TAKUKURU yamuita Mahalu, na Happiness Katabazi
Tanzania Daima
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewapa siku saba aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Mahalu na Grace Martin, wanaokabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi, kuorodhesha mali zao, Tanzania Daima imegundua.
Uamuzi huo wa TAKUKURU umekuja katika kipindi cha wiki mbili sasa tangu Mahakama Kuu itoe amri ya kusitishwa usikilizwaji wa ombi la Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, linalotaka kupitiwa upya kwa dhamana ya Professa Mahalu na mtuhumiwa mwenzake.
DPP katika ombi lake hilo aliiomba Mahakama Kuu ipitie upya dhamana ya Balozi Mahalu iliyotolewa katika Mahakama ya Kisutu mapema mwaka huu.
Vyanzo vya habari vya kuaminika vimeiambia Tanzania Daima kuwa Mahalu alipigiwa simu kuhusu suala hilo Jumatatu na akatakiwa afike ofisini hapo siku iliyofuata kwa ajili ya kukabidhiwa hati ya kuorodhesha mali zake.
Habari zaidi zinadai kwamba, Balozi Mahalu na Grace Martin wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi, waliitikia wito huo na Jumanne saa 4:30 walifika ofisini hapo na kupokewa na ofisa mmoja wa taasisi hiyo (jina linahifadhiwa), ambaye aliwaingiza kwenye chumba mahususi kwa mashauriano.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mahalu na mwenzake waliokuwa wameongozana na mawakili wao, walitakiwa kufanya hivyo baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa wamejilimbikizia mali.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa dakika takriban 20, Mahalu na Grace walikuwa wameongozana na mawakili wao, Bob Makani (anayemtetea Mahalu) na Cuthbert Tenga, anayemtetea Grace.
Mara baada ya mazungumzo hayo, watuhumiwa walipewa fomu maalumu za kujaza ambazo walikuwa wakitakiwa kuzirejesha ndani ya siku saba.
Hata hivyo habari zaidi zinaeleza kwamba, katika mazungumzo yao hayo, walielezwa kuwa, hati hiyo ya kutaka watuhumiwa waorodheshe mali walizonazo haina uhusiano wa kesi ya msingi iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mahalu ambaye alilithibitishia gazeti hili kuhusu kuitwa kwake TAKUKURU na kukabidhiwa hati hiyo ya maelezo, alimwelekeza mwandishi kuwasiliana na mawakili wake kwa taarifa zaidi.
Mmoja wa mawakili wake, Alex Mgongolwa, aliithibitishia Tanzania Daima kuhusu kuitwa kwa mteja wake na akaeleza kushangazwa kwake na hatua hiyo.
Kwa mujibu wa Mgongolwa, kitendo hicho cha TAKUKURU kinakwenda kinyume cha sheria kwa kuwa kesi ya msingi inayomkabili mtuhumiwa wake ingali ipo mahakamani na ilikuwa ianze kusikilizwa leo.
"Nasema kitendo cha TAKUKURU kumuita Mahalu wakati kesi ya msingi inaanza kusikilizwa mahakamani ni ukiukwaji wa sheria, kwani taasisi hiyo ilipaswa kuorodhesha mali za mteja wake mapema kabla ya kumfungulia kesi ya msingi inayomkabili, ambayo imepangwa kuanza usikilizwaji wake kesho (leo)," alisema Mgongolwa.
Mei 20 mwaka huu, Jaji Amir Mruma, alitoa uamuzi wa kusimamisha usikilizwaji wa ombi la DPP kwa kuwa alikubaliana na hoja na vigezo vilivyotolewa na jopo la mawakili wanaomtetea mwombaji (Mahalu), ambao waliiomba mahakama hiyo iangalie vigezo vitatu vya kusitisha au kutokusitisha kusikiliza ombi la DPP.
Uamuzi huo wa Jaji Mruma ulikuja baada ya kuwapo kwa kesi nyingine ya kikatiba iliyofunguliwa na Mahalu mahakamani hapo, Mei mwaka huu, aliyekuwa akipinga Sheria ya Uhujumu Uchumi kwa maelezo kuwa inakwenda kinyume cha Katiba.
Mbele ya Jaji Mruma, mawakili hao wa Mahalu na Grace waliiomba mahakama kulitupa ombi la DPP kwani kuendelea kulisikiliza, kunaweza kukaathiri kesi ya Katiba iliyofunguliwa na mteja wao.
Mawakili hao waliiomba mahakama kuangalia mizania ya nani ataathirika zaidi katika pande hizo mbili na hivyo kuathiri haki za mshitakiwa kabla ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa (na Mahalu) haijaamuliwa.
Sambamba na vigezo hivyo, mawakili hao waliiomba mahakama hiyo isitishe usikilizwaji wa ombi la DDP ambalo lilitaka sheria ya uhujumu uchumi itumike katika kufikia maamuzi ya dhamana dhidi ya Profesa Mahalu na mwenzake.
Chini ya sheria hiyo ya uhujumu uchumi, mtuhumiwa anatakiwa kutoa kama dhamana, fedha taslimu, ambazo ni sawa na nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba, jambo ambalo Mgongolwa alisema ni kinyume cha Katiba ya nchi, inayosema dhamana ni haki ya kila mtu na inapiga marufuku mtuhumiwa kutochukuliwa kuwa ni mkosaji, hadi mahakama itakapomtia hatiani.
Jaji Mruma alisema mahakama ilipitia kwa kina vigezo hivyo na kuona kwamba Profesa Mahalu ataathirika endapo sheria hiyo ya uhujumu uchumi itatumika dhidi yake na kuongeza kuwa, tangu kesi hiyo ianze, mshitakiwa amekuwa akifika mahakamani bila kukosa.
"Katiba ni sheria mama ya nchi, kwa maana hiyo, hakupaswi kuwepo na sheria nyingine inayopingana na Katiba na kwa sababu hiyo basi, natoa amri ya kusitishwa usikilizaji wa ombi la DPP hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwombaji itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi," alisema Jaji Mruma.
Aliongeza kuwa, endapo kesi ya DDP ikiendelea kusikilizwa, inaweza kuathiri haki za msingi za mshitakiwa. Mei mwaka huu, Profesa Mahalu alifungua kesi ya kikatiba ya kupinga sheria ya uhujumu uchumi, akidai kuwa, inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi na muda mfupi baada ya kufungua kesi hiyo, aliwasilisha ombi la kuiomba mahakama hiyo itoe amri ya kusitisha usikilizwaji wa kesi ya DPP.