SoC02 Kazi tatu za kumwingizia mwanafunzi pesa akiwa chuoni

SoC02 Kazi tatu za kumwingizia mwanafunzi pesa akiwa chuoni

Stories of Change - 2022 Competition

Prof Sankara

Member
Joined
Sep 17, 2021
Posts
6
Reaction score
10
Utangulizi
Mfumo wa elimu nchini humfanya mwanafunzi azingatie Sana kusoma, Hali ambayo inamfanya kuwa mbali na harakati za kutafuta pesa zake mwenyewe.

Tunajua namna ambavyo shule huchukua muda mrefu mpaka kumaliza kiwango cha shahada ya kwanza.

Kwa kawaida mtu anaweza kuhitimu shahada ya kwanza akiwa na miaka kati ya 22 hadi 25 au zaidi. Kijana akimaliza shadada yake anarudi mtaani akiwa hana maarifa mbadala ambayo anaweza kuyatumia kujipatia kipato. Hili ni tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka ili kumwezesha kijana kusoma na wakati huo huo anakuwa na uwezo wa kuingiza kipato chake mwenyewe akiwa chuoni.

Dhana hii inaweza kumsaidia hata wakati atakapohitimu chuo kuwa na kitu cha kufanya wakati anatafuta ajira. Mwingine anaweza asiwe na muda wa kusaka ajira badala yake anaweza kuendelea na shughuli ambayo imekuwa ikimwingizia kipato akiwa chuoni.

Zifuatazo ni kazi ambazo mwanafunzi wa chuo anaweza kujifunza na kuzifanya na kupata pesa za kutosha.

Upigaji picha
Upigaji wa picha inahitaji kuwa na kamera nzuri na komputa. Vifaa ambavyo mwanafunzi anaweza kuvipata haraka mara tu anapoingia chuo. Kupiga picha ni kazi rahisi kujifunza na kuifanya kwa sababu inafanyika katika maeneo ya chuo au nje ya chuo. Bei za kawida kwa picha moja ambayo ni nakala laini (soft copy) inaweza kuwa elfu mbili hadi elfu tano, (2,000- 5,000). Mwanafunzi atapata urahisi wa kunadi na kuikuza biashara yake kwa wanafunzi ambao kwa kazi yake ndio wateja lengwa. Atapata kazi ya kupiga picha za sherehe wanafunzi kama vile siku ya kuzaliwa, mahafali, paspoti na picha mbalimbali. Iwe mwanamke au mwanamke anaweza kumudu kazi hii kwa ufanisi.

Usanifu wa picha na matangazo
Hapa mwanafunzi anatakiwa kuwa na komputa tu na kuweka program maalum (Adobe Photoshop, illustrator nk) ambazo atazitumia kusanifu picha na matangazo mbalimbali. Mwanafunzi anapaswa kujifunza usanifu kutoka kwa watu waliobobea kwa kuwalipa pesa kiasi.

Kazi ya usanifu anaweza kuifanya muda wowote na popote awapo. Matangazo atayapata kutoka kwa wanafunzi na idara mbalimbali za wanafunzi wa chuo kuhusu mambo mbalimbali kama vile, matukio ya sherehe,mikutano, vikao, matamasha na ziara mbalimbali au hata matangazo ya biashara, mabango na vipeperushi mbalimbali.

Hii ni kazi inayolipa kwa sababu wanafunzi wengi wanapenda kuchapisha picha zao au za biashara zao katika mitandao ya kijamii, kama vile facebook, instagram na twita ambapo wanafunzi wengi ni watumiaji wakubwa wa mitandao hiyo.

Ususi na uuzaji wa bidhaa zake
Wanafunzi wanapenda kupendeza na kwenda na wakati katika masuala ya mitindo ya ususi. Hivyo kama mwanafunzi atajifunza kusuka vizuri ni rahisi kuteka soko kwa sababu wanafunzi wamemzunguka chuoni. Kinachotakiwa ni msusi kupangilia ratiba yake kwa ajili ya kuwahudumia wateja wake. Vifaa vya ususi ni rahisi kuvibeba kwenye begi hivyo halazimiki kuwa na ofisi ya ususi. Ataweza kuuza bidhaa za ususi kwa mteja akiwa anahitaji wakati wa kusuka, vifaa kama vile rasta, mafuta na vilainishi mbalimbali vya nywele na ngozi.

Kutengeneza kucha
Kazi ya urembo ina nafasi kubwa sana chuoni kama mwanafunzi ataamua kuifanya kwa ufanisi. Wanafunzi wanahitaji kutengeneza kucha, kama vile kupaka rangi, na kuweka kucha bandia. Mwanafunzi hana haja ya kwenda mbali kwa ajili ya kutengeneza kucha kama kuna mtu anayetoa huduma hiyo karibu na eneo lake.

Hizi ni baadhi ya kazi ya msingi ambazo mwanafunzi wa chuo anaweza kuzimudu kuzifanya bila kuathiri muda wa masomo yake kutokana na aina za kazi zenyewe kuwa na uwezo wa kufanyika popote na muda wowote.

Hitimisho
Zipo kazi zingine ambazo zinaweza kufanywa na mwanafunzi wa chuo na kujipatia pesa nzuri, kama vile ushonaji wa nguo, upishi wa keki, ushereheshaji, ushinaji wa viatu na upakaji wa kiwi, udalali wa vitu mbalimbali, uuzaji wa nguo, ufundi wa komputa na simu nk.

Hata hivyo baadhi ya kazi ni rahisi kufanyika kwa mwanafunzi anayeishi nje na bweni za chuo, kwa sababu anahitaji kuweka vifaa vya kazi kama vile mashine za kutengeneza keki na cherehani kwa kazi ya ushonaji.
 

Attachments

Upvote 5
Back
Top Bottom