Ningelikuwa Ziito Na Amina
Nimekuwa nikifuatilia maisha ya kisiasa ya ndugu zangu hawa wawili yaani Dada Amina binti Chifupa na Kaka yangu Zitto mwana wa Kabwe kwa muda mrefu sana. Zitto tangia akiwa pale Mlimani na Amina tangia alipoanza ule utundu wake katika Radio Clouds. Ni wazi kuwa haiba, ujuzi na fikira za ndugu zangu hawa wawili ni tofauti lakini sina shaka na kushabihiana kwao kuhusu upendo wao wa dhati kwa binadamu wenzao na Tanzania yao, utayari wao wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa letu na zaidi vipaji vyao kisiasa.
Sitaongelea sana kuhusu Zitto lakini kuhusu Amina ambaye ndiye mpaka sasa amekuwa muhanga mkuu wa kadia hili ambaye nathibitisha kuwa nipo tayari kuzama naye. Hapo mwanzoni mimi kama walivyo watanzania wengi mijini ambao tunajiona usomi wetu ni kigezo tosha cha kuamua nani atuongoze na nani asituongoze, nilikuwa mmoja wa watu ambao walikuwa wanapinga kabisa kwa Amina kuwa mbunge.
Kutokana na kugubikwa na taswira ya uchafu dhidi ya dada yangu Amina aliyokuwa akipewa na watu wachache wanaojiona kuwa wao ndio wasafi na wana haki ya kutumia uwezo wao wa umiliki na uandishi wa vigazeti mbalimbali vya udaku, nilikubali kabisa kuwa Amina hafai kuwa kiongozi katika jamii yetu.
Hata hivyo baada ya kuangalia undani wa mwenendo wa uandishi wa habari za kumchafua Amina katika magazeti mbalimbali ya udaku ambayo baadae nikagundua kuwa mengi yanamilikiwa na kusimamiwa na mtu mooja ambaye alikuwa na vita binafsi na Amina niliweza kufungua kichwa changu na kujenga ushawishi wa kutaka kumjua zaidi Amina.
Ndipo siku mmoja mahala fulani nilipopata bahati ya kumsikia Amina akiwa jukwaani mbele ya umati wa vijana wenzake wengi wao wakiwa ni wasomi wanaochipukia. Baada ya kusikiliza kwa makini hotuba ya Dada Amina nikagundua kuwa ni wazi Amina niliyekuwa nalazimishwa na vijigazeti vya udaku na maneno ya watu si huyo ninayemuona mbele mbele. Huyu ni Amina mwenye kipaji kikubwa cha kisiasa na Amina mwenye uthubutu mkubwa wa kusema yale anayoamini bila ya kujali madhara yake kwake binafsi. Ni Amina ambaye yupo tayari kuwa yeye bila ya kujaribu kuwa mtu mwengine kama wanasiasa wetu wengi tuliowazoea walivyo ama watanzani wengi wengelitaka awe.
Kuanzia siku hiyo niligundua kuwa hata kama dada yangu Amina ana mapungufu yake, ni wazi kuwa ana sifa ambazo kama zitathaminiwa, kujengwa na kutumiwa ipasavyo ni hazina kubwa ya taifa letu linalohitaji vijana wenye kuwa na moyo na haiba ya uthubutu kama aliyonayo Amina.
Wengi wamekuwa wakimwona Amina kama kijana mdogo ambaye amekosa wasifu wa kuwa kiongozi katika jamii. Wengi wanamuona Amina kama ni mtu anayependa sifa na asiye na umakini. Wapo wanamuona Amina kama ni mropokaji anayepaswa kudhibitiwa mapema. Wapo wanamuona Amina kuwa ni mfano mbaya wa kimaadili katika jamii yetu. Wapo wanaomuona kuwa ni hatari kwa maslahi ya Taifa. Wapo wanao muona kuwa ni hatari kwa maslahi yao. Wapo pia wanaomuona kuwa ni hatari kwa maslahi ya Chama chake.
Hawa wote wana haki ya kumuona hivyo lakini vilevile ni wazi hawana haki ya kumuhukumu na zaidi wengi wao hawana hata uhalali wa kumuonyesha kidole Dada yetu mpendwa Amina. Waanze kujinyoshea wao kwanza!!!!
