WATAALAMU wa sheria wamesema aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake tisa waliaochiwa huru katika kesi ya mauaji, hawawezi kushitakiwa tena kwa kosa hilo.
Kauli ya wanasheria hao imetokana na kuwapo kwa taarifa kuwa, serikali inakusudia kukata rufani, kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, uliotolewa Jumatatu wiki hii wa kuwaachia huru.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, aliwaachia huru Zombe na wenzake, waliokuwa wakidaiwa kuwaua wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi, kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Harold Sungusia, alisema kisheria hakuna nafasi tena kwa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi mpya, hata kama anayetafutwa kwa mauaji hayo akikamatwa, hivyo njia pekee ni kukata rufani.
"Hata kama aliyeua akikamatwa kama Mahakama Kuu ilivyoagiza, Zombe na wenzake wanaweza kuitwa kutoa ushahidi tu na si kushitakiwa kwa kuwa itakuwa ni kukiuka misingi ya haki za binadamu, na endapo watafikishwa mahakamani, wataachiwa huru tena," alisema Sungusia.
Kwa upande wake, Wakili Domitian Rwegoshora wa Kampuni ya Uwakili ya MK Partners ya Dar es Salaam, alisema: "Hukumu yoyote ya kesi inatokana na ushahidi unaotolewa, kesi ya mauaji adhabu yake ni kubwa, hivyo kwa ushahidi dhaifu mahakama haiwezi kuwatia hatiani washitakiwa".
Naye Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema hukumu hiyo ilitokana na udhaifu wa Jeshi la Polisi katika kufanya upelelezi.
Lissu alisema wanaopaswa kubeba mzigo ni Jeshi la Polisi, kwa kuwa halina wataalamu wa kisasa wanaoweza kuchunguza makosa ya jinai, hivyo kuwasilisha ushahidi usiojitosheleza.
"Sheria za nchi zote zinataka ili mtu atiwe hatiani kwa kosa la jinai ni lazima kuwe na ushahidi usio acha shaka yoyote kwa mtuhumiwa," alisema Lissu.
Alisema ingawa hajaisoma hukumu ya jaji iliyowaachia huru watuhumiwa hao, lakini anafikiri alichokitumia ni ushahidi uliowasilishwa, hivyo kama haukujitosheleza hawezi kutoa hukumu isiyo na haki.
Wengine walioachiwa huru ni Christopher Bageni, Ahmed Makelle, Rajab Bakari, Philipo Gwabisabi, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shoza na Abeneth Saro.
Walikuwa wakituhumiwa kuwaua wafanyabiashara wa madini Sabinus na Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva wa teksi Juma Ndugu.
Mauaji hayo yalifanyika msitu wa Pande, mkoani Dar es Salaam, Januari, 2006.