Wakaguongo
Member
- Sep 23, 2026
- 95
- 38
Gazeti la The Standard la Jumatano, Oktoba 28, 2026, limeibua mjadala huu kwa kichwa cha habari “Abductors Paradise”, likiangazia hofu kwamba Kenya inaweza kupoteza nafasi yake ya kuwa kimbilio salama kwa wapinzani wa kisiasa wanaokimbia ukandamizaji katika mataifa yao.
Tukio la hivi karibuni ni kutoweka kwa mwanaharakati wa Tanzania na aliyekuwa kiongozi wa vijana wa chama cha upinzani cha CHADEMA, Twaha Mwaipaya, ambaye aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana katika eneo la Kamulu, kaunti ya Machakos, Oktoba 25, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Amnesty International Kenya, watu hao walikuwa wakitumia magari matatu. Kufikia wakati taarifa za awali zilipochapishwa, mahali alikokuwa na utambulisho wa waliohusika havikuwa vimebainika kwa uhakika.
Hata hivyo, tukio la Mwaipaya si la kwanza kuzua wasiwasi kuhusu usalama wa wakosoaji wa kisiasa kutoka nchi jirani walioko Kenya. Mnamo Novemba 2024, kiongozi wa upinzani kutoka Uganda, Dkt. Kizza Besigye, alitekwa akiwa Nairobi na baadae akajikuta nchini Uganda akikabiliwa na mashtaka.
Aidha Januari 2025, mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai naye alitekwa kwa muda mfupi jijini Nairobi kabla ya kuachiliwa. Matukio haya yameongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa ukandamizaji wa kisiasa kuvuka mipaka na kuwafikia watu wanaotafuta hifadhi nje ya nchi zao.
Kinachozua maswali zaidi ni namna mamlaka za Kenya zinavyoshughulikia matukio haya. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanataka Serikali itoe majibu kuhusu mahali alipo Mwaipaya, ichunguze mazingira ya kutoweka kwake na kuhakikisha usalama wake.
Kwa nchi inayojivunia Katiba inayolinda haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na haki ya kila mtu kupata ulinzi wa sheria, matukio kama haya yanahitaji majibu ya wazi na uchunguzi huru. Mtu anayekimbia vitisho katika nchi yake hapaswi kuishi kwa hofu kwamba anaweza kufuatiliwa na kupotea anapokuwa katika nchi aliyotarajia kumpa usalama.
Zaidi ya suala la usalama wa wanaharakati wa kigeni, kinachowekwa hatarini ni imani katika utawala wa sheria na nafasi ya Kenya kama mshirika wa kikanda anayeheshimu haki za binadamu. Ikiwa watu wanaotafuta hifadhi hawawezi kuwa na uhakika wa usalama wao, ni maswali gani ambayo wakimbizi, wanaharakati na wakosoaji wengine wa kisiasa wataanza kujiuliza kuhusu Kenya?
Ewe mdau, Kenya ilikuwa ikitazamwa kama kimbilio la watu wanaokimbia ukandamizaji wa kisiasa katika nchi jirani. Je, matukio haya yanaashiria mabadiliko katika nafasi hiyo, na serikali inapaswa kufanya nini kurejesha imani kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria?