Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Jaji Kiongozi Fakhi Jundu
Kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda imeendelea kusikilizwa, huku upande wa waleta maombi wakijibu hoja za pingamizi zilizowasilishwa awali na serikali.
Wanaosikiliza shauri hilo hilo ni jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakhi Jundu Majaji wengine ni Dokta Fauz Twaib na Augustine Mwarija ambapo awali upande wa serikali ulikuwa na hoja tano ambazo mawaliki wa LHRC na TLS walitakiwa kuzitolea majibu.
Wakili kutoka upande wa waleta maombi, Jeremia Mtobesya akijibu maombi hayo alisema kuizungumzia hoja hiyo ni sawa na kuifanya mahakama kuingia katika msingi wa shauri lenyewe.
Miongoni mwa hoja ni ile iliyosema kuwa mahakama hiyo haiwezi kutolea maamuzi maombi ya LHRC na TLS.
Wakili huyo alidai hatua ya serikali kusema kuwa mahakama hiyo haiwezi kusikiliza na kutolea uamuzi maombi yao ni sawa na kuongelea suala la maombi ambayo yanatokana na kesi ya msingi katika hatua za awali.
Aidha, kutokana na sababu hiyo, Mtobesya aliiomba mahakama hiyo itupilie mbali hoja hiyo ya serikali kwa kuwa haina msingi wowote.
Katika pingamizi lao la awali, upande wa serikali unadai kuwa kesi hiyo ni batili Kikatiba kwa sababu inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Haki, Mamlaka na Kinga za Bunge ambazo zinakataa suala lililotokea wakati wa shughuli za Bunge kutohojiwa au kujadiliwa na chombo chochote.
Kesi hiyo imehairishwa na itaendelea kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 11, mwaka huu ambapo upande wa waleta maombi utaendelea kujibu hoja za pingamizi la tatu na la nne lililotolewa na serikali.
CHANZO: NIPASHE