Hivi ni kweli kuwa kidonge kikianguka chini i.e sakafuni kinakuwa hakina uwezo tena wa kufanya kazi yake mwilini pale kinapomezwa?
- Tunachokijua
- Maana ya kifamakolojia inaitaja dawa kama kemikali, au zao la kemikali (isipokuwa chakula) ambayo hutumiwa kuzuia, kutambua, kutibu, au kupunguza dalili za ugonjwa au hali isiyo ya kawaida. Pia, zinaweza kuathiri jinsi ubongo na mwili wote unavyofanya kazi na kusababisha mabadiliko katika hisia, ufahamu, mawazo au tabia.
Mgawanyo wa dawa unaweza kufanyika kwa namna mbalimbali. Tunaweza kuzigawa kwa kuzingatia;
- Sehemu zinapofanya kazi
- Mfumo wa dozi zake
- Namna zinavyofanya kazi
- Sheria zinazoongoza utolewaji wake kwa wagonjwa
- Jinsi zinavyotumika (Kupaka, kumeza au sindano)
Kuacha kufanya kazi kikidondoka chini
Vidonge ni aina ya dawa iliyo kwenye hali yabisi (Solid state), ambayo mara nyingi hutengenezwa kwa kutumia unga wenye kemikali hai moja au zaidi pamoja na viambato vingine vya kuongeza ujazo, kushikilia kemikali pamoja na kuzuia isiharibike kirahisi.
Tofauti na sindano zilivyo, vidonde havina uwezo wa kuingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu, hupaswa kupitia kwanza mfumo wa chakula ili visagwe, kisha vifyonzwe na mwili ili vioneshe athari zake. Hatua ya utakasaji (Sterilization) wa hali ya juu ili kuangamiza kabisa vimelea kama ilivyo kwa dawa zinazotolewa kwa mfumo wa sindano mara nyingi huwa haifanyiki.
Hii inamaanisha kuwa utakasaji wa kemikali hai zilizopo kwenye vidonge mara nyingi hufanyika tumboni kwenye mfumo wa chakula, hivyo kidonge kinaweza kuwa na aina fulani ya uchafu ambayo ikiingia tumboni itasafishwa kabla hakijaingia kwenye damu.
JamiiCheck imezungumza na wafamasia wenye ujuzi wa kutosha kuhusu dawa na kubaini kuwa sio kweli kuwa kidonge kikidondoka chini hukosa uwezo wa kutibu ugonjwa.
Kama ilivyo kwa vyakula na vitafunwa vingine, Kidonge kikidondoka chini kinaweza kuchafuka, pamoja na kubeba vimelea vya magonjwa vinavyoweza kuwa hatari kwa afya ikiwa kitamezwa.
Badala ya kupona, mhusika anaweza kupatwa na ugonjwa mwingine wa hatari, au hata kuongeza ukubwa wa tatizo alilonalo.
Hivyo, ili kuondoa hatari hii, unashauriwa kutokunywa kidonge kilichodondoka chini. Ni muhimu kwa tiba na usafi wa mwili.