SoC02 Katiba Mpya ni haki ya Wananchi, sio huruma ya Watawala

SoC02 Katiba Mpya ni haki ya Wananchi, sio huruma ya Watawala

Stories of Change - 2022 Competition

GoJeVa

Member
Joined
Sep 15, 2021
Posts
41
Reaction score
60
Katiba ni sheria au kanuni zinazoainisha jinsi ambavyo nchi, chama, au shirika vitakavyoendesha shughuli zao.
Kwa upande wa nchi, katiba ni sheria mama inayoainisha misingi mikuu ya kisiasa na kuonesha madaraka na majukumu ya serikali. Katiba za nchi pia huainisha haki za msingi za wananchi. Katika andiko langu hili nitajikita zaidi kudadavua juu ya katiba ya nchi ya Tanzania.

Katiba ya nchi ya Tanzania ina historia kubwa na ndefu toka mwaka 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru kutoka kwa Waingereza hadi sasa nchi hii inajulikana kama Tanzania baada ya muungano wa nchi mbili mwaka 1964 ambazo ni Tanganyika na Zanzibari. Kwa uchache nitataja na kutoa maelezo mafupi juu ya vipindi ambayo katiba ya Tanzania imevipitia kutoka mwaka 1961.

1. Katiba ya Tanganyika 1961.
Muundo wa katiba hii ulikuwa bado una mfumo wa waingereza ndani yake, ambapo malkia alibaki kama mtawala na waziri mkuu alikuwa mtendaji mkuu. Kwa maana hiyo mwaka 1961 Tanganyika ilikuwa na waziri mkuu tuu bila raisi. Hivyo bado Tanganyika ilikuwa na kivuli cha umalikia kutokana na muundo huo wa katiba.

2. Katiba ya Jamuhuri ya Tanganyika 1962.
Hiki ni kipindi cha pili katika historia ya katiba ya Tanzania, ambapo mfumo wa Uraisi uliingia katika katiba. Mfumo huu ulimtambua raisi kama mtawala na kiongozi wa nchi, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuunda serikali.

3. Katiba ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibari 1964.
Kutokana na kuungana nchi mbili yaani Tanganyika na Zanzibari 26/04/1964, ilibidi madiliko yafanyike kwenye katiba ya mwaka 1962 ili kuendana na muungano uliotokea.

4. Katiba ya Muda 1965.
Katika kipindi hiki cha nne, katiba ya muda ilipitishwa ili kuendana na madiliko ya kisiasa, kiuchumi na jamii kutokana na muungano wa nchi mbili uliofanyika.

5. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania 1977.
Hii ndio katiba tunayotumia hadi leo, japo imepitia marekebisho mbali mbali. Katiba hii ilipatika kutokana na tume ya raisi, ambayo ilikuwa na wajumbe 20 kwa kuzingatia idadi sawa kutoka pande zote za muungano. Tume hii iliongozwa na Sheikh Thabit Kombo akisaidiwa na Pius Msekwa kama katibu wa tume. Hata hivyo tume hii ni ileile iliyotunga katiba ya CCM.

Je, kama Taifa tunahitaji katiba mpya? Kama jibu ni ndio au hapana…..inabidi tujadili kwa hoja kuntu, kwa nini jibu ni ndio au kwa nini jibu ni hapana.

Kwa mtazamo wangu, naonelea ni muhimu kama Taifa kutengeneza katiba mpya kutoka na mapungufu mengi yaliyopo katika katiba hii tunayoitumia. Najadili mtazamo wangu huu kama ifuatavyo;

Kwanza kabisa inabidi tufahamu kuwa katiba ndio dira na sheria mama katika nchi, hivyo basi Nchi yoyote isipokuwa na katiba bora lazima itapoteza dira muda wowote.

Namnukuu raisi ya kwanza wa Tanzania Mwl.Julius Kambarage Nyerere aliwai kusema;…. “Katiba hii imenipa madaraka makubwa sana, siku atakuja mtu ataitumia atakavyo na kuwa kama Mungu.” Nitaorodhesha mapungufu yaliyopo kwenye katiba yetu na kutoa maelezo kwa uchache;

1. Kutokuwepo ushirikishwaji wa wananchi katika uundaji wa katiba tunayoitumia.
Kwa sasa tunatumia katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977, ambapo tunajua katiba hii ilitengenezwa na tume ya raisi iliyokuwa na wajumbe 20. Tume hii iliongozwa na Sheikh Thabit Kombo akisaidiwa na Pius Msekwa kama katibu wa tume.

