JE, MUNGU YUKO UPANDE GANI KATIKA KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA?
Mahakama Kuu imemuachia huru mjane wa Bilionea Msuya katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili. Kwa upande wake, Mahakama Kuu imetenda haki. Lakini dada wa Bilionea Msuya na yeye ameibuka na kuilalamikia Mahakama Kuu kuwa haikutenda haki. Yeye anadai kuwa kabla ya hukumu hiyo, nyumba kule Upareni na Arusha zilikuwa zinapakwa rangi na wakisema kuwa atatoka kwa gharama yeyote ile.
Kama forensic investigation itafanyika kuhusu upakaji rangi wa nyumba na kama maneno yao yatakuwa yamerekodiwa na kuchunguzwa juu ya nani aliyeyasema inaweza kufubaza nguvu ya kimaadili ya hukumu hiyo kama kutakuwa na ukweli wowote? Je, watu waliokuwa wakisema maneno hayo walikuwa na maana gani kusema kuwa atatoka kwa gharama yeyote? Je, walijua kabla maudhui ya hukumu hiyo na ndio maana wakaanza kupaka rangi nyumba? Je, mawakili wa utetezi walijua kuwa hoja zao zilishinda na hata kabla ya jaji hajaanza kuiandika hukumu hiyo na wakaenda kuwaeleza ndugu wa mteja ndio maana wakaanza kupaka nyumba rangi?
Je, maneno ya dada huyo ni ya kupuuzwa? Je, kama yatapuuzwa wakati yameibua tuhuma nzito dhidi ya mahakama kwa kuihusianisha hukumu na mambo yaliyokuwa yakiendelea nje ya mahakama juu ya upakaji rangi wa nyumba kule Arusha na Upareni, taswira ya mahakama itakuwaje katika jamii?
Je, mahakama ina fursa ya kujitetea endapo watu wataituhumu nje ya mahakama kufuatia hukumu inazotoa? Ikitokea kuwa tuhuma hizo zina mashiko lakini walalamikaji wakaamua kutokukata rufaa kwa sababu mbalimbali kama kukosa imani na mahakama au kukosa fedha za kuendeshea kesi; mahakama inao ujasiri na uwezo wa kuamua kuipitia upya hukumu?
Je, maneno ya huyo dada yanaweza kuwaibua TAKUKURU kwenda Arusha na Upareni kwa ajili ya kuchunguza mazingira ya upakaji rangi hizo nyumba? Lakini kuna kosa gani kupaka rangi nyumba hata kama mhusika yu gerezani kama ndugu zake wanaweza? Lakini kuna kosa kwa ndugu wa mtuhumiwa kuamini kuwa mtu wao atatoka kwa gharama yeyote?
Je, kusema mtu atatoka kwa gharama ye yote ni kosa? Nini maana ya neno gharama ye yote? Je, dada wa Bilionea Msuya ndiye aliyekuwa ni mlalamikaji katika kesi hiyo au ni Jamhuri? Je, Jamhuri inaposhindwa katika kesi ya mauaji na ikaamua kuishia hapo, ndugu wa marehemu kama wao hawajaridhika watafanya nini?
Je, kuna mapungufu ye yote katika sheria zetu kwa kuacha dhamana ya kulalamika katika kesi ya mauaji mikononi mwa Jamhuri pekee bila ya familia au ndugu kuwa ni wadau pacha au hata walalamikaji wa moja kwa moja? Kama Mungu yuko upande wa wanaoonewa, unafikiri katika hili yuko upande gani? Je, yuko upande wa mke wa Bilionea Msuya au yuko katika upande wa dada wa Bilionea Msuya? Je kwa nini unafikiri hivyo? Unadhani haki haina gharama ye yote?
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Dar es Salaam, 24 Februari 2024; 1:07 usiku