Bubu Msemaovyo
JF-Expert Member
- May 9, 2007
- 4,120
- 3,468
Siri zafichuka kesi ya Zombe
na Asha Bani
na Asha Bani
SHAHIDI wa 14 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi inayomkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake, Sajenti mstaafu D 6829 Constantino, ameiambia mahakama kuwa risasi alizowakabidhi askari hao wanaodai kuzitumia siku ya tukio zilirudishwa kama zilivyokuwa.
Shahidi huyo ambaye ni mtunza silaha katika Kituo cha Polisi Chuo Kikuu Dar es Salaam, alidai usiku wa Januari 14 mwaka 2006 aliwakabidhi askari waliokuwa zamu siku hiyo risasi 68 na bunduki tatu aina ya SMG, na kwamba zote zilirudishwa zikiwa hazijatumika, licha ya askari hao kudai kulikuwa na kurushiana risasi baina yao na majambazi siku hiyo.
Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo na wakili wa Serikali, Angaza Mwaipopo, yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Shahidi hebu ielezee mahakama kuwa unaitwa nani na unafanya kazi gani.
Shahidi: Naitwa Costantino nilikuwa nafanya kazi katika Kituo cha Polisi Chuo Kikuu kama msaidizi wa mkuu wa kituo. Nilikuwa na namba D 2829 kwa sasa nimestaafu.
Wakili: Unakumbuka Januari 14 kuamkia 15 mwaka 2006 kulitokea nini kituoni kwako?
Shahidi: Siku hiyo nilikuwa zamu kituoni na nilitakiwa kuwakabidhi silaha askari waliokuwa zamu (lindo) siku hiyo, ikiwa ni moja ya majukumu yangu ya kawaida.
Aliendelea kueleza kuwa aliwakabidhi silaha tatu ikiwa ni bastola moja na bunduki aina ya SGM mbili, zikiwa na risasi 68 ambazo alidai hazikutumika.
Constantino alidai silaha hizo aliwakabidhi askari D 1406 Koplo Emmanuel, F 5612 PC Noel, na D 901 Lema, ambao aliwatambua mahakamani. Wengine ni Koplo James na Sajenti Alawi, ambao hawakuwapo mahakamani.
Alidai asubuhi ya Januari 15 aliingia ofisini kwa mkuu wa kituo (OSS) Sebastian Masinde na kukuta Polisi zaidi ya 10 wakiwa wanapongezwa kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuua majambazi usiku uliopita.
Alinukuu maneno ya Masinde: "Hongereni sana vijana wangu mmejitahidi kupambana na majambazi, hongereni sana, mmefanya kazi nzuri." Alidai baada ya kusikia hivyo aliuliza kuna nini? Akaambiwa kuwa askari hao wamefanikiwa kupambana na majambazi na kwamba wameua majambazi wanne, na yeye akadai kuanza kuwapongeza pia.
Aliendelea kuidai kuwa baada ya hapo hawakuandika ripoti yoyote ya tukio kama kawaida yao na badala yake askari hao waliitwa Kituo cha Polisi Oysterbay na hakujua kilichoendelea.
Naye shahidi wa 12 katika kesi hiyo, Zainabu Hashim (33), mfanyakazi katika Hoteli ya Bondeni, alidai siku ya Januari 18 wakiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili walifika askari polisi zaidi ya 10 waliokuwa wamefuatana na Zombe huku wakiwa wamevalia soksi usoni na kubakisha macho (mask).
Alidai askari hao waliokuwa wameambata na Zombe waliruka kwenye gari la Polisi la wazi walilokuwa wamepanda na kuvamia msikitini wakati wa ibada ya mwisho ya kumuombea marehemu Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi ikiwa inaendelea.
Alidai watu waliokuwepo katika eneo la tukio walishangaa na wengine kuanza kukimbia kwa kuwa si tukio la kawaida.
Sehemu ya mahojiano kati ya Zainabu na wakili Angaza Mwaipopo yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: shahidi hebu iambie mahakama kuwa unajishughulisha na nini.
Shahidi: Najishughulisha na shughuli za uhudumu katika Hoteli ya Bondeni iliyopo Magomeni.
Wakili: Unaweza ukawakumbuka wateja waliokuja kwako siku ya Januari 13 na 14 mwaka 2006?
Shahidi: Nawakumbuka na niliwarekodi katika kitabu cha kumbukumbu nikiwa kama mhudumu (receptionist).
Wakili: Unaweza ukawataja ni kina nani waliokuja siku ya Januari 13 na kulala hadi 14 mwaka 2006?