Kuhusu haiba yake ya udogo ama utoto ni wazi kuwa wanao kuwa hivyo kunamuondolea uhalali wa yeye kuwakilisha vijana wenzake wwa CCM wanashindwa kuelewa nini maana ya uongozi na zaidi nini maana ya uwakilishi bungeni. Udogo wa Amina ama ukitaka utoto wake ni mchango muhimu katika bunge letu. Maana ya BUNGE kama historia inavyoonyesha ni kuwa mahala ambapo kuna mkusanyo wa uwakilishi wa mawazo ya raia wa aina zote. Udogo ama Utoto wa Amina ni hazina na chachu muhimu kwa maaendeleo ya kimawazo katika jamii na nchi yetu. Kama ni busara za Uzee wapo kina Mzee Malecela, Kingunge, Kabuye, Mama Mongela, Mama Anna Abdalla na wengine wengi tu ambao daima wamekuwa wakitekeleza wajibu huo. zaidi pia wapo vijana kama kina nanihii ambao wakiwa na umri chini ya miaka 40 wanacho ongea hakina tofauti na wazee wa miaka 80 na hawa wameteuliwa eti kwa kigezo cha kuongeza uwakilishi wa vijana bungeni. Wanashindwa hata na Mzee Mzindakaya ambaye ingawa naye tayari amemua kujiunga na kundi la viona mbali kimaslahi, bado maoni na michango yake ina uthubutu wa kiujana akiungana na Rais wetu aliyechaguliwa na asilimia 80 ya watanzania waliopiga kura mwezi desemba 2005.
Kwa wale wanaomuona ni mtu wa kupenda sifa na asiye na umakini ni wazi wanawakilisha utamaduni mbovu wa watanzania wasiokuwa tayari kujitokeza mbele kutenda na kusimamia kile wanachoamini kinahitajika kufanyika katika jamii yetu. Bahati mbaya utamaduni huu unawafanya kila atokeapo mwenzao aliyetayari kuthubutu kutenda na kusimamia kile wangelipenda kitendwe huishi kumuona ni mpenda sifa. Amina ameonyesha kuwa tofauti na wengi wetu kwa kuwa tayari kutenda yale anayoamini anapaswa kuyatenda bila ya watu watasema. Inasikitisha kuwa watu hao hao wanaokimbilia kusema kuwa Amina ni mpenda sifa ndio wasiokwisha kulalama kuhusu mapungufu katika jamii yetu.
Kiongozi mmoja mstaafu barani Afrika aliwahi kunifundisha ni jinsi gani bara letu linavyokwazwa na kile kinachoitwa umakini ama busara. Kwake yeye na nakubaliana naye kwa dhati kuwa mara nyingi tumekuwa tukitumia dhana za umakini na busara katika kuulinda na kuukingia kifua uozo mbalimbali katika jamii zetu. Kijana kama Amina ni wakati wake kuripua yasiyotakiwa kuripuliwa bila ya kujali kile tunachokiita umakini. Umri unamruhusu na maslahi ya jamii yetu yanamhitaji kufanya hivyo. Kama Amina ama Zitto akianza kujizuia kusema ama kutenda yale ambayo yanapaswa kusemwa ama kutendwa eti kwa kuonyesha umakini, Wazee kama kina Mzee Malecela, Kingunge, Mzee Sitta, Mama Mongela, Anna Abdallah na wengine wanafanya nini katika uwanja wa siasa? Hao ndio wenye jukumu la kusimamia kile kinachoitwa Busara na Umakini na mchango wao tunauthamini kama tunavyopaswa kuthamini na kutetea michango ya Amina na Zitto.
Na wale wanaomuona Amina kuwa ni mfano mbaya kwa maadili kwa jamii yetu napenda kuwauliza kosa la ndugu hawa kama kweli wametenda wanachoshutumiwa, ni hilo tendo lenyewe ama kutokana na wao kushindwa kulizuia suala hilo lisifikishwa katika vyombo vya habari kama ambavyo wakubwa wao walio wengi katika ulingo wa siasa na uongozi walivyofanikiwa kufanya. Tunataka kujifanya kuwa haya yanayosemwa kuhusu ndugu zangu hawa wawili ni mageni kwetu? Hivi tumekaa tukajiuliza ni lini suala hili limekuwa dhambi katika jamii yetu iliyojaa ufuska wa kila aina katika kila kona?
