Hoja kuu zilizompeleka Zitto Z.Kabwe mahakamani ni mbili.Kwanza, kuizuia Kamati Kuu ya CHADEMA kumjadili juu ya uanachama wake kufuatia barua aliyopokea ikibeba tuhuma 11 dhidi yake.Pili, kuiomba Mahakama imuamuru Katibu Mkuu wa CHADEMA kumpatia Zitto mwenenndo wa shauri lake ndani ya Kamati Kuu(siku alipovuliwa wadhifa wake) ili Zitto aweze kukata rufaa katika Baraza Kuu la CHADEMA. Hivyo tu. Lakini,kinachoripotiwa ni tofauti. Hatuwezi kunyamazia upotofu.
Kesi hii imekuwa ikiripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini na nje kwa kukuzwa na kupotoshwa sana. Inazungumzwa kana kwamba ni vita ya kufa au kupona kwa mmoja wa pande za kesi hiyo. Kama si Zitto basi CHADEMA.Kwamba,baada ya hukumu ya leo ya Jaji Utamwa, Zitto au CHADEMA ataibuka kidedea na mwenzake atakuwa ameanguka na kuangamia kabisa.
Upotofu huu ndio uliosababisha yanayoshuhudiwa sasa.Kwamba eti kuna kundi la Zitto na CHADEMA. Kwamba eti kuna vurumai kubwa kati ya makundi hayo. Hakuna haja ya vurugu.Hakuna haja ya sherehe.Hakuna haja ya bifu. HAKUNA haja ya kujipongeza au kusikitika.Haki haihitaji uadui.
Kwa matokeo yoyote ya kimahakama leo, bado michakato ya kichama itaendelea.Kama Mahakama itakubaliana na maombi ya Zitto,basi kikao cha Kamati Kuu hakitamjadili juu ya uanachama wake.Pia, Zitto atapewa mwenenndo na Katibu Mkuu wa CHADEMA na kukata rufaa Baraza Kuu la CHADEMA.
Kama Mahakama itakataa maombi ya Zitto, Kamati Kuu yaweza kuitishwa na kumjadili Zitto hasa kuhusu uanachama wake kuhusiana na tuhuma zilizopo dhidi yake. Kwa namna yoyote iwayo, CHADEMA itaendelea kuwepo. Itaendelea na michakato yake kichama na kisiasa.