Endelea kusoma.........
KESI YA BABU SEYA
Nguza Viking(Babu Seya) na Johnson Nguza(Papii Kocha) ni wananchi kutoka nchini Kongo ambao walihamia nchini kwajili ya shughuli zao za mziki. Wanamziki hao pamoja na wenzao watatu(Mwalimu, Nguza Mbangu na Francis Nguza) ambao hata hivyo walifutiwa mashitaka na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu(Mwalimu) na Mahakama ya rufaa(Francis Nguza & Nguza Mbangu) hasa baada ya mahakama hizo kutowakuta na hatia kwenye kosa la ubakaji wa pamoja(Gang rape) kinyume na kifungu cha 131A cha kanuni ya adhabu, walishitakiwa kwa makosa 10 ya ubakaji na 11 ya ulawiti na mahakama ya mkazi Kisutu kuwakuta na hatia na kuwahukumu kifungo cha maisha jela.
Kutokana na wingi wa hukumu za kesi hii na kutokana ukweli kwamba ushahidi na utetezi ndio msingi katika kila uwamuzi wa kesi yoyote, pamoja na usumbufu unaoweza kujitokeza katika baadhi ya sehemu za ushahidi na utetezi wa kesi hii, nimekusudia kuweka mambo hayo hadharani kutokana na umuhimu wake ili tuweze kujifunza na kujua mambo kadhaa yanayotokana na kesi hii.
USHAHIDI NA UTETEZI
_Ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama ulionesha kwamba mwaka 2003 Aza Hussein(PW12-Prosecution witness/shahidi wa 12 wa upande wa mashitaka), Rehema Mgweno(PW5), Alacia Longino(PW3), Agneta Sia(PW 14), Isabella Angowile(PW9), Juliet Mbariki(PW8), Dei Jaffari(PW13), Gift Kipwapwa(PW2), Yasinta Mbele(PW11) na Amina Shomari(PW5) wote wakiwa ni wanafunzi wa darasa la kwanza wa shule ya msingi Mashujaa._
_Mtu anayefahamika kwa jina la Candy David Mwaivaji(PW1) alikuwa ni mlezi wa PW2(Gift) na walikuwa wakiishi pamoja. PW2 ambaye wakati huo alikuwa msichana wa miaka 7, alikuwa ni mtoto wa shemeji yake PW1(Candy). PW1 mbali na kuishi na mtoto huyo, alikuwa pia anaishi na msichana wa kazi anayeitwa Selina John._
_October 8, 2003 wakati wa usiku, Candy alihisi harufu mbaya iliyotoka kwa PW2. Licha ya kumtaka kwenda kuoga, PW1 aliendelea kuhisi harufu hiyo kutoka kwa mtoto huyo hata baada ya kutii agizo la kwenda kuoga._
_Siku iliyofuatia wakati ambao PW2 alikuwa ameenda shule, PW1 alijaribu kumuuliza Selina(msichana wa kazi) kwanini harufu ile mbaya(foul smell) iliyokuwa inatoka kwa PW2. Selina alimueleza kuwa alimuona PW2 akiwa na shilingi 200 na alipomuuliza ni wapi ameipata, PW2 alimjibu ameipata pesa hiyo kutoka kwa mtu anayeitwa Babu Seya @ Nguza ambaye ni mwanamziki. Hii ilimfanya PW1 kuwa na wasiwasi._
_Baada ya PW2 kurudi kutoka shule, alimuuliza ni kwanini Babu Sea alimpa pesa ile. Kwa mujibu wa PW1 anasema PW2 alikuwa muwazi sana. Msichana huyo alieleza jinsi alivyokutana na Babu Seya ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza alivyomrubuni kwa kumpa soda na jojo. Mwisho alifanikiwa kumpeleka chumbani kwake. Baada ya kufika chumbani, alimwambia afumbe macho, kisha akamfunga kitambaa cheusi machoni na kumvua nguo kabla ya kuanza kufanya naye mapenzi ikiwa ni pamoja na mtoto huyo kumnyonya sehemu zake za siri (Nimelazimika kupunguza baadhi ya maneno makali)_
_Mrufani huyo namba moja, baada ya kitendo hicho alimtishia PW2 kumpeleka polisi na kumkata masikio endapo angemwambia mtu yeyote kuhusu kitendo hicho. PW2 pia alimwambia PW1 kuwa sio yeye peke yake aliyefanyiwa hivyo na mtuhumiwa. Aliwataja wahanga wengine._
_Baada ya PW1 kumchunguza PW2 kwenye sehemu zake za siri, alibaini uwepo wa damu na usaha na ndipo aliamua kumpeleka hospitali ambapo alipimwa na kukutwa na ugonjwa wa kisonono na kupatiwa matibabu._
_Mbali na kuripoti tukio hilo polisi, PW1(Candy) akisaidiana na Gift(PW2), walianza kutafuta makazi ya wahanga wengine wa vitendo hivyo vya jinai. PW1 alifanikiwa kuwafahamisha wazazi na walezi wa watoto hao waliofanyiwa mambo hayo na watuhumiwa. Kwa mujibu wa ushuhuda(testimony) kutoka kwa wazazi, walezi na ndugu wa walalamikaji(watoto wanaodai kubakwa na kulawitiwa), walisema walalamikaji wote walikiri kushiriki vitendo hivyo na watuhumiwa(Papii Kocha & Babu Sea)._
