SHAHIDI wa 36 katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake 12 wanaokabiliwa na kesi ya mauaji, Sydney Mkumbi, amedai mtuhumiwa wa 11 katika kesi hiyo, Rashid Lema ana kikaratasi chenye maelezo waliyopewa na Zombe wakaandike.
Mkumbi alidai alipomhoji mtuhumiwa huyo, alimuonyesha maelezo hayo, lakini mtuhumiwa huyo alisema hatamwamini mtu yeyote kumkabidhi karatasi hiyo hata mkewe, kwani anaamini maelezo hayo yataweza kumsaidia siku za usoni.
Alidai karatasi hiyo ina maandishi ambayo yameshachapwa na alipewa na Zombe ayasome, ili aende kuzungumza katika Tume ya Jaji Musa Kipenka iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza mauaji hayo.
"Alinionyesha karatasi aliyodai kupewa na Zombe ambayo ilikuwa na maelezo ambayo aliwaambia wakayaseme katika Tume ya Jaji Kipenka, lakini pia alisema hataweza kumuamini na kumpa mtu yeyote hata mkewe, kwani anaamini yatakuja kumsaidia hapo baadaye," alidai Mkumbi.
Aidha, Jaji Kiongozi Salum Masati anayesikiliza kesi hiyo, alimhoji shahidi huyo kuwa wale askari wanaoshitakiwa kwa kosa la mauaji wangeweza vipi kuzuia mauaji yale baada ya kupata amri ya mkuu wao wa kazi.
Mkumbi alijibu askari wale walipaswa kutekeleza amri hiyo kama walivyofanya, lakini waliporejea walipaswa kuwasiliana na maofisa wengine na kueleza kila kitu kilichofanyika.
Alidai askari hao hawakufanya hivyo badala yake walidanganya, yote ikiashiria walikuwa wamepanga njama ya kutekeleza mauaji hayo.
Alidai ni kosa kwa askari wa chini kutotekeleza amri halali ya mkuu wake wa kazi na hata askari hao walipokuwa wanakwenda na watuhumiwa katika msitu wa Pande walikuwa sahihi, lakini utekelezaji wa amri hiyo haukuwa sahihi.
"Kazi ya askari ni kuzuia kosa lisitendeke, lakini pia kutekeleza amri ya wakuu wake wa kazi hivyo kama waliona wametekeleza amri isiyo halali baada ya kutoka msituni walipaswa watoe taarifa kwa maofisa wengine na si wale waliowatuma," alieleza Mkumbi.
Aidha, shahidi huyo alikana kuwapo kwa sampuli mbili za uchunguzi wa damu walizozipeleka katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Alidai achokijua yeye kuwa ni kupeleka sampuli ya udongo uliochanganyika na damu kutoka katika msitu wa Pande na si Sinza kama shahidi wa 31, Nickobay Mwakajinga, alivyodai mahakamani hapo alipokuwa akitoa ushahidi wake.
Alidai kama Nickobay alifanya hivyo, basi ni katika kipindi kingine, lakini si katika uchunguzi wa timu yake.
Baada ya kufunga ushahidi wake, wakili wa utetezi, Majura Magafu alitaka kujua kama alishawahi kusikia kuwa askari hao walichukua fedha za wafanyabiashara waliouawa kwa madai ya ujambazi.
Shahidi huyo alidai aliwahi kuyasikia, lakini hakuwahi kuyafanyia upelelezi kwa kuwa ni kosa la wizi na yeye kwa wakati huo alikuwa anashughulikia suala la mauaji.
Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo na Wakili Magafu yalikuwa kama ifuatavyo:
Myovela: Mbali na ushahidi wa Rashid na Rajabu kuna ushahidi mwingine mlioupata?
Shahidi: Ndiyo, nimesikia watuhumiwa wakiwa gerezani waliandika maelezo mengine ambayo hayakuwa tofauti na yale waliyoyatoa mtuhumiwa wa 11 na wa 12.
Myovela: Hivi shahidi unafikiri kwamba endapo Rajabu na Lema wasingeandika maelezo hayo mngeweza kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani?
Shahidi: Uchunguzi nilioufanya ungeniongoza kufikia hatua hiyo ya watuhumiwa kupelekwa mahakamani.
Myovela: Ni kosa kwa askari wa chini kukataa kutii amri ya mkuu wake?
Shahidi: Ndiyo ni kosa.
Aidha, shahidi wa 37 katika kesi hiyo, Mkemia Mkuu daraja la pili katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias, alidai ofisi yake ilipokea ombi moja la uchunguzi wa sampuli nne za damu zilizoletwa na Ofisi ya Upelelezi wa Kituo cha Polisi Osterybay.
Alidai alitakiwa kuchunguza kuwa sampuli hizo nne kuwa ni za damu ya binadamu, mnyama na kundi la damu na wala hakupokea ombi jingine kutoka Makao Makuu ya Polisi.
Alidai alishindwa kutambua kundi la damu hizo kutokana na chembe chembe zilizokuwa zimeharibika, hivyo hakukuwa na uwezakano wa kujua ni damu ya kundi gani.
Baada ya mkemia huyo kumalizia kutoa ushahidi wake, Wakili Magafu alimuuliza shahidi huyo kuwa ni kemikali gani wanayotumia katika kutambua sampuli hizo.
Shahidi huyo alidai alitumia kemikali inayoitwa Anti Sera na pia kuna kemikali za kutambua kama damu ni ya mnyama au binadamu.
Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Magafu na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:
Magafu: Damu ikikaa kwa wiki nane au wiki tatu inaweza kutambulika?
Shahidi: Inategemea na hali ya eneo la tukio, lakini damu inaharibika kutokana na mvua, jua, umande na kupitapita kwa watu.
Magafu: Je, nikikuambia kuwa damu iliyoletwa ilikuwa ni moja, lakini katika makundi tofauti utasemaje?
Shahidi: Hilo mimi sijui, inawezekana lakini kazi yangu haikuwa hiyo bali ni kufanya uchunguzi kulingana na ombi la Polisi.
Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Noel Leornad, Jane Andrew, Moris Nyangelela, Emanuel Mabula, Felix Cedrix, Koplo Michael Abeneth, Koplo Rajabu, PC Rashid Lema na Festus Bwabisabi.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya maujai hayo Januari 14 mwaka 2006, ambapo waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini, ambao ni Ephraim Chigumbi, Sabinius Chigumbi na Mathias Lunkombe na dereva teksi, Juma Ndugu. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo.