Balozi Costa Mahalu kortini Dar kwa kuhujumu uchumi, wizi.
Na Nora Damian.
Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, ambaye sasa amerejeshwa nyumbani, jana alipandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kwa makosa sita ya uhujumu uchumi, wizi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh2 bilioni.
Balozi Mahalu alitiwa mbaroni na maafisa wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takuru) pamoja na watu wengine wawili waliokuwa maofisa wa Ubalozi wa Tanzani nchini humo ambao nao wanaohusishwa na tuhuma hizo. Wengine ni Steward Migwano ambaye alikuwa Mtunza Fedha na Grace Martin ambaye alikuwa Afisa Utawala ubalozini hapo.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo ya Kisutu jana asubuhi wakiwa kwenye gari la Takuru aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili T385 ALK na kusomewa mashtaka hayo yanayohusiana na upotevu wa Euro 2,065,827.60 wakati wakiwa maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Euro ni sawa na Sh1,692.74.
Wakiwa bado nje ya majengo ya mahakama hiyo wakisubiri kuingia mahakamani, Profesa Mahalu akiwa amevaa suti nyeusi, alipowaona waandishi wa habari na wapiga picha wa vyombo mbalimbali, alikimbia na kujificha ndani ya gari lililowapeka mahakamani hapo.
Takribani nusu saa baadaye, Balozi Mahalu akiwa na wenzake alioshitakiwa nao, walishuka kwenye gari hilo na kuingia mahakamani huku muda wote kabla ya kuingia katika chumba cha mahakama akionekana akibofya simu yake ya mkononi huku akiwa ameinamisha uso wake chini.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Sivangilwa Mwangesi na kusomewa mashitaka sita na waendesha mashitaka.
Katika shitaka la kwanza, Wakili wa serikali, Joseph Haule, alidai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko Italia.
Aliendelea kudai kuwa katika shitaka la pili, watuhumiwa hao walimpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi, kwani Septemba 23, 2002 katika ubalozi wa Italia jijini Roma, washitakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58 maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.
Mwendesha Mashitaka huyo wa serikali aliendelea kudai kuwa shitaka la tatu ni la matumizi ya hati za kupotosha, akidai kuwa Oktoba Mosi, 2002 washitakiwa wakiwa waajiriwa wa serikali kwa pamoja walisaini mkataba wa mauzo ambao ulikuwa na maelezo ya uongo na yenye lengo la kumdanganya mwajiri wao yaliyoonyesha kuwa ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia ni euro 3,098,741.58.
Alieleza kuwa shitaka la nne linahusu matumizi ya hati za kupotosha ambazo washitakiwa walizitumia Oktoba Mosi, 2002, kuonyesha kuwa muuzaji wa jengo la ubalozi mjini Rome alipokea Euro 3,098,741.58, huku wakijua kwamba ni uongo.
Katika shitaka la tano, mwendesha mashitaka mwingine wa serikali, Tabu Mzee, alidai kuwa Oktoba Mosi, 2002 katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, washitakiwa hao kwa pamoja waliiba euro 2,065,827.60 ambazo zilikuwa mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika shitaka la sita, Mzee alidai kuwa Oktoba Mosi mwaka 2002, washitakiwa waliisababishia hasara Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Euro 2,065,827.60.
Washitakiwa wote walikana mashitaka yote na upande wa mashitaka uliiomba mahakama itaje tarehe nyingine ya kuendelea kwa kesi hiyo kwa madai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Wakili anayewatetea washitakiwa hao, Alex Mgongolwa, aliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake kwa kile alichodai kuwa ni watu ambao kitaaluma hawawezi kuruka masharti ya dhamana.
Katika mazingira ambayo upelelezi wa kesi bado kukamilika, mheshimiwa hakimu tunaomba mahakama yako tukufu iwape dhamana washitakiwa wote watatu, tunaomba masharti nafuu ya dhamana kwa kuwa ni haki yao na hawana kumbukumbu zozote za kuwahi kuruka masharti ya dhamana, alieleza Mgongolwa wakati akiomba dhamana hiyo.
Kwa upande wake, wakili wa serikali, Joseph Haule, aliieleza mahakama kuwa upande wa mashitaka hauna pingamizi la dhamana iwapo tu itazingatia sheria ya uhujumu uchumi.
