Mnamo tarehe 09 Aprili, 2025 Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Tundu Lissu
alikamatwa na jeshi la polisi mara baada ya mkutano wa hadhara alioufanya Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma na kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Aprili 24, 2025 Lissu
alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka matatu ikiwemo uhaini na kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa X ambapo kesi hiyo ilihairishwa hadi Mei 06, 2025.
Aidha tarehe 03 mwezi Mei Jopo la mawakili wanaomtetea Lissu walifanya
mkutano na waandishi wa habari wakiongozwa na wakili Peter Kibatala ambapo
alisema wameamua kuzungumza na waandishi wa habari ili kuwaeleza watanzania uhalisia wa masuala mbalimbali kuhusu kesi hiyo.
Madai
Kumekuwapo na taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii ikidaiwa kuchapishwa na Nipashe kuwa Kibatala amewataka wanachama wa CHADEMA kuiacha mahakama ifanye kazi yake bila miingiliano.
Uhalisia
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia maneno muhimu (Key Word Search) ulibaini kuwa Chapisho lenye taarifa hiyo si la kweli kwani halijachapishwa katika kurasa rasmi za Nipashe.
Katika mkutano na waandishi wa habari Kibatala
alieleza kusikitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari kwa kile alichodai kuwa ni kutoa kauli zinazoingilia uhuru wa mahakama na kuingilia kesi inayoendelea inayomhusu Lissu. Rejea
hapa dakika 1:05:00 hadi 1:16:00
Pia
aliongeza kuwa wataendelea kusisitiza haki ya wananchi kushiriki kwa uwazi ili wapate kujifunza kutokana na kesi hiyo.
“Tutaendelea kusisitiza haki ya wananchi kushiriki katika kesi yao kwa wazi ili wajifunze uhaini ukifanya unachakatwa hivi na adhabu yake ni.. Ili nao wasifanye uhaini, tutaendelea kusema mahakamani kinachofichwa ni nini?”