Hata hivyo tume hii ni ileile iliyotunga katiba ya CCM. Ikumbukwe, katiba ni mali ya wananchi sio watawala, katiba ili iwe bora katika uundaji wake inabidi wananchi washirikishwe kwa asilimia mia moja 100%. Watawala wasiunde katiba kwa utashi wao, wala kwa kupenda kwao.

Hadi hapo tunaona wananchi hawakushirikishwa katika uundaji wa katiba hiyo, hivyo si ajabu wananchi hajui kilichomo katika katiba hiyo, ndio maana raisi wa awamu iliyopita Jakaya Mrisho Kikweta alipoanzisha mchakato wa katiba mpya kupitia tume ya jaji Warioba alihakikisha wananchi wanashirikishwa vizuri na hii ilipelekea kupata rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, japo hadi sasa imewekwa kabatini na haijafanyiwa kazi.


2. Katiba iliyopo kutokuwa na tume huru ya uchaguzi.
Katiba iliyopo inampa madaraka raisi wa Tanzania kuteua viongozi wa tume ya uchaguzi, kama vile kumteua mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, pia kuteua wakurugenzi katika halmashauri ambapo ndio wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo.

Pia, ikumbukwe raisi wa Tanzania ndiye mwenyekiti wa chama kinachoongoza nchi, hivyo ni rahisi kwake kupitia ubovu wa katiba kushinda kila uchaguzi kwa idadi ya kura atakayotaka. Kwa muundo wa tume hii ya uchaguzi kupitia katiba yetu ni ngumu chama kilichopo madarakani kushindwa uchaguzi, narudia kusema ni NGUMU..!!!!, Pia aliyekuwa katibu mkuu wa CCM taifa Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliwai kusema; …..“Ukishakuwa chama tawala, kuna dhana inaitwa incumbency advantage, unafuu wa mwenye madaraka, na ukishindwa kutumia unafuu huo utakuwa kama KANU.

Unajua KANU iliposhindwa kutumia nafuu hii haikuwai kurudi maradarakani au UNIP ya Zambia. Unashika dola, alafu unatumia dola kubaki kwenye dola. Halafu akitokea mtu ambaye ana busara akikwambia usitumie dola kubaki kwenye dola usimsikilize, siku ukishatoka hurudi..! hata kwenye kazi, kazi inatafuta kazi…..aliye na dola ananufaika na dola hiyo kubaki madarakani..”.

Kauli tata kama hizi za viongozi zinatishishia ustawi wa demokrasia, na wana dhubutu kutoa kauli hizi kwa sababu ya ubovu wa katiba yetu. Hivyo katiba mpya inahitajika kufanya viongozi wawe wawajibikaji na sio walafi wa madaraka kupitia ubovu wa katiba.

3. Katiba iliyopo inampa madaraka makubwa raisi wa nchi. Ambalo ni kosa kubwa.
Narudia nukuu ya raisi wa kwanza wa Tanzania Mwl.Julius Kambarage Nyerere aliwai kusema;…. “Katiba hii imenipa madaraka makubwa sana, siku atakuja mtu ataitumia atakavyo na kuwa kama Mungu.”. Hivyo sasa inamaanisha raisi wa nchi anapewa madaraka makubwa na katiba na anaweza kutumia madaraka hayo kuumiza watu.

Hitimisho.
Wenye nchi ni wananchi, katiba ni kwa manufaa ya wananchi. Katiba mpya itasaidia matumizi mazuri ya rasimali za Taifa, katiba mpya itazuia ufisadi wa viongozi, katiba mpya itakomesha viburi, ulafi wa madaraka wa viongozi na itaongeza uwajibikaji.
Katiba mpya ni sasa kwa manufaa ya Taifa.

AHSANTENI.

MAREJEO.
1. Kabudi, P.J.A.M., International Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar: A Federal or Unitary State? L.L.M. Dissertation, University of Dar-es-Salaam (1986).
2.Wikipedia, kamusi huru. www.wikipedia.org.
3.Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.
 

Attachments

Upvote 3
Back
Top Bottom