Baada ya kusikiliza pande zote, Hakimu Mwangesi, aliahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika kumi ili apate fursa ya kupitia vifungu vya sheria ya masharti ya dhamana katika kosa kama hilo.
Baada ya kupitia vifungu hivyo, majira ya saa 6 mchana, Hakimu alitoa masharti ya dhamana akimtaka kila mshitakiwa ajidhamini kwa maandishi kwa Sh5 milioni pamoja na kuwa na wadhamini wawili watakaosaini Sh5 milioni kila mmoja.
Wadhamini wawili lazima wawe watu ambao wanaaminika na hasa watumishi wa serikali, mnatakiwa kuwasilisha hati zenu za kusafiria na hamruhusiwi kutoka nje ya Dar es Salaam, alisema Hakimu Mwangesi.
Washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana wakati huo na wakili wao akalazimika kuiomba mahakama itoe muda kidogo hadi saa 7:30 mchana ili wakatafute wadhamini.
Mheshimiwa Hakimu washitakiwa leo walienda kazini kama kawaida na walipofika kazini wakakamatwa hivyo suala la kupata wadhamini kwa muda huo likawa gumu, tunaomba muda kidogo hadi saa 7:30 tutafute wadhamini,alisema.
Hakimu alikubali ombi hilo na kuhahirisha kesi hiyo hadi saa 7:30 na washitakiwa hao waliweza kutimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 20 itakapotajwa.
Sakata la Profesa Mahalu limekuwa likigonga vichwa vya habari vya magazeti nchini na katika mkutano wa bajeti bungeni liliibuka, serikali ikitakiwa kutoa msimamo wake.
Katika hotuba yake ya kuchangia kuhusu bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba, msemaji wa kambi hiyo, Fatma Maghimbi, alihoji hatua ya serikali kupeleka suala hilo Takuru badala ya mahakamani.
Tumesoma katika magazeti kwamba kumetokea wizi wa kughushi katika balozi yetu nchini Italia wa fedha za Tanzania Sh2 bilioni, wizi wa kughushi kwa lugha ya kisheria ni forgery (kughushi) na sio corruption (rushwa), alisema
Maghimbi.
Kambi hiyo iliitaka serikali kutoa ufafanuzi wa kwanini tuhuma hizo zisipelekwe mahakamani badala ya Takuru na kama ni kweli limetokea tukio hilo basi ieleze ni nani waliohusika.
Kimya cha muda mrefu cha seriali kilimalizika jana, baada ya suala hilo kufikishwa mahakamani.
Wakati hayo yakitokea, tayari Profesa Mahalu alikuwa amekwisafungua kesi ya madai Mahakama Kuu akidai fidia ys Sh12 bilioni kwa vyombo vya habari zilivyoripoti habari zake, akidai kuwa viliandika habari za uongo dhidi yake.
Profesa Mahalu katika mashtaka yake, alikuwa anadai kuchafuliwa jina lake wakati yeye katika muda wa miaka minne ya utumishi kama balozi aliwahi kutunukiwa tuzo ijulikanayo kama Stella Della Solidarieta Italiana ambayo alitunukiwa na Rais wa Italia Aprili 13 kabla ya kurudi Tanzania.
Katika kesi hiyo anayotetewa na Kampuni ya Uwakili ya Adili, mdai anataka mahakama iamuru waliomuandika wakanushe habari hizo zilizochapishwa kwenye magazeti hayo na kutangazwa kwenye vituo vya televisheni na radio vinavyomilikiwa na mshitakiwa wa kwanza. Anataka pia mahakama izuie walalamikiwa kuchapisha tena habari zozote zenye mwelekeo wa kumchafua na kumkashifu.
Pia mahakama hiyo iwaamuru walalamikiwa kumlipa fidia na riba ya gharama ambazo walalamikiwa wataamuliwa kumlipa pamoja na gharama atakazotumia kuendesha kesi hiyo.
Katika hati yake hiyo, Profesa Mahalu alieleza juu ya mpango wa serikali wa kununua jengo la ubalozi mjini Rome, Italia. Balozi huyo anadai kuwa Juni 2001 alielekezwa na serikali kutafuta jengo mjini humo kwa ajili ya ofisi za ubalozi wa Tanzania. Anadai Julai, 2001 alikamilisha kazi hiyo na kutoa ripoti kwa mwajiri wake.
