonga ubao wa kukatia ilijaa hewani. Katikati ya mvuke na sauti za makarai, Ruth Washima Seni, mwanafunzi kijana wa Tanzania anayesomea mambo ya huduma, anajaribu kukata viazi kwa usahihi, vipande vyembamba kama nywele.

Hii ni aina ya ukataji wa "sindano ya fedha", jaribio gumu sana la ujuzi wa kisu katika mapishi ya Kichina. Kwa Seni, sio tu inawakilisha mbinu ya kupikia ; bali pia ni sehemu ya mustakabali mpya.

"Sikujifunza jinsi ya kupika chakula cha Kichina tu. Nilijifunza mbinu, lishe, nidhamu, na utamaduni," alisema Seni, akifuta paji la uso wake baada ya kujua vizuri kukata. "Sasa naweza kupika jiaozi, mikate, na nyama ya ng'ombe ya kukaanga, na ninaelewa ni kwa nini vyakula vya Kichina vinazingatia sana afya na uwiano."

Seni ni mmoja wa wanafunzi 20 katika kundi jipya la wanafunzi wa programu ya kipekee ya upishi katika Taasisi ya Teknolojia na Usimamizi ya Kilimanjaro (KITM). Ikizinduliwa Januari 2026, kozi hiyo inatolewa kwa ushirikiano kati ya taasisi hiyo na "The Best Company," kampuni ya China inayoshughulikia mawasiliano ya kitamaduni.

Programu hiyo ni zaidi ya kufundisha mapishi, kwani inawaingiza wanafunzi katika falsafa ya vyakula vya Kichina. Ukiongozwa na Mpishi Wang Bo kutoka Mkoa wa Sichuan, mtaala unashughulikia joto la mapishi yenye pilipili ya Sichuan, utamu wa kina wa kitoweo cha kaskazini mashariki, na ladha maridadi na freshi za vyakula vya Cantonese.

"Vyakula vya Kichina vinabadilika sana," alisema Wang. "Unaweza kuchanganya na kubadilisha viungo. Lakini ili kufanya hivyo vizuri, lazima uelewe kanuni zinazohusiana na chakula hicho."

Kwa wanafunzi, mkondo wa kujifunza sio tu unahusisha ladha pekee, bali pia unajumuisha ujuzi wa matumizi ya vijiti vya kulia na kuelewa hadithi za jadi zinazohusiana na mapishi kama vile Jiaozi, ambazo zinaashiria utajiri na umoja.

"Nimegundua kuwa watu wa China si kwamba wote wako sawa," Seni alibainisha. "Kila eneo lina utamaduni na chakula chake."

Ingawa mawasiliano ya kitamaduni ni mazuri, kichocheo kikuu cha vijana hawa wenye ndoto ni fursa za kiuchumi.



Filbert Haule, mwalimu wa somo la huduma katika KITM, alielezea kwamba uamuzi wa kuanzisha vyakula vya Kichina ulikuwa wa kimkakati. Kutokana na watalii wa China na wafanyabiashara kubeba jukumu linaloonekana zaidi katika uchumi wa Tanzania, mahitaji ya chakula halisi cha Kichina yanaongezeka.

Zaidi ya hayo, Tanzania inajiandaa kupokea wageni wengi wa kimataifa wakati ikijiandaa na Kombe la Mataifa ya Afrika la 2027 (AFCON).

"Tunataka kuwapa wageni ladha mpya," Haule alisema. "Wawekezaji na wamiliki wa migahawa watakapoona wanafunzi hawa wanaweza kupika chakula halisi na kitamu cha Kichina, watavutiwa. Hilo linatoa fursa zaidi."

Muundo wa kozi ni mgumu. Asubuhi hutumika kujifunza masomo kwa kutazama video kutoka kwa wapishi waliobobea nchini China, ikifuatiwa na vipindi vya kujifunza kwa vitendo wakati wa alasiri katika majiko ya KITM ambapo viungo vya ndani yaani nyama ya ng'ombe ya Tanzania, kondoo, na vyakula vya baharini hubadilishwa kuwa vyakula vya asili vya Kichina.

Kwa Mpishi Wang, chakula ni diplomasia kuu. "Chakula ni daraja linalowaunganisha watu," alisema. "Wanafunzi wanapoelewa utamaduni, wanapika kwa hisia, na chakula kinafikia kiwango cha juu."

Wahitimu wa programu hiyo wanapendekezwa katika migahawa na hoteli za Kichina katika kanda yote, na kuwapa njia ya haraka ya kupata ajira.

Kwa Ruth Seni, karai limefungua ulimwengu wa uwezekano. Sasa ananoa ujuzi wake nyumbani, akijiamini kwamba ana uwezo wa kushindana katika soko la ajira.

"Huu ndio ujuzi unaokufanya uwe tofauti," alisema, akiangalia chakula chake kilichokamilika cha nyama ya ng'ombe iliyokaangwa. "Ni utamaduni, afya, biashara, na uhusiano. Ninaweza hata kuanzisha mgahawa wangu siku moja."
 
Back
Top Bottom