_Hawa ni Aisha Mrutu(PW4), mama wa Alicia Longino(PW3); Hadija Omari(PW6), mama wa Rehema Mgweno(PW5) na Congesta Audax(PW7), mama wa Juliet Mbanki(PW8). Wengine ni Mary Victory Chitumbi(PW10), mama wa Isabella(PW9); Brigetha Kamenya(PW16), Bibi wa Dei Jaffari(PW13); Hassan Gamaka(PW17), Baba wa Aza Hassan(PW12); John Mbele(PW18), Baba wa Yasinta Mbele(PW11); Lilian Mbawala(PW19), mlezi wa Agnesta Sia(PW14) na Amina Zuberi ndugu wa Amina Shomari(PW15)._
_Kwa mujibu wa mashahidi, walalamikaji wote walieleza kuwa vitendo hivyo vilifanyika kwenye nyumba No. 607 iliyopo Sinza ambapo walisema palikuwa makazi ya mtuhumiwa namba moja(Babu Seya). Kilichokuwa kinafanyika ni kwamba, walalamikaji (watoto) walikuwa wanapelekwa kwenye makazi hayo ya mtuhumiwa huyo na kuambiwa wavue nguo na mtuhumiwa huyo ku'oil sehemu zao za siri na kisha kufanya nao mapenzi kwa njia zote za siri(nimepunguza ukali wa maneno). Wengine walikuwa wanawekwa kwenye magodoro kitandani na wengine kwenye magodoro sakafuni. Pia walikuwa wanaambiwa na mtuhumiwa kunyonya sehemu zake zote za siri(Nimeondoa maneno makali)._
_Vitendo hivi vilifanyika mara kadhaa kati ya April na October 2003. Wahanga wote walifanyiwa vipimo na Dk. Petronila Ngiloi(PW20), ambaye ni mtaalamu wa magonjwa wa watoto(specialist paediatric). Kwa mujibu wa maoni yake ya kitaalamu(expert opinion), Dk Ngiloi alisema Alicia(PW3), Gift Kipwapwa(PW2) na Amina Shomari(PW5), walilawitiwa(they were sodomized), huku Aza Hassan (PW12), Juliet Mbareki(PW8), Isabella Angomile(PW9) na Dei Jaffari(13) iligundulika wamebakwa. Agnesta Sia(PW14) na Yasinta Mbele (PW11) walikuwa wamebakwa na kulawitiwa._
_Kati ya watoto 10 ambao walifanyiwa vitendo hivyo, ni mtoto mmoja tu Rehema Mgweno ambaye alikuwa salama kwa mujibu wa ripoti ya daktari huyo. Hata hivyo, ushahidi wa Hadija Omary(PW6) ambaye ni mama wa PW5(Rehema), ulikuwa kwamba uchunguzi wake wa macho ulionesha sehemu za siri za mwanae zilikuwa zimepanuliwa(en larged). Kwa ushahidi huu, watuhumiwa walikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela._
_KATIKA UTETEZI WAO, watuhumiwa wote walikana mashitaka na wote kujikita kwenye utetezi wa kuwa mbali na eneo la tukio(alibi). Kila mshitakiwa alieleza kuwa kulingana na kazi waliyokuwa wanafanya kwajili ya kuishi(muziki), hasa kwa mrufani namba mbili (Papii Kocha) ambaye ni mwanamziki anayefanya shughuli hiyo kila siku na wakati mwingine kufanya shughuli hizo nje ya DSM, hivyo isingewezekana wao kuwa kwenye eneo la tukio(locus in quo) na kufanya makosa hayo ambayo wanatumiwa nayo._
_Vilevile mtuhumiwa huyo aliiambia mahakama kuwa, alikuwa hanithi(impotent) hivyo asingeweza kufanya vitendo hivyo. Alisema pamoja na kwamba aliomba upande wa mashitaka kumsaidia kufanya uchunguzi wa tatizo hilo, majibu aliyopata yalikuwa hasi._
_Utetezi mwingine uliowasilishwa kwenye mahakama za juu ulikuwa ni pamoja na kupinga ushahidi uliotolewa na watoto hao wenye umri kati ya miaka 6-10 kuwa haukukidhi matakwa ya kifungu cha 127(7) cha sheria ya ushahidi kinachohitaji mtoto anayefanyiwa kiapo na mahojiano(voire dire examination) kuwa na ufahamu kuhusu kiapo hicho. Wakili wa kina Babu Seya pia hakusita kutumia kesi ya Juma Sunday dhidi ya Jamuhuri ambayo pia uwamuzi wake unashabihiana na kifungu hicho. Wakili huyo pia aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakimu aliyewahukumu wateja wake alijikita kwenye kifungu cha 127(2) ambacho pamoja na mambo mengine, kinatoa uzito wa kipekee kwenye ushahidi unaotoka kwa mtoto hasa yule ambaye ni mhanga(victim)._
_Hata hivyo, licha ya kupitia kwenye mahakama zote za ndani (exhaustion of local remedies) na mahakama hizo kuendelea kuwakuta na hatia, Babu Seya pamoja na mwanae Papii Kocha wamepeleka maombi yao kwenye mahakama ya Afrika._
Mwisho, nimejitahidi sana kufupisha andiko hili kwa nia njema ya kutokukuchosha hivyo nimelazimika kutoweka kila kitu. Mengi yamezungumzwa sana kuhusu kesi hii, lakini naamini baada ya kusoma andiko hili sasa unaweza kufanyia kazi maneno ya JK, ''akili za kuambiwa changanya na zako.
Asante.
--------------
Bob Wangwe