Wakati China na Afrika zikiendelea kutafakari kwa kina mafanikio yao tangu kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, FOCAC, mwaka 2000, wadau wanasisitiza umuhimu wa pande mbili za ushirikiano kuwa zingativu ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya China na Afrika.
Kwenye mazungumzo ya FOCAC yaliyoandaliwa hivi karibuni na Kituo cha Sera na Ushauri cha Afrika na China chenye makao yake makuu nchini Ghana, wataalamu waliangazia kwa kina mkutano wa kilele wa FOCAC utakaofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6, kama fursa nzuri ya kuimarisha uhusiano kati ya China na Afrika. Mkutano huo ambao, utawezesha pande mbili kudumisha urafiki wao, kuchunguza ushirikiano wao na kufungua zaidi njia ya kuelekea siku nzuri zijazo.
Kwa juhudi za pamoja za China na Afrika, Mkutano wa kilele wa FOCAC wa mwaka huu wa 2024 unatarajiwa kuwa wa mafanikio makubwa, pia utafungua mtazamo mpya na mpana wa uhusiano kati ya China na Afrika na kuandika ukurasa mpya wa kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.
Kwa mataifa mengi ya Afrika, maendeleo ya China ya kisasa, njia ambayo ni ya maendeleo iliyoratibiwa kwa juhudi za miaka 75 za watu wa China, inasimama kama chaguo jipya, na pia ni msukumo wa mustakabali mzuri unaojikita katika kuheshimiana na kunufaika kwa pamoja.
Ndio maana Waafrika wengi wanaamini kuwa njia hii mpya ya maendeleo ya China ya kisasa iko kinyume kabisa na ile iliyotumiwa na nchi za Magharibi ambazo zilijipatia maendeleo ya kisasa kwa njia ya dhuluma na kuwanyima watu wengi uhuru wao kupitia ukoloni, zikiwakandamiza binadamu na kuwachukulia kama wanyama.
Wahenga wanasema “Mla ndizi husahau, ila mtupiwa ganda hasahau”, cha ajabu ni kwamba udhalimu huo bado umo kwenye vichwa vya watu, na hisia zake hadi leo bado zinaendelea kukumbukwa na watu wa Afrika. Hivyo kupitia FOCAC, nchi zinazoendelea zinataka kudumisha uhuru wao wa mawazo huku zikikua kwa kasi kwa pamoja.
Maendeleo ya kujenga China ya kisasa, yanatetea ustawi wa pamoja na ushirikiano wa kunufaishana. Pia yamekuwa treni ya kasi ambayo kila nchi ya Afrika inataka kupanda na kuhakikisha wanagawana kwa pamoja fursa zinazotokana na maendeleo hayo kupitia ushirikiano wenye nguvu wa FOCAC na pendekezo la “Ukanda Mkoja Njia Moja”, ambao unapunguza utegemezi wa taasisi za mbalimbali za magharibi zikiwemo IMF na Benki ya Dunia.
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Afrika na China katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Johannesburg, David Monyae, alisema nchi za Afrika zinapaswa kuiga mfano wa China, ambayo inalenga kuendesha uchumi wake kwa teknolojia mpya kama vile akili bandia, nyenzo za hali ya juu, bioteknolojia na nishati ya kijani.
Ni ukweli usiopingika kwamba kwenye suala la maendeleo, China imepiga hatua kubwa sana, ikiwa kila siku inajitahidi kuvumbua njia za kuleta maendeleo zaidi kwa nchi yake na dunia. Kupitia juhudi za China za kuleta maendeleo ndani ya nchi yake, viongozi wa bara la Afrika ambalo ni mshirika wa karibu sana wa China, wanapaswa kutumia ushirikiano huu wa FOCAC kuiga mfano huu mzuri ulio mbele yao, ili kuboresha maisha ya watu wao na kuleta maendeleo ya nchi zao.
Katika mkutano ujao wa FOCAC wakuu wengi wa nchi za Afrika watafanya mazungumzo ya moja kwa moja kati yao, na pia na Rais wa China Xi Jinping kuhusu jinsi ya kuupeleka ushirikiano wao ambao umeshazaa matunda matamu katika ngazi nyingine.
Hivyo kabla ya mkutano wa FOCAC kufanyika, inaaminika kuwa karne ya 21 itashuhudia maendeleo ya pamoja na ufufuaji wa China na bara la Afrika, ambalo kwa sasa linazidi kuangalia Mashariki. Na ushirikiano huu kupitia FOCAC unatarajiwa kuleta maendeleo ya kisasa kwa Afrika, yakiungwa mkono kwa kina na China ambayo ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.