Siasa zaharibu ndoa ya Chifupa
*Kisa ni kuutaka uenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM
*Baba yake Amina amzuia kutoa siri kwa waandishi
Na Waandishi Wetu
TALAKA kwa Mbunge wa Viti Maalum-Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amina Chifupa imeingia katika sura mpya baada ya kubainika kuwa kiongozi mmoja wa UVCCM, alikataa ombi la mbunge huyo kutaka ampigie debe katika nafasi ya Mwenyekiti wa umoja huo katika uchaguzi utakaofanyika mwakani.
Chifupa alikaririwa na vyombo vya habari jana akilalamika kuwa, kiongozi mmoja wa UVCCM ambaye pia ni Naibu Waziri na Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri ya CCM, alitumia ushawishi wake kwa mumewe hali iliyosababisha yeye kupewa talaka.
Taarifa zingine zilieleza kuwa, tukio hili la kupewa talaka linahusishwa na kitendo cha Mbunge huyo kuonyesha tamaa ya madaraka ya juu katika UVCCM. Hata hiyo, mbunge huyo alipoulizwa kufafanua ukweli wa dai hilo, hakupenda kubainisha wazi kuhusu dai hili.
Kilichobainika baadaye kufuatia uchunguzi wa gazeti hili ni kuwa, Chifupa amekuwa katika kampeni za chinichini zenye lengo la kutaka kuiongoza UVCCM.
Katika harakati za Mbunge huyo kusaka sapoti, alifika kwa kiongozi huyo wa ngazi ya juu katika UVCCM na kutaka baraka zake. Kiongozi mmoja wa UVCCM aliiambia gazeti hili kuwa, Chifupa alikataliwa bila kuelezwa sababu za kukataliwa kwake.
Habari zaidi zinasema kwamba kiongozi huyo alisema Chifupa hawezi kuwa kiongozi wa umoja huo, kwa madai kwamba hana uwezo wa kushika nafasi nyeti kama hiyo.
Kuna hali ya kuanza harakati za kutaka madaraka katika UVCCM. Kwa sasa makundi yameashaanza kujiandaa huku yakifanya kampeni za chini chini.
Hali hii, inaonyesha kuwepo uchaguzi mgumu kabisa mwakani katika UVCCM na kama utaratibu wa CCM utatumika, kuna uwezekano zoezi la kufungia makada kadhaa kutogombea likafanyika. Ni jambo la wazi kuwa kuna ushahidi wa makundi na baadhi ya makada kuanza kupiga kampeni.
Tukio hili la Chifupa kumhusisha kiongozi mmoja wa UVCCM linabainisha hali iliyopo ndani ya chama hicho. Kinachoelezwa sasa ni kuwa, uongozi wa UVCCM umekuwa ukitumika kama nguzo ya kusaidia kampeni za urais kupitia CCM. Zoezi hili mara kadhaa linawahusisha viongozi wa juu katika serikali na chama, kama inavyoanza kujionyesha sasa.
Mwananchi ilipowasiliana na Mwenyekiti wa UVCCM, Emanuel Nchimbi, ili kupata upande wa uongozi wa umoja huo, simu yake ilikuwa imezimwa. Lakini habari zaidi zinadai kuwa Nchimbi kwa sasa yupo Songea kikazi.
Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti juzi na jana kuwa Amina alitalikiwa na mumewe baada ya kubainika kuwa na uhusiano na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na kwamba mwanaume huyo alichukua uamuzi huo baada ya 'kuumwa sikio' na kiongozi huyo wa UVCCM.
Hata hivyo, Kabwe alikaririwa na gazeti moja jana akikanusha kuwapo kwa uhusiano huo, akisema amemzoea Amina kama Mbunge mwenzake, kuanzia siku walipoteuliwa kuhesabu pamoja kura za wabunge wakati walipokuwa wakithibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Mbunge huyo jana alishindwa kutimiza ahadi yake ya kuzungumza na waandishi wa habari kumtaja Naibu Waziri katika serikali ya Awamu ya Nne anayedaiwa kuvuruga ndoa yake.
Badala yake, Baba mzazi wa Mbunge huyo, Luteni Mstaafu Hamis Chifupa, alifika katika Ukumbi wa Maelezo jijini Dar es Salaam na kutangaza kuwa amemzuia mwanawe kutangaza jambo hilo kwenye vyombo vya habari kwa kuwa ni suala la ndani ya familia.
"Kila jambo linapotokea lina taratibu zake, namna ya kulitatua hivyo hata mgogoro huu wa Amina na mumewe lazima ufuate taratibu zinazotakiwa katika kuusuluhisha, hata kama angekuja kuongea na ninyi angeongelea masuala mengine lakini siyo hili la kuachwa kwa talaka moja," alisema Chifupa.
Luteni Chifupa alikiri kuwa mtoto wake huyo ameachwa na mumewe, Mohamed Mpakanjia kwa talaka moja kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo, alikataa kueleza kwa undani sababu ya kuvunjika kwa ndoa hiyo.
Alisema kwa kuwa suala la kuachwa kwa mtoto wake ni jambo la ndani ya familia, wamemzuia Amina kulizungumzia suala hilo katika vyombo vya habari.
Mbunge huyo jana alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa alitaka azungumze na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kuachika kwake, lakini kinyume na matarajio ya waandishi waliokuwa wamefurika kumsuburi, alijitokeza baba yake na kutangaza kutokuwepo kwa mkutano huo.
Alisema ameamua kufanya hivyo kwa kuwa kigogo huyo wa serikali ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, alikwenda kwa ofisi kwa mumewe na siku hiyo hiyo akapewa talaka, jambo analohisi kuwa lilichangia kuachwa kwake.
Alipoulizwa na waandishi wa habari mahali alipo mtoto wake, Kapteni Chifupa, alisema hajamuona tangu alipoachwa ili wamekuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu.
"Kwa kuwa tuna ndugu wengi siwezi kujua anakaa wapi, licha ya kuwa kwa taratibu za dini ya Kiislamu anatakiwa kukaa eda huku akiendelea kuhudumiwa na mume wake," alisema Chifupa.
Alisema watoto ni sawa na pensheni kwa wazazi, hivyo wameamua kumlinda mtoto wao kwa kulizungumzia suala hilo wakati taratibu nyingine zinafanywa ili kuweka mambo sawa.
Alipoulizwa juu ya sababu iliyomfanya mtoto wake apewe talaka moja, alisema haelewi akisisitiza kuwa hayo ni mambo ya ndani ya familia.