*SOMO LA NNE – AINA YA VITABU AU UANDISHI*
_AINA YA VITABU_
Tuendelee na masomo yetu. Baada ya somo letu la tatu, nilipata maswali muhimu kadhaa. Baadhi nilishayajibu lakini nikashtuliwa kwamba kuna mengine ambayo sikuyagusa. Nisiyoyagusa yalikuwa manne. Tangu wakati ule hadi leo maswali hayo manne sijayajibu bado. Sijayajibu kwa sababu nilikuwa nafikiria jinsi ya kuyafikisha kwenu pasipo kuharibu darasa letu. Hivyo si kwamba sina majibu yake, la hasha! Majibu yake yana ugumu unaopaswa kuondolewa kwanza. Basi, nikawa natafuta namna ya kuyaleta katika sura laini kwa wote. Nimechelea sana kuyaleta uwanjani na kuchokoza maswali mengine mia na ushehe kwa sababu ya kuwavurugeni. Hatimaye, kwa kusudi la kuzuia mkasa wa kulivuruga darasa, nimeona vyema nilete kwanza somo maalumu, somo la nne.
Somo hili linaeleza kitu kimoja tu: *mitindo au aina za uandishi zilizomo katika Biblia.* Aina za uandishi ni kitu kinachokuja kufuatia ushiriki wa mwandishi mwanadamu. Ni hivi, aina za uandishi zilizomo kwenye Biblia si aina moja. Aina, au mtindo, au tukitaka fani, kwa kizungu ni “genre”. Neno hili ni la Kifaransa lakini linatumika kama lilivyo katika Kiingereza.
Ni hivi, kusudi Mungu afanikishe nia yake ya kuwaletea wanadamu ujumbe wake mzito, aliwaruhusu na aliwasaidia waandishi wanadamu watumie aina au mitindo mbalimbali za uandishi.
Katika Biblia kuna walau aina kumi na nane za uandishi:
i. *Hadithi* – mfano masimulizi ya kuumbwa ulimwengu na vitu vilivyomo (katika kitabu cha Mwanzo)
ii. *Historia* – matukio ya Misri na masimulizi yote ya Kutoka (katika vitabu vya Torati na vitabu vya historia)
iii. *Usimuliaji wa mtiririko* – masimulizi ya maisha ya Abrahamu, Isaka, Yakobo n.k
iv. *Hekima* - vitabu vya Ayubu, Zaburi, Mithali, Hekima ya Sulemani, Wimbo Ulio Bora, Mhubiri na Yoshua bin Sira
v. *Zaburi (mashairi)* – mfano wimbo wa Musa (Kut 15), kitabu cha Zaburi, wimbo wa Zakaria (Lk 1:68-79), wimbo wa Bikira Maria (Lk 1:46-55), wimbo wa mzee Simeon (Lk 2:29-32)
vi. *Misemo ya kinabii* – katika vitabu vya manabii (vitabu vya Isaya mpaka Malaki)
vii. *Nyimbo* – mfano wimbo wa kuusifu utii wa Yesu (Flp 2:6-11)
viii. *Sala* – mfano sala ya Sulemani katika kulitabaruku hekalu (1Fal 8:22-61), sala ya Baba Yesu (Mt 6:9-13)
ix. *Injili* – mfano Injili za Mathayo, Marko, Luka na Yohane
x. *Mifano* – mfano katika Mt 13:1-50 na Mk 4:1-34
xi. *Miujiza* – masimulizi ya makuu ya Mungu (mfano katika Mk 1:21-34, Yn 2:1-12 n.k.)
xii. *Methali* – mfano katika vitabu vya Mithali na Hekima ya Sulemani
xiii. *Barua au nyaraka*: mfano barua au nyaraka 21 za Agano Jipya
xiv. *Uandishi wa kiapokaliptiko (ufunuo)* – Danieli 8-9, Mt 25, Mk 13 na kitabu cha Ufunuo
xv. *Lugha ya picha au isitiari* – mfano katika kitabu cha Mwa 1-3 na
xvi. *Lugha ya mafumbo* – mfano katika kitabu cha Ufunuo
xvii. *Lugha ya chuku (ndiyo kutilia chumvi)* – mfano habari ya mtu kukata miguu au mikono yake mwenyewe (Mt 18:6) au ngamia kupita kwenye tundu la sindano (Mk 10:25) na
xviii. *Lugha ya kinyume* – mfano katika Mk 4:12.
_UMUHIMU WA KUJUA AINA ZA UANDISHI_
Kuzijua na kuzipambanua aina za uandishi zilizomo kwenye Biblia ni muhimu, tena muhimu sana. La sivyo, Biblia inaweza kusomwa vibaya. Kwa maneno mengine, kujua aina za uandishi ndiyo msingi mmojawapo wa kujua kusoma na kutafsiri vizuri Biblia. Mfano, katika Agano la Kale, usisome wala kutafsiri vitabu vya Torati (ambavyo ndani yake kuna uandishi wa kihadithi, kihistoria, usimuliaji wa mtiririko, miujiza na sala) kama vitabu vya hekima. Wala usisome vitabu vya historia kama vitabu vya kinabii. Usisome zaburi (ambazo ni mashairi na sala) kama hadithi wala usisome vitabu vyenye hadithi kama vitabu vya nyimbo au sala na kadhalika.