Shahidi: Nawakumbuka kwa kuwa walikuwa wateja wetu tangu mwaka 2003 ambao ni Sabinus Chigumbi, Ephraim Lunkombe na Mathius Lunkombe.
Wakili: Unakumbuka nini siku ya Januari 15 mwaka 2006?
Shahidi: Nakumbuka siku hiyo nikiwa hotelini nilipokea simu kutoka kwa Ngonyani ambaye ni ndugu wa marehemu na alinitaarifu nifunge chumba cha marehemu, ikiwa ni pamoja na kunitaarifu kuwa kina Jongo wamekamatwa na Polisi.
Alidai wakati anakwenda kufunga chumba na kutoa vitu vya marehemu hao alimkuta msichana aliyemtaja kwa jina la Stella ambaye alidai kuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Jongo.
Alieleza alimtaka Stella atoke ili afunge mlango sambamba na kukusanya vitu vya marehemu na kuvihifadhi hadi watakapojua kinachoendelea.
Alieleza baada ya kukusanya vitu hivyo na kuvitunza alipiga simu kwa askari Polisi Mbaraka Kituo cha Urafiki, ambaye mke wake anafanya naye kazi na kumuuliza kama anafahamu lolote kuhusiana na kukamatwa kwa watu hao.
Alidai Mbaraka alimwambia awaambie ndugu wa marehemu kwenda nyumbani kwake kwa ajili ya mazungumzo na wakafanya hivyo, baada ya kufika nyumbani kwa Mbaraka aliweza kuzungumza nao na kuwataarifu kwamba wale watu waliokamatwa wameuawa kwa tuhuma za ujambazi.
Kwa upande wake, shahidi wa 11, Jaffer Amir Jaffer (3 ambaye ni mfanyabiashara katika duka la kuuzia vito vya thamani eneo la Mkunguni, Kariakoo, aliiambia mahakama kuwa waliouawa hawakuhusika na wizi katika duka lake, Januari 14 mwaka 2006.
Jaffer alidai kuitwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuwatambua majambazi hao ambao aliwaona wakiwa wanne, lakini hakuweza kuwatambua.
Alidai anakumbuka Januari 14 mwaka 2006 akiwa dukani kwake walifika watu wawili na kuulizia mkufu wa dhahabu na alipowatajia bei walitaka wapunguziwe.
Alidai baada ya kuomba kupunguziwa bei, ghafla aliingia mwanamke ambaye pia aliulizia mkufu huo na ghafla aliondoka akaingia tena mwanamume mmoja ambaye alimuonyesha silaha kichwani na kuchukua vito alivyokuwa anaviuza.
Shahidi huyo alieleza wakati ameinama kutaka kuchukua silaha walimvamia na kumkandamiza kiunoni na kushindwa kuichukua na kisha kumnyang'anya silaha hiyo.
Alidai kufanikiwa kuchukua vito hivyo na wakati wanaondoka walikuwa wanarusha silaha na pia kumjeruhi mlinzi wake aliyekuwa mlangoni.
Alidai kuwa wale aliowaona mochwari wakiwa wamehifadhiwa hawahusiani na waliokuwa wamemuibia dukani kwake, na kwamba hata akiwaona leo atawafahamu.
Shahidi mwingine wa 12 Koplo John katika Kituo cha Msimbazi anayejishughulisha na kupokea simu za matukio mbalimbali na kusambaza katika vituo vingine (control room), alidai siku ya Januari 14 -15 mwaka 2006 hapakuripotiwa tukio lolote la ujambazi linalohusiana na kurushiana risasi kati ya askari na majambazi.
Alidai tukio ambalo liliripotiwa ni la ujambazi wa Kampuni ya mafuta ya BIDCO OIL, ambalo lilitokea siku hiyo na unyang'anyi wa gari, lakini majambazi hao hawakufanikiwa kunyang'anya gari hilo.
"Siku hiyo hakuna simu yoyote au taarifa kupitia chumba cha mawasiliano (control room), zilizokuwa zinasema kulikuwa na majibizano ya risasi au kuna majambazi maeneo ya Sam Nujoma yalirushiana risasi na Polisi,"alieleza Koplo John.
mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Kontebo Jane Andew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emanuel Mabula, Koplo Felix Sedrick, Konstebo Michael Shonza na Koplo Abeneth Salo.
Wengine ni Koplo Rashid Lema, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Wabisabi.
Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Januari 14 mwaka 2006 waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis.