HIlo ndilo ambalo Tanzania Civil Aviation Authority (TCAA) chini ya Bwana Hamza Johari wanakutana sasa kujadili
Wadau wa usafiri wa anga watakutana kwa siku mbili mjini hapa kujadili mambo mbalimbali, ikiwemo namna ya kuufanya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) kuwa njia panda ya usafiri wa anga.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema leo Jumatatu kuwa, mada tisa zitajadiliwa miongoni mwa hizo zikiwa ni kupungua kwa shehena ya mizigo katika sekta hiyo, udhibiti wa matumizi ya ndege zisizo na rubani na ukaguzi wa viwango vya kimataifa.
TCAA kwa kushirikiana na wadau wa usafiri wa anga wameandaa kongamano la siku mbili kuanzia kesho kujadili namna ya kuiinua na kuiboresha sekta hiyo.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu ‘Kupeleka juu sekta ya usafiri wa anga’ litafanyika mjini hapa na litazinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
"Kongamano hili litatusaidia kujua wapi tunakosea na kuibua mpango mkakati wa namna ya kusahihisha makosa hayo. Ili nchi iweze kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati ni lazima kila sekta ifanye mambo muhimu," amesema Johari.
Amesema wadau wa sekta watazungumza na wao watajitathmini kila mmoja kwa nafasi yake na baadaye watachukua hatua itakayowafikisha mahali wanapotarajia kufika.
"Kwa mujibu wa Shirika Usafiri wa Anga la Kimataifa (ICAO), katika ukaguzi na udhibiti wa viwanja vya ndege tumepiga hatua kutoka asilimia 37.8 mwaka 2013 hadi asilimia 64.4 mwaka huu na tunapaswa kuendelee juu zaidi," amesema Johari.