Aibu CCM!
2007-05-07 17:43:59
Na Abdul Mitumba, Makumbusho
Chama cha Mapinbduzi Jijini Dar kimekumbwa na aibu kubwa kutokana na skendo ambalo makada wake wanadaiwa kukutwa wakilifanya usiku wa manane.
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinadai kuwa kitendo hicho kinachofananishwa na kuwanga, huenda kikakifanya chama kuwapa adhabu kali wanachama wake kibao waliohusishwa.
Makada hao wanadaiwa kukutwa usiku wa giza nene wakilishwa pilau na wafadhili wanaodaiwa kuwa wanataka wagombea wao wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho waweze kupita kirahisi.
Baadhi ya wana CCM walio hatarini kuwajibishwa kutokana na tukio hilo la aibu ni wale wa Kata ya Makumbusho iliyopo manipsaa ya Kinondoni Jijini.
Taarifa zinasema wengine walikamatwa na wengine waliruka ukuta kukwepa kuwekwa chini ya ulinzi, wakati viongozi wa CCM ngazi ya wilaya walipowafumania katika ukumbi wa Chasimba uliopo Basihaya Campsite Boko ambako walifichwa wakijiandaa na uchaguzi wa viongozi wa matawi.
Inadaiwa kuwa viongozi na wanachama hao walipelekwa huko na viongozi wa CCM kata ya Makumbusho wakitumia basi dogo aina ya Toyota Coaster yenye namba za usajili T 415 ADK, ambapo baada ya kuwekwa chini ya ulinzi dereva wake amekiri na kwamba bado anadai malipo yake ya sh.80,000.
Tukio hilo lilitokea kati ya saa 4:30 hadi 6:30 usiku, ambapo kabla viongozi wa kata wa CCM wanaomuunga mkono katibu, waliwasiliana na katibu wa CCM Kinondoni, Bw. Abilahi Mihewa juu ya kuwepo kwa tukio hilo.
Bwana Mihewa naye aliwasiliana na Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Bw.John Barongo naye akamjulisha Mkuu wake, Luteni Yusuf Makamba, ambapo alimuagiza Bw. Mihewa kufuatilia kwa kina tukio hilo.
Akizungumza na Alasiri jana ofisini kwake, Bw. Mihewa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho wilaya ya Kinondoni, amesema baada ya kupewa rungu na Makamba, akiwa na vigogo wa CCM kata na wilaya, walikwenda hadi Boko kwa lengo la kuthibitisha kuwepo kwa taarifa hizo.
Akasema walipofika na baada ya mabishano ya dakika kadhaa na mlinzi wa ukumbi huo, hatimaye alikubali kufungua geti ndipo walipowakuta wanachama hao ambao ni wapiga kura na baadhi ya viongozi wanaogombea nyadhifa mbalimbali.
``Kwa kutambua wachofanya ni kosa, baadhi yao waliruka ukuta na kukimbia lakini wengi kati yao tulifanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi na majina yao tunayo,`` amesema Bw. Mihewa.
Akaongeza kuwa ndani ya ukumbi huo, kulikutwa na masufuria matatu ya pilau lililokuwa tayari kuliwa na mmoja kati ya wanachama waliokimbia aliangusha bahasha ndogo 13 za kaki zinazoashiria kuwepo kwa mazingira ya kutembezeana mlungula mwingine wa fedha.
Kufuatia tukio hilo, Bw. Mihewa amesema alimpigia simu mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Mstaafu Fabian Massawe ili akajionee tukio hilo na ikiwezekana awasiliane na vyombo vya usalama kwa hatua zaidi za kisheria.
``Kikatiba DC Massawe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya na baada ya kufika katika eneo la tukio, aliahidi kulishughulikia kisheria na usalama zaidi kwa ajili ya kukisafisha chama,`` amesema.
Amefafanua kuwa kila mtu aliyeulizwa nani aliyewezesha wao kufika Boko, walidai ni viongozi wa CCM kata ya Makumbusho, akiwemo mwenyekiti na katibu mwenezi wa kata na diwani.
Alasiri ilipowasiliana na diwani wa kata hiyo, Bw.Christopher Mutayoba, alikiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini akaruka kimanga kuhusika ambapo alisema wakati hayo yakiendelea, yeye alikuwa amelala nyumba kutokana na kuumwa.
Akizungumzia hatma ya uchaguzi huo, Bw. Mihewa amesema umesimamishwa hadi vikao vya kuwajadili wanachama hao ngazi ya wilaya na mkoa vikapofanyika na Kamati Kuu ya CCM Taifa itakapotoa uamuzi dhidi yao.
Uchaguzi huo wa marudio ungehusisha matawi matatu kati ya tisa ya kata hiyo, ambayo yalishindwa kutoa washindi wakati uchaguzi wa awali ulipofanyika wiki moja iliyopita. Matawi hayo ni Mchangani, Kisiwani na Minazini.
SOURCE: Alasiri
AMA KWELI SASA CCM MAMBO YAKO JUU