MAHAKAMA Kuu Tanzania kesho inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, na wenzake 10.
Zombe na wenzake wanatuhumiwa kuwaua wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi aliyekuwa anaishi Dar es Salaam.
Washitakiwa hao wanadaiwa kuua kwa kukusudia Januari 14, 2006 kwenye msitu wa Pande, Mbezi Luis jijini Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi, Salum Massati, anatarajiwa kutoa hukumu hiyo inayosubiriwa kwa hamu hasa ikizingatiwa kuwa kesi hiyo ilikuwa na mvuto wa aina yake.
Mahakama ilimtaka Zombe na wenzake wajibu mashitaka yanayowakabili, walipewa nafasi ya kutoa ushahidi. Mahakama pia ilichambua ushahidi wa upande wa mashitaka na ule wa utetezi uliokuwa na mashahidi 37.
Awali, washitakiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Abdallah Zombe, Christopher Bageni, Ahmed Makele, F 5912 Noel Leonard, na WP 4513 Jane Andrew.
Wengine ni D6440 Nyangerella Moris, D1406 Mabula, E6712 Felix, D 8289 Michael, D 2300 Abeneth, B 1321 Rashid Lema, D 4656 Rajab Bakari na D1367 Festus Gwabisabi.
Baada ya uchambuzi baadhi ya washitakiwa waliondolewa katika kesi hiyo wakabaki Zombe, Bageni, Makele, WP 4513 Jane, D1406 Mabula, D8289 Michael, D2300 Abeneth, B1321 Rashid, D4656 Rajab na D1367 Philipo.
Mshitakiwa Lema amefariki dunia hivyo mashitaka dhidi yake yamefutwa.
Kesi hiyo ilianza 2006 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji ilihamishiwa Mahakama Kuu.
http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=3226