Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya
wafanyabiashara wa madini, Abdallah Zombe, ameiomba Mahakama Kuu aruhusiwe kutoa tena ushahidi wake mahakamani hapo ili kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi barua alizodai kuwa zina utata. Barua hizo ni alizodai ziliandikwa na washitakiwa wenzake katika kesi hiyo wakiwa gerezani, ambazo zilielekezwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wakati huo (Geofrey Shahidi) bila kufuata utaratibu wa kuzipitisha kwa Mkuu wa Gereza na zikiwa na tarehe zinazopishana.
Akiongozwa na wakili wake, Jerome Msemwa, Zombe ambaye wakati wa tukio alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Dar es Salaam alidai mbele ya Jaji Salum Massati kuwa anaiomba mahakama imruhusu kutoa tena ushahidi kama ilivyoomba notisi ya wakili wake aliyoitoa Februari mwaka huu ili atoe ufafanuzi ambao hakuutoa wakati akijitetea awali. Mheshimiwa Jaji naomba shahidi namba moja (Zombe) aje atoe tena ushahidi wake mahakamani hapa na naamini hii ni mahakama ya haki, lazima haki itendeke hivyo nyaraka hizo tulizoelezwa zipo kwa DPP ziletwe sasa hivi maana ofisi yake si mbali ili mteja wangu asikilizwe, alidai Msemwa.
Wakati huo Zombe akiwa kizimbani tayari kutoa ushahidi tena, tafrani fupi ilizuka baada ya Zombe kutaka kujitetea mwenyewe kwa kumtaka Jaji asimamie haki itendeke kwa kusema; Jaji naamini hii ni mahakama ya haki
. Hata hivyo, Jaji Massati alimtaka atulie kwani malumbano baina ya mawakili hayajafikia mwisho hadi kumwezesha shahidi kuingilia kati shauri.
Aidha, ombi hilo la kurudia utetezi wake, lilipingwa na mawakili wa serikali pamoja na mawakili wengine wa upande wa utetezi akiwamo, Gaudias Ishengoma anayemtetea mshitakiwa wa pili (Christopher Bageni) na Majura Magafu anayewatetea washitakiwa watano katika kesi hiyo kwa madai kuwa endapo barua hizo zitaletwa mahakamani kama kielelezo na Zombe akapewa nafasi ya kujitetea tena, akiwagusa washitakiwa wenzake, mahakama itoe nafasi ya wao kujitetea vilevile.
Tunaomba suala hili liangaliwe kwa makini sana, wakati ule mawakili wa serikali walibaini kuwa nyaraka nyingine ni za bandia, tunaomba lisichukuliwe kirahisi, tunaomba maelezo ya kina yatolewe ili lisiathiri mwenendo mzima wa kesi, alidai Magafu. Jaji Massati alisema atatolea uamuzi suala hilo leo saa nne asubuhi ili kujua kama atatoa utetezi tena au la, na akamruhusu shahidi pekee wa Zombe kutoa ushahidi mahakamani hapo.
Shahidi huyo, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Samwel Nyakitina (59) akitoa ushahidi wake uliolenga kuieleza mahakama anachofahamu kuhusu utaratibu wa wafungwa na mahabusu kutembelewa gerezani au uandikaji wa barua na washitakiwa kumiliki simu na fedha baada ya Zombe katika ushahidi wake wa awali kulalamikia baadhi ya washitakiwa wenzake walikamatwa na simu gerezani na barua na namna ambavyo aliandika barua za malalamiko kwa DPP na Waziri wa Mambo ya Ndani kupitia kwake, shahidi huyo alionyesha kuwa kinyume na matarajio ya Zombe. Sehemu ya mahojiano baina ya shahidi na Wakili Msemwa mbele ya mahakama hiyo yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili: Shahidi hebu ieleze mahakama utaratibu wa mfungwa au mahabusu kuandika barua na kuipeleka nje ya gereza ukoje.
Shahidi: Akishaandika barua inapita mapokezi kisha inakwenda ofisi ya Mkuu wa Gereza inagongwa mihuri na saini ndipo inaenda nje, bila hivyo inakuwa si halali na ni ngumu kutumika katika ofisi za serikali
..lakini sasa ni juu ya mwandikaji na mpokeaji huko nje.
Wakili: Unasema nini kuhusu barua ya Zombe ya Februari 14, 2007 kwenda kwa Jaji Mkuu Mfawidhi na ile ya kutoka kwa Zombe kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Ndani akimlalamikia kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka amemtengenezea kesi ya mauaji?
Shahidi: (akiwa ameshika barua hizo) Saini ni kama yangu na mihuri ya Gereza la Ukonga, lakini sina ukakika nazo mpaka nikaangalie katika makabrasha yangu maana mmenishtukiza sikujiandaa.
Wakili: Unaiambia nini mahakama kuhusu vielelezo kama simu na fedha ulizowakuta nazo washitakiwa wakati kuwa na hivyo vitu gerezani ni kinyume cha sheria na taratibu za gereza.
Shahidi: (akatoa vielelezo ambavyo ni simu nne) siku ya tarehe 15/09/2006 siwezi kusema hapa mshitakiwa yupi alikamatwa na simu, labda mpaka nikaangalie katika majalada, lakini siku hiyo askari waliwapekua mahabusu 30 na waliotoka mahakamani na wafungwa zaidi ya 1,000 walioenda kazini kama utaratibu unavyoelekeza na walikutwa na simu nne na fedha taslimu Sh 153,000. Tukio hilo sina kumbukumbu zake zote hapa.
Awali katika ushahidi wake, mshitakiwa wa 13 ambaye ni wa mwisho katika kesi hiyo inayowakabili washitakiwa tisa hivi sasa, Festus Gwabisabi alidai kuwa alishiriki kuwapekua watuhumiwa waliouawa katika eneo la Sinza Palestina wakiwa hai siku ya tukio bila majibizano yoyote ya risasi na kwamba alishangaa kusikia kupitia vyombo vya habari siku mbili baadaye kuwa wameuawa.
Akiongozwa na wakili wake Longino Myovela, Gwabisabi alidai akiwa na Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Urafiki, Ahmed Makelle, mshitakiwa wa tatu, alimpekua mtuhumiwa mmoja na kumkuta na bastola moja na mkoba mweusi waliodai una Sh milioni tano na kwa mara ya pili huo mkoba na bastola aliuona mezani kwa Zombe asubuhi ya Januari 15, 2006 walipoitwa kupongezwa kwa kazi nzuri ya kukamata majambazi.
Alidai pia kuwa Zombe aliwafundisha washitakiwa hao namna ya kujieleza pindi watakapoitwa kuhojiwa katika Tume ya Jaji Kipenka kuhusu tukio hilo kwamba waeleze kulikuwa na majibizano ya risasi katika Ukuta wa Posta, Sinza jambo ambalo yeye (shahidi) alilikataa kwani aliwakamata kwa amani bila majibizano na alishauri wapelekwe kituoni kuhojiwa, lakini hakujua walikopelekwa.
Zombe na wenzake wanatuhumiwa kuwaua Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi, Matius Lukombe na dereva taksi, Juma Ndugu katika msitu wa Pande, Mbezi Louis, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Januari 14, 2006. Wakati kesi hiyo inaahirishwa Februari mwaka huu, Jaji Massati aliwaachia huru washitakiwa watatu ambao ni Noel Leonard, Moris Nyangelela na Felix Cedrick baada ya kuonekana kuwa hawana kesi ya kujibu kuhusu mauaji hayo.
SOURCE: Habari Leo