Hivi hivyo vinyang'au vidogo walioamua kutumia muda wao kubomoa Nyumba ya dada yetu Amina ambayo ukweli ni kuwa ilishabomoka tangia wakati wa ujenzi wake wanataka kutuambia kuwa wao ni wasafi na ndio maana wengine wanajigamba kwamba piga ua ni marais 2015. Hivi vile vyumba vya uzinzi wanavyomiliki na kulipia kodi za pango kila kukicha katika mahoteli na nyumba kadhaa katika kila pembe za jiji na nchi hii wameshavigeuza makanisa na misikiti kuanza kutubia? Hivi ………… ngoja tu ninyamaze nisije na mimi pia nikahukumiwa kwa kutokuwa na hekima na umakini.
Kwa kweli inasikitisha kuona ni jinsi gani hivi vinyang'au vyeneye nia ya kulinda uozo wao na mabwana zao wanavyoweza kuchezea akili za watanzania kiasi hiki. Ningelikuwa mimi ndio Amina na Zitto ningelifanya yafuatayo.
Kwa kuwa ni wazi sehemu kubwa ya jamii imeshakubali ulaghai wa hivi vinyang'au vinavyochipukia ambavyo vinajitahidi kulinda kulinda uozo wao na wa wengine wa wazazi wao, kwa kuwa jamii imeshaamua kuwahukumu kama wanavyokimbilia kuwahukumu viongozi wetu wengine kutokana na kile kinachoitwa hulka zao, kwa kuwa wao ni vijana na tofauti na hao vinyang'au wao wana nafasi kubwa ya kulibadilisha taifa hili na siku moja tukajivunia, na kwa kuwa kwa muda mchache walio upata wameweza kutusemea vijana wenzao tunachotaka watusemee na kututhibitishia uchungu wao kwa taifa letu sisi vijana wa taifa la leo, na kwa kuwa wao ni vijana waliothibitisha kuwa wapo tayari kujitoa muhanga kwa ustawi wa taifa letu.
Ningewashauri baada ya kushauriana na wale wawapendao na sio wale malaghai waliokuwa wakiwatumia kwa maslahi yao binafsi na kuwakimbia mara tu mambo yanapoeleka kuharibika. Kwa pamoja watoke mbele vichwa juu na hata kama hawajafanya hicho wanachotuhumiwa, wakubali na kuwaomba radhi wale wote waliojenga matumaini kwao kwa kutokuwa waangalifu dhidi ya mbinu za maadui wa masalahi ya watanzania yanayoendelea kukanyagwa na manyang'au wakubwa na hivi vinyang'au vidogo vinavyoota kuwa hadi 2015 watanzania bado tutaendela kulea uozo wao na wao wakawa marais wa nchi hii.
Baada ya kukubali kujitwika kafara hilo wawashukuru watanzania wote waliojitokeza kulizungumzia suala hilo na kuwaomba waendelee kulijadili kwa mapana yake na kuhoji uhalali wa kuendela kunyamazia mambo kama hayo katika jamii yetu ambayo sisi wenyewe tunayafanya na kuyafumbia macho kila kukicha. Wawaombe Watanzania wengi zaidi kujitokeza kuungana nao katika misa na sala maalumu za maungamo binafsi na halafu wajiunge nao katika kuanzisha ukurasa mpya wa kimaadili katika taifa letu. Waungane nao katika kuhoji yale yote yasemwayo vichochoroni kuhusu mporomoko wa maadili katika jamii yetu na zaidi miongoni mwa wale ambao tumewaamini kuwapa madaraka ya kuliongoza taifa letu.
Mimi naamini kuwa kuanzia viongozi mpaka waongozwao kwa pamoja tunapaswa kuchukua hatua za haraka na za kishujaa kusimama kidete kupambana na tatizo la uporomokaji wa maadili binafsi miongoni mwetu. Badala ya kutumia muda wetu mwingi kuwasulubu ndugu zetu hawa tunapaswa kutumia nafasi hii kuleta mabadiliko ya kinyakati ambayo yatatusaidia kulinda utanzania wetu na Tanzania yetu kwa ujumla. Pamoja na hali kuonekana kuwa ni ya kusikitisha naamini kuwa kilichotokea ni nafasi adimu kwa jamii yetu kuweza kuamka na kuukabili ukweli kuwa jamii yetu ina tatizo sugu la ukoseu wa maadili binafsi.
Kaka Zitto na dada Amina, Simameni vichwa juu na shikeni usukani kutuongoza katika mpambano huu muhimu katika kulinda Utanzania wetu. Amkeni tuwakabidhi ufunguo wa Tanzania mpya. Amkeni ndugu zangu tujenge Tanzania iliyo njema kwa wote. Tupo pamoja yenu na daima tutakuwa pamoja.
Pamoja tutajenga Tanzanianjema