View attachment 308383 Mapinduzi Ndani na Nje ya Afro-Shirazi Party
Sheria mbili kati ya saba za chama cha Afro-Shirazi zinasema:
1. Kutafuta uhuru na utawala kamili utaokuwa miongoni mwa Dola zilizomo katika Shirikisho la Udugu na Dola ya Kiingereza?
2. Kuifanya na kuiamirisha Serikali ya Kidimokrasi katika visiwa vya Unguja na Pemba chini ya utawala na utii kwa Bwana Seyyid Mtukufu.21
Maneno yenye kuongoza kunako sheria mbili za chama cha Afro-Shirazi ni maneno ?Shirikisho? na ?utii kwa Bwana Seyyid Mtukufu.? Hizo zilikuwa ni sheria rasmi za chama cha ASP ambazo zilikubaliwa na viongozi wake na kukubalika kwa mujibu wa sheria za wakati ule.
Msomaji anatakiwa awe makini kabisa na hata kabla hajaendeleya kusoma inampasa afahamu kuwa viongozi wakubwa wa chama cha Afro-Shirazi, kama marehemu Mzee Abeid Amani Karume, na marehemu Mzee Thabit Kombo Jecha, au Sheikh Aboud Jumbe, hawakushiriki katika mipango halisi ya mapinduzi ya Zanzibar. Amekiri Mzee Jumbe katika kitabu chake The Partner-ship: Tanganyika Zanzibar Union: 30 Turbulent Years pale alipoandika kwenye kurasa 9?10 kuwa ?ijapokuwa nilikuwa Katibu wa Mipango wa chama cha Afro-Shirazi, sikujuwa vizuri [kuhusu Mapinduzi] asubuhi ya tarehe 12 Januari 1964. Ilikuwa ni siri iliyohifadhiwa vizuri ambayo ilifahamika na uongozi wake [Karume] tu. Mpaka hii leo hadithi kamili imefungwa ndani ya nyoyo na kumbukumbu zao.?22 Mzee Jumbe amemuingiza marehemu Mzee Karume katika uongozi wa mapinduzi bila ya kutowa dalili au ufafanuzi wa aina yoyote.
Marehemu Mzee Thabit Kombo ambaye alikuwa chini ya marehemu Mzee Abeid Amani Karume pia ndani ya kitabu Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha kilichoandikwa na Minael-Hosanna O. Mdundo na chenye Utangulizi aliouandika Mwalimu J.K. Nyerere, amekiri kwa maneno yafuatayo:
Usiniulize vijana wetu walioendesha mapinduzi walipata wapi mafunzo, au nani hasa alivamia mahali gani; mimi sijui. Nasikia hadithi tu kila mmoja akijinasibu baada ya kushinda, mengi ya kweli na mengine ya uwongo mtupu.23
Mpaka sasa hivi hakuna ushahidi wowote, mbali ya ule wa kinaga ubaga ambao unaweza kuthibitisha kuwa marehemu Mzee Abeid Amani Karume alikuwa jemedari wa Mapinduzi ya Zanzibar kama ilivyofanywa iaminike na kusadikiwa na wengi. Mara utasikia jemedari alikuwa Mzee Karume, na mara nyingine utasikia jemedari mkuu alikuwa ni ?Field Marshall? John Okello. Mara nyingine utasikia mpishi mkuu alikuwa marehemu Abdulrahman Mohammed Babu na nadhariya iliozamishwa ndani ya bongo za kila Mzanzibari na asiyekuwa Mzanzibari ni Mapinduzi yaliongozwa na Kamati ya Watu 14 au 13 + 1.
Hili ni jambo muhimu kuweza kuufahamu undani wake kwa sababu hapa ndipo kwenye kizungumkuti cha Mapinduzi ya Zanzibar. Hapa ndipo penye guo zito ambalo linatakiwa angalau ligeuzwe liwe chandarua. Kuanguka kwa Kamati ya Watu 14 kwenye chati ya Mapinduzi ya Zanzibar ni njia pekee ya kulivuwa guo la khadaa na kuirudishiya jamii nzima ya Kizanzibari na ya Kitanganyika nuru ya kufahamu inakotoka na kujipangiya inakotaka kwenda na kufika. Suala ni jee, Kamati ya Watu 14 walikuwa ndio viongozi wa mapinduzi ya Zanzibar au walikuwa ni walinzi wa kulilinda paziya la uongozi khasa wa mapinduzi?
Kati ya memba wa Kamati ya Watu 14 waliokuwa hai na wenye siha ya kuzungumza ni wazee Hamid Ameir na Abdalla Saidi Natepe. Katika mahojiano ambayo alifanyiwa Mzee Hamid Ameir katika gazeti la Mwananchi la tarehe 11 Januari 2008, mwandishi Salma Said alimuuliza ?ni kwa nini wewe uko kimya kiasi hicho na hadi vizazi vya sasa haviutambui mchango wako?? Alijibu Mzee Hamid Ameir, memba wa Kamati ya Watu 14 kwa kusema:
Mimi sipendi kujitokeza kwa sababu kuna vitabu vingi sana tayari vimeshaandikwa kuhusu historia ya Sultani na kufanyika kwa Mapinduzi lakini cha muhimu zaidi ni kuwa unapojitokeza na kuzungumza wanatokea watu wanajibu hoja ulizozungumza na kuweka listi kubwa ya watu waliofanya Mapinduzi, nami kwa kuwa sipendi mabishano na kwa kuwa nafahamu kwamba kuna mtu siku moja ataandika historia ya kweli, hivyo mimi nimeamua kukaa kimyaa.24
Tarehe 8 Septemba 2002, alizungumza marehemu Mzee Khamis Daruweshi, memba mwengine wa Kamati ya Watu 14, na gazeti la Johari ya Mwananchi katika habari yenye kichwa cha maneno ?Hamis Daruweshi afichua siri ya Mapinduzi Zanzibar?. Katika sababu alizozitowa Mzee Daruweshi za kufanyika mapinduzi Zanzibar ni kuwa watu wa Zanzibar ?walikuwa hawataki kujinasibu kama Waafrika. Hawapendi kuunga mkono Waafrika na walikuwa wakiwaita wakata maji.? Daruweshi pia alielezea kuwa:
Huyu Okello alikuwa miongoni mwa Afro Shirazi [Youth] League. Tulimchukua Pemba alikokuwa akichonga mawe ili kutoa matufali. Tulimchukua kwa kazi maalum kwa sababu baada ya mapinduzi, tulijua tulihitaji mtu ambaye atatangaza mapinduzi hayo kwa lafudhi ambayo ni tofauti kabisa na ya wenyeji wa Zanzibar.25
Mzee Daruweshi alijifahamisha kuwa:
Mimi ni Myao, mtu wa Ruvuma, Tunduru, kijiji cha Masuguru, kata ya Malumba. Lakini hapa Zanzibar nimekuja zamani kidogo tangu mwaka 1941, niko hapa ?nimenationalize? uraia wa Zanzibar. Nilipiga kura katika uchaguzi wa mwaka 1957. Lakini uchaguzi wa pili ikaja pingamizi kwamba wote waliozaliwa Bara hawatapiga kura. Ukijipanga kwenye mstari, wanakuja wakikuuliza, katika mstari walikuwapo mawakala wa Hizbu na wa ASP. Unaulizwa utamke ?halua?, wengine hawawezi wanasema ?haarua? kwa hiyo wanakutimua kwenye mstari kwa kuwa wanajua kwamba wewe siyo Mzanzibari na kwa hiyo tuliotoka Bara wengi tukashindwa kupiga kura. Kwa hiyo nikaomba uraia wa Zanzibar Aprili 19 mwaka 1960 na kupewa kadi nambari 2020.26
La msingi katika mazungumzo ya Daruweshi ni kule kuelezea kwake bila ya kuweka ushahidi au vielelezo vyovyote vile kuwa: ?Labda ni vyema ikajulikana tangu mwanzo kwamba kamati iliyoundwa na Karume ya kuongoza mapinduzi hayo, ilikuwa na jumla ya watu 14.?27
Walipotembeleya Cuba katika mwezi wa Mei 1964, Shirika la Habari la Cuba liliwafanyiya mahojiano memba wawili wa Kamati ya watu 14, Ramadhani Haji na Saidi Idi Bavuai yenye kutowa mwangaza mzuri juu ya maandalizi ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kutowa historia fupi ya Afro-Shirazi kutokeya mwaka 1957 walielezeya matukio yaliofikiya kupinduliwa kwa Sultan Sayyid Jamshid bin Abdullah:
Uchaguzi ulipofanyika mwaka 1963 chini ya utawala wa kikoloni wa Kiingereza, chama cha Afro-Shirazi kilishindwa na kiliunda kamati ya kufanya mapinduzi. Baada ya uchaguzi kikundi kidogo cha chama cha Afro-Shirazi kiliungana na Chama cha Kizalendo (Nationalist Party).
Haya mapinduzi ya watu 14 hayakuungana wakati wowote ule na chama chochote chengine kikiwemo chama cha Afro-Shirazi?hata chama cha Afro-Shirazi chenyewe kilikuwa hakielewi kinachoendelea.28
Inaendelea ripoti ya Kiingereza juu ya ziara ya Bavuai na Haji:
Mchango wa kimapinduzi wa John Okello ulidharauliwa na Iddi na Haji na walisema kuwa mashirika ya habari yalikosea kumhusisha yeye kama ni kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar?Waliwaeleza Rais Karume na Waziri wa Mambo ya Nje Babu kuwa ni watu ambao hawakushiriki moja kwa moja katika harakati za mapinduzi, lakini hata hivyo, wanastahiki vyeo walivyokuwa navyo.
Inavyoonyesha, memba hao wawili wa Baraza la Mawaziri walishtukiwa na muungano wa Zanzibar na Tanganyika, na waliona haya kutamka chochote kuhusu maendeleo hayo huku wakieleza kuwa [muungano] umefanyika wakati wao wako nje ya Zanzibar.29
Mara nyingi imekuwa ikisikika kuwa Mzee Abdalla Saidi Natepe ameandika kitabu kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar lakini hakitotolewa mpaka kufariki kwake. Hapa panaonekana kuna dalili kuwa mwanamapinduzi Mzee Natepe amekosa ushujaa wa kuandika kuhusu mapinduzi ya Zanzibar katika uhai wake na kuweza kuingiya katika midani ya mazungumzo wakati yungali hai.
Fikra iliyozoweleka na kushindiliwa ndani ya bongo za Wazanzibari na wasiokuwa Wazanzibari ni kuwa Kamati ya watu 14 ndiyo kamati iliyokabidhiwa kazi ya kuyapanga mipango ya mapinduzi na Mzee Karume. Hapana shaka memba wa kamati hiyo walihusika na mapinduzi na kama alivyosema marehemu Mzee Thabit Kombo ?Usiniulize vijana wetu walioendesha mapinduzi walipata wapi mafunzo, au nani hasa alivamia mahali gani; mimi sijui. Nasikia hadithi tu kila mmoja akijinasibu baada ya kushinda, mengi ya kweli na mengine ya uwongo mtupu.?30
Sasa inawezekana kuwa Mzee Karume alikuwa jemedari wa Mapinduzi na msaidizi wake Mzee Thabit Kombo asiwajuwe vijana wa mapinduzi na awe amesikia hadithi tu. Lakini hili la ?uwongo mtupu? ndilo linalofaa kutushughulisha. Ni uwongo gani huo wenye kuupotosha ukweli wa Mapinduzi ya Zanzibar? Uwezekano unaoingiya akilini na msomaji akawa ana uhuru wa kupima baada ya kumaliza kukisoma kitabu ni mambo mawili. La kwanza ni kuna utata wa idadi na majina ya memba wa hiyo Kamati ya Watu 14. Pili, na muhimu zaidi, inamkinika sana kuwa Kamati ya watu 14 iliundwa na kukwezwa baada ya Mapinduzi kwa lengo la kuufunika ukweli wa chimbuko la Mapinduzi yenyewe.
Tukirudi kunako kitabu maarufu na muhimu cha Mzee Aboud Jumbe The Partner-ship utakuta anwani yenye kusema ?siasa za Zanzibar kabla ya muungano.? Mzee Jumbe anaelezeya kuwa:
Hata kabla ya Mapinduzi, Uongozi wa Siasa [wa ASP] ulikuwa haujaungana sawasawa. Kulikuwa na mvutano wenye kukuwa, kati ya wale, nikiwemo mimi mwenyewe, tuliomuunga mkono Karume, na baadae tukapewa jina la ?Karume-Yeka?; na wale waliokuwa wakimpinga; na waliobakia waliojaribu kuyakubali makundi yote mawili. Mpasuko huu nusura ukivunje chama mwaka 1961 kwenye mkutano mkuu wa chama uliofanyika Municipal Hall, Mji Mkongwe.31
Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu The Zanzibar Revolution and Its Aftermath, Anthony Clayton, ?tarehe 2 Januari [1964] mivutano ndani ya A.S.P. ilikamilika pale walipojiuzulu Othman Sharif, Hasnu Makame, Idris Wakyl na Saleh Saadalla.?32
Bwana George Mooring, katika barua yake ya tarehe 29 Agosti, 1963, kwaW. B. L. Monson wa Ofisi ya Makoloni, London, ameandika kuwa:
Imeripotiwa kuwa Moshe Feinsilber, Yahudi mwenye kuendesha biashara ya samaki hapa [Zanzibar], amejishughulisha na siasa kwa kuiunga mkono A.S.P. na yumo kujaribu kuwavutia viongozi wakubwa wa chama waachane na Abeid Karume na waungane na Othman Shariff katika jitihada zake za kuungana na Z.P.P.P. Ijapokuwa kikawaida maoni yake huwa yana uzito ndani ya chama, yeye [Finsilber] pia ameshindwa kukipeleka chama kwa Othman Shariff.
Wakati huu viongozi wa A.S.P. wamekuwa wakitembelea Dar es Salaam mara kwa mara kwa kupata ushauri, ambapo imeripotiwa kuwa washauri wao wakubwa ni Kawawa na Kambona. Inasemekana kuwa Watanganyika wameshinikiza kuwa endapo Z.P.P.P. itakataa kujiengua kutoka Z.N.P. na kujiunga na A.S.P. basi A.S.P. iwe chama cha upinzani na isikubali kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na vyama vingine viwili [Z.P.P.P. au Z.N.P.]. Bahati mbaya ushauri huu umekubaliwa na A.S.P.; kwa vyovyote vile uwezekano wa kuundwa Serikali ya vyama vyote ya Umoja wa Kitaifa, umepotea.
Hapana shaka A.S.P. wameridhika kuwa mwisho wake, uzito wa kuungwa mkono na bara ndio utakaowaweka madarakani Zanzibar, na inawezekana ni imani hiyo kuliko kitu chengine chochote inayotuweka kwenye hali tuliyo nayo.33
Ripoti ya siri na kielelezo cha mukhtasari cha kitengo cha usalama cha Zanzibar cha tarehe 31 Julai?28 Agosti, 1963 kinamuelezeya:
MOSHE FINSILBER, mtu wa Israel Zanzibar, ambaye ni memba kamili wa A.S.P. Katika mikakati ilioelezewa katika kifungu kilichopita, [Finsilber] dhahiri amekuwa akimuunga mkono OTHMAN SHARIFF MUSA katika mkakati wake wa kuungana na Z.P.P.P. na amejaribu kwa uwezo wake wote kumvuta SALEH SAADALLA AKIDA na ABOUD JUMBE MWINYI kuachana na ABEID AMANI KARUME na kujiunga na OTHMAN SHARIFF MUSA. Lengo la FINSILBER, ni bila shaka, ni kukingowa chama cha Z.N.P. chenye kuongozwa na Waarabu ili kisiungwe mkono na walio wengi. Anatumia ushawishi wake mkubwa ndani ya chama [A.S.P.] kuondowa ushirikiano wowote ule wa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itaihusisha Z.N.P.34
Ni dhahiri baada ya kukamata khatamu za serikali marehemu Mzee Karume aliwabadilishia kibao Maisraeli kwa kule kuwaunga mkono makhasimu wake ndani ya A.S.P. Anaandika William Edgett Smith kwenye kitabu chake Nyerere of Tanzania:
Israel, kwa mfano, ilikuwa iwe rafiki wa kwanza na wa karibu wa serikali mpya, kwa sababu Maisraeli walikuwa wachangiaji wakubwa wa chama cha Afro-Shirazi katika miaka kabla ya uhuru. Lakini, baada ya mapinduzi, Maisraeli walipojaribu kuanzisha mahusiano na serikali ya Karume, walikutana na upinzani mkubwa usiofahamika.35
Kwa upande wake, Mzee Jumbe ameonyesha kuwa mvutano ulikuwa baina ya ujumbe kutoka Pemba ambao ulishikiliya kuwa Othman Shariff awe Waziri Mkuu baada ya uchaguzi mkuu wa kabla ya uhuru wa Zanzibar. Mvutano huo, anaendeleya kuelezeya Mzee Jumbe, uliendeleya kufukuta na ulijitokeza kwa nguvu katika mkutano wa pili wa kikatiba uliofanyika jijini London. Anaandika Mzee Jumbe:
Karume alikuja kujuwa kuwa baadhi ya wajumbe wa ujumbe wake walikuwa wanataka kufanya urafiki na ujumbe wa serikali kwa lengo la kutaka kujuwa wangeliweza kupewa nafasi gani za uongozi wakiamuwa kutoka kwenye chama cha upinzani [ASP]?Karume alifupisha mazungumzo ya London na akaweza kuuondowa uwezekano wa mpasuko ndani ya safu ya chama.36
Mpasuko ndani ya ASP ambao Mzee Jumbe amejaribu kuuonesha ni mpasuko baina ya ujumbe wa ASP kutoka Pemba na ule uliokuwa chini ya uongozi wa Mzee Karume. Hakuna mahala ambapo Mzee Jumbe ameutaja upinzani wa marehemu Abdalla Kassim Hanga, Abdulaziz Twala au Saleh Saadalla Akida dhidi ya uongozi wa Mzee Karume. Wala hakutowa maelezo yoyote kuhusu TANU kama ilikuwa ikimuunga mkono Mzee Karume au kundi lipi lililokuwa dhidi ya uongozi wake ndani ya ASP. Kwa mujibu wa Mzee Abbasi, ?TANU ilikuwa imeshachoka na hayati Mzee Karume na khasa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Julai 1963.?37
Katika kuthibitisha kutoelewana Mzee Karume na Mwalimu Nyerere, anaelezeya Profesa Issa G. Shivji, kuwa Mzee Aboud Jumbe anaelezeya kuwa baada ya daktari wa Kichina kumuambiya kuwa Mzee Karume alikufa palepale alipopigwa makao makuu ya A.S.P. Kisiwandui, Mzee Jumbe moja kwa moja alimpigiya simu Mwalimu Nyerere na kumwambiya:
Huku jambo kubwa limetokea. Yeye [Nyerere] akaniambia ?Karume?? Nikasema ?ndio.? Akasema ?basi nitaitisha Baraza la Mawaziri.? ?Sauti ya maelezo ya Mzee Jumbe ilitowa ujumbe kuwa Mwalimu Nyerere alikwishajuwa kuwa Karume ameshauawa Zanzibar kabla ya kuarifiwa na Mzee Jumbe.38
Kipindi cha kabla ya kuuliwa kwa Mzee Karume hali ya uhusiano baina yake na Mwalimu Nyerere ilikuwa mbaya kuliko wakati mwengine wowote ule.
Anaelezeya Shivji:
Kwa mujibu wa Jumbe [Karume na Nyerere] walikuwa hawazungumzi kwa mwaka mzima au kama hivyo kabla ya kuuliwa. Bhoke Munanka kwa upande wa Nyerere, na Jumbe kwa upande wa Karume, walikuwa wajumbe wa kupeleka na kurudisha habari. Salim Rashid amemuambia mwandishi [Shivji] kuwa alipokwenda kumuaga Karume baada ya kuwacha kazi serikalini siku moja kabla ya kuuliwa, Karume alimshauri kuwa asiwache kazi kwa sababu alikuwa anataka kuuvunja Muungano.39
Undani wa kuuwawa kwa marehemu Mzee Karume umeficha Mapinduzi kama kuundwa kwa Kamati ya Watu 14 kulivyolifunika kombe mwanaharamu apite. Nadhariya iliyopo ni kuwa waliyopanga kumuuwa marehemu Mzee Karume walikuwa wanafanya kazi ndani ya mpango ambao hawakuutambuwa undani wake. Maalim Seid Sharif Hamad ameandika kuwa ?Baadhi ya watu wanafikiria kuwa Nyerere alimtumilia Babu na chama cha Umma kumuuwa Karume kwa sababu ikijulikana vizuri kuwa yeye [Nyerere] na Karume walikuwa hawana masikilizano mazuri.?40
Alipohojiwa Babu na mwandishi wa televisheni wa Kiingereza alikiri kuwa Balozi wa Cuba aliyekuwepo Dar es Salaam alikuwa hajui chochote kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kama alivyokuwa hakuyajuwa yeye. Babu aliyarudiya maneno ya John Okello kwa kusema kuwa hakusaidiwa na nchi za kikoministi katika kuyapanga mapinduzi ya Zanzibar bali alisaidiwa na ?Mungu wa Waafrika.?
Jee, Waingereza hawakumuona ?Mungu wa Waafrika? alipokuwa akiandaa kupinduliwa kwa Dola ya Zanzibar na badala yake waliamua kuwanyosheya kidole wana-Umma Party kutokana na imani yao kuwa ASP haikuwa na uwezo wa kufanya Mapinduzi bila ya Tanganyika? Na si hivyo tu, Mzee Karume, Babu na viongozi wengi wengine wakaipokeya sifa ya kuyaongoza mapinduzi na kumfunikia kombe ?Mungu wa Waafrika?? Kama John Okello alikuwa ni mtu aliyekuwa na nyota mbaya iliyochomoza na kuanguka papohapo, na marehemu Babu na Karume walikuwa hawayajuwi mapinduzi lakini walijaaliwa kupata vyeo, watakuwa wamebakiya nani na kwa ushahidi gani ambao walikuwa viongozi wa mapinduzi ya Zanzibar? Ni Waafrika waliowapinduwa Waarabu Zanzibar au ni Waafrika waliowapinduwa Wazanzibari?
Takwimu za Kikabila Zanzibar
Ukiiweka kando propaganda inayolinganisha Ubantu peke yake na Uafrika utakuta Marais wakubwa wa Kiarabu wa Kaskazini ya Afrika, marehemu Gamal Abdel Nasser, na Ahmed Ben Bella ambaye yuhai, walikuwa upande wa ASP na TANU katika kuyafanikisha mapinduzi ambayo kijuujuu yamekuwa yamefahamishwa na kufahamika kuwa yalikuwa mapinduzi ya ?Waafrika? wanyonge dhidi ya ?Waarabu? mabepari wa Zanzibar. Kana kwamba hao Waarabu wote wa Zanzibar walikuwa matajiri na mabepari.
Akitumiya takwimu za Michael Lofchie, Profesa Issa G. Shivji ameeleza yakuwa asilimia moja (1) tu ya jamii ya Kiarabu ilokuwa ikiishi Zanzibar kabla ya Mapinduzi ilikuwa katika tabaka la juu la kijamii, na asilimia 76 ya Waarabu walikuwa katika tabaka la chini. Kwa mujibu wa takwimu za kikabila za 1948 Waafrika Asilia (Washirazi) walikuwa asilimia 56.2, Waafrika kutoka bara walikuwa na asilimia 19.4, Waarabu asilimia 16.9, Wahindi asilimia 5.8, na Wangazija asilimia 1.2.41
La msingi si kutafautisha baina ya tabaka za Waarabu baina ya asilimia 1 na 76, bali kufahamu kuwa hawa Waarabu masikini za Mungu wa asilimia 76 waliokuwa wakiishi mashamba ndio walioubeba mzigo wa kifo na maangamizi katika mapinduzi ya 1964.42 Na hao hao Waarabu wa kawaida wa Kizanzibari waliokuwa wakulima, wavunjaji mbata na wazegazega hubebeshwa tuhuma za utumwa. Na katika hiyo asilimia 1 ya tabaka la juu na la kati la Kiarabu ipo haja pia ya kujiuliza Waarabu wa Zanzibar wakijiona kama raia au watawala? Kama watawala mbona hawajazijaza skuli za Kiarabu nchini? Mbona wengi wao walikuwa hawaijuwi lugha ya Kiarabu? Na nini mchango wa Waarabu katika kuijenga Zanzibar? Mlango wa Pili 30
Leo Mji Mkongwe wa Zanzibar una heshima ya Kimataifa (World Heritage Site) uliopewa na shirika la UNESCO la Umoja wa Mataifa (UN). Wakfu wa mwanzo wa maji ya mji wa Zanzibar ulianzishwa na Sayyid Barghash bin Said bin Sultan. Mchango wa Wahindi hauelezwi vya kutosha na khasa katika kuigharimiya misafara ya utumwa, au kuipa misaada ya kifedha chama cha Afro-Shirazi, au hata mchango katika kazi za udobi, ukataji nywele, au kuuza vifuu. Na huenda sababu ikawa kutaka kuonyesha pengo la kibaguzi baina ya Waafrika kutoka bara (asilimia 19.4) na Waarabu (asilimia 16.9). Takwimu hazisemi asilimia ngapi kati ya Waafrika kutoka Bara na Waarabu walikuwa Wazanzibari kisheria au kinyume na sheria.