Hali kadhalika, katika Agano Jipya mtu asisome Injili kama barua au barua kama kitabu cha kiapokaliptiko. Aidha, ndani yake mtu asisome sehemu zilizoandikwa kama zaburi au sala kama anasoma mambo ya kiapokaliptiko.
Basi, aina za uandishi ndizo zinazotofautisha vitabu vya Biblia. Lakini, wala si katika Biblia tu bali ndicho kinachotofautisha hata leo hii, barua za serikali na zile za kirafiki au na zile za mapenzi, matangazo ya kifo redioni na matangazo ya biashara, hotuba za kwenye mazishi na hotuba za kwenye sherehe za ndoa, magazeti ya dini na magazeti mengineyo kama MWANANCHI, MAJIRA, NIPASHE, TANZANIA DAIMA, MZALENDO, UHURU, MWANA SPOTI, DIMBA, IJUMAA, TANZANITE, TIMES, THE NEW AFRICAN ama NEWSWEEK, vitabu vya dini na vitabu vya hadithi, vitabu vya sayansi na vitabu vya lugha na kadhalika.
_NIA YA KUTUMIA AINA NYINGI ZA UANDISHI_
Mungu aliwaruhusu waandishi wanadamu watumie aina mbalimbali za uandishi ili wawaeleweshe wanadamu wenzao mambo mazito aliyokusudia wayaelewe vyema. Ni kama darasani, kusudi mwalimu awaeleweshe wanafunzi mambo magumu anaweza kutumia picha, nyimbo, hadithi, mifano na kadhalika. Mwalimu asiye mbunifu katika hayo mara nyingi huishia kujielewa mwenyewe tu.
Kumbe, msomaji wa Biblia hawezi kuufahamu vyema ujumbe wa Mungu pasipo kuelewa aina, fani au miundo ya vitabu vilivyo ndani yake. Kifupi, aina za uandishi zimetumika kama nyenzo za kubebea ujumbe wa Mungu asiyeonekana na asiyezungumza lugha za binadamu kwa midomo yenye mate kama yetu. Mungu hakutaka wanadamu wapokee ujumbe wenye utata isipokuwa unaoeleweka kama maji. Kwa kisa hicho akaruhusu hata waandishi wanadamu watumie hadithi za watu wao wenyewe kubebea ujumbe wa Mungu.
Mfano wa ruhusa hii unaonekana wazi katika sura za mwanzo za kitabu cha Mwanzo, sura 1-3, ambapo hadithi vya visasili vya watu wa Mashariki ya Kati zimetumika kuwaeleza watu kwamba kila kitu mwanzo wake ni Mungu, mamoja uwe ulimwengu na magimbe yake, dunia na vilivyomo ndani yake na hata wanadamu wenyewe. Hapo hadithi zimetumika kubebea vitu kama vikapu, magunia, viroba na rambo vinavyotumika kubebea vitu vyenye thamani kubwa. Ukipokea vitu hivyo unaweza kutenganisha kikapu, gunia, kiroba au rambo na kitu kilichobebwa. Usipoweza kutenganisha mambo kwa namna hiyo, ndiyo umeyakoroga mambo.
_UWEZEKANO WA KITABU KUWA NA AINA KADHAA ZA UANDISHI NDANIMWE_
Kwenye kitabu kimoja kunaweza kuwa na aina kadhaa za uandishi. Ufundi au umahiri wa waandishi wanadamu waliovuviwa na Roho Mtakatifu katika kuyaandika Maandiko Matakatifu ni mambo yanayotofautisha kitabu kimoja cha Biblia na kingine. Kila mwandishi aliandika kadiri ya wasikilizaji au wasomaji wake na hata lengo lake. Kwa kukidhi haja yake, wakati mwingine ilimpasa achague mara hadithi, mara usimuliaji wa mtiririko, ama shairi, mara wimbo au zaburi, mara mfano, mara isitiari, mara methali, mara lugha ya picha au lugha ya mafumbo au mtindo wa kiapokaliptiko na kadhalika. Mwishowe, kitabu chake kimoja kiliweza kuwa ndani yake na aina kadhaa za uandishi. Hivi ndani ya Injili, kwa mfano, kunaweza kuwa na historia, masimulizi ya miujiza, mifano, mithali, sala, sehemu ya kiapokaliptiiko na kadhalika. Mfano, chukua Injili ya Marko, ndani yake kuna sura za usimuliaji wa mtiririko, miujiza na mifano, ndiyo sura 1-12 na sura 14-16 na pia sura ya kiapokaliptiko, ndiyo sura 13. Ni lazima msomaji atambue jambo hili kusudi atafsiri atakayoyasoma kwa namna tofauti tofauti.
*Hatima:* Basi, maswali nitakayoyajibu yatahusika na aina tatu za mwanzo za uandishi: hadithi, historia na usimuliaji wa mfululizo.
Mwisho wa somo la nne (maandalizi ya kujibu maswali nisiyoyajibu bado).
*Admin: Fr. Titus Amigu*