Alidai kuwa alipata majengo matatu na thamani yake zilikuwa kati ya Dola za Marekani 2.25 milioni na Dola 3 milioni na kuambatanisha barua iliyoandikwa na ofisi yake kwenda Wizara ya Mambo ya Nje kuwajulisha bei za majengo hayo matatu yaliyopendekezwa na balozi kwa serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Profesa Mahalu, Julai 2001 mtathmini wa majengo aliyemtaja kwa jina moja la Kimweri kutoka serikali ya Tanzania alienda mjini Rome, Italia kwa ajili ya kutathmini majengo hayo na akapendekeza kununuliwa kwa jengo la Via Cortina D'ampezzo 185 Roma kwa gharama za Dola 3 milioni.
Ripoti ya Kimweri ya Agosti 2001 ilielezea jengo hilo kuwa ni la ghorofa tatu lenye ukubwa wa meta za mraba 1,000 na kiwanja chenye ukubwa wa meta za mraba 2,500. Jengo hilo lilielezwa kuwa liko mahali pazuri kwa vile ghorofa mbili zingefaa kutumika kama ofisi huku ghorofa moja inatumika kama nyumba ya ofisa wa ubalozi.
Profesa Mahalu pia aliambatanisha barua inayoijulisha Wizara ya Mambo ya Nje namna ambavyo mthamini wa serikali alivyopendekeza jengo hilo lishushwe bei kutoka Dola 3.7 milioni hadi hadi kufikia kati ya Dola 2.7 ambazo wakati huo zilikuwa sawa na Sh2.5 bilioni.
Maelezo hayo yanaonyesha kuwa mwaka 2002 Balozi Profesa Mahalu alikuja nchini kufuatilia malipo ya awali ya fedha hizo na wizara ikampatia Sh700 milioni badala ya Sh1 bilioni zilizokuwa zimepitishwa na Bunge kwa ajili ya ubalozi wa Italia.
Julai 03, 2002 Profesa Mahalu aliandika barua nyingine kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kumweleza majadiliano yake na mmiliki wa jengo lake na ushauri waliopeana ili asiliuze jengo hilo kwa wahitaji wengine. Katika barua hiyo balozi huyo ameeleza sababu ya kufungua akaunti katika benki ya Credito Italiano.
Profesa Mahalu anadai kuwa walilazimika kufungua akaunti hiyo maalum kwa ajili ya kuhifadhi fedha za kununua jengo hilo. Anadai walifungua akaunti namba 725400464 na wakaweka Euro 2 milioni za malipo ya awali ya jengo hilo na malipo mengine ya Euro1.09 milioni ilikuwa ni lazima yaingizwe kwenye akaunti hiyo kabla ya Septemba 2002.
Alidai kutokana na hali hiyo ubalozi ulilazimika kufungua akaunti hiyo na kuweka Sh1.9 bilioni "Maelezo ya akaunti hiyo yatawasilishwa kwako hivi karibuni huku tukisubiri kiasi kingine cha Sh1.2 bilioni," ilisema sehemu ya barua hiyo.
Profesa Mahalu pia aliandika barua Julai 05, 2002 kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje kumjulisha uamuzi wa ubalozi wa kufungua akaunti hiyo.
Septemba 23, 2002 ubalozi huo uliandika barua kwa meneja wa direzione Territoriale Italia Centrale kumwomba ahamishe Euro 3.08 milioni kutoka kwenye akaunti namba 725-400464 ya ubalozi wa Tanzania. Benki hiyo ilihamisha fedha hizo Oktoba Mosi, 2002.
Katika barua ya Profesa Mahalu ya Oktoba 8, 2002 kwenda kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, inaonyesha kuwa balozi huyo alisaini makubaliano ya kuuziana jengo hilo Oktoba Mosi na jengo hilo likakabidhiwa serikali ya Tanzania.
Katika maelezo ya ziada kwenye malalamiko yake, Profesa Mhalu alidai amewahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Italia mwaka 2000, Kabla ya hapo aliwahi kuwa ofisa wa ubalozi nchini Ujerumani kuanzia mwaka 1997.