Nakumbuka tatizo la mgawo wa umeme lilipotokea mwaka 2006 mhe. Rais J. M. Kikwete pamoja na Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo walitangazia wananchi kuwa hakutatokea tena kamwe tatizo hilo. Alienda mbali zaidi na kusafiri hadi nchini Marekani akasema kwa kaka yake George W. Bush taarifa ya namna hiyo na kuwahakikishia wawekezaji mbalimbali kutoka Amerika waje kuwekeza maana umeme hautakuwa tatizo tena. Leo baada ya kipindi cha miaka takilibani miwili na kitu, tatizo hilo ndani ya uongozi wake limejitokeza tena kwa makali makubwa hata kuzidi ya kipindi hicho.
Ujumbe wangu ni kwamba, kama watanzania hatutabadilika na kuondokana na kutoa ahadi za maneno pasipo matendo yeyote, basi hata yote yaliyosemwa na serikali hakika hayawezi kufikiwa. Kuna semi mbalimbali kama "maisha bora kwa kila mtanzania, kilimo kwanza na mengine mengi". Hakika kwa mfumo huu uliopo maendeleo yatapatikana wapi. Napenda nikumbushe tu tatizo letu linalotusababisha tubaki hapo tulipo. Ni kuanzia Rais kushuka chini, tumepokonywa utambuzi wa nini tunatakiwa tuviweke kipa umbele kama uwekezaji wa kitaifa wenye manufaa ya kubadilisha maisha ya watanzania kwa muda mrefu (long run basis). Badala yake serikali na watendaji wake kwa shinikizo la "kushinda uchaguzi ujao" wamekuwa wakitupia nguvu ngingi katika kutekeleza Ahadi alizozitoa Mhe, wakati wa kampeni za uchaguzi zenye mtazamo wa makundi na siyo utaifa. Kwa mfano, kama wasukuma aliona hawapendi hiki, basi alisema tutakiondoa hiki na kuwaletea kitu mbadala. Hivi kweli huo ni msimamo anaopaswa kuwa nao mkuu wa nchi??.... Hata kidogo, hapa nayasema haya siyo kwa shinikizo lolote lile tofauti na Utanzania wangu.
Vipa umbele vipo vingi sana ambavyo kwa kipato kidogo cha taifa letu hatuwezi kuyatimiza yote mara moja. Hivyo tunatakiwa tutekeleze yale muhimu (First ranked Priorities) kwa malengo ya kuboresha uchumi wa pato kwa wakati mfupi na mrefu (short-run and long-run). Huwezi ukapata maendeleo ya uchumi wakati ukuaji wa uchumi utokanao wa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji haufanyiki. Hadi hapo Rais atakapokuwa mwendawazimu wa maamuzi ndipo Tanzania tutaona maisha yetu ya baadaye yana dalili za kustawi. Uwendawazimu ninaousema hapa ni kuachana na mfumo huu uliochafuka kwa makundi yasiyo na uzalendo badala yake unatazama kwa jicho la "sisi na chama chetu" na siyo Watanzania na nchi yetu. Mara nyingi sana serikali hii hii ilishasema haina fedha za kuwekeza kwenye miradi mikubwa lakini utashangaa leo (juma hili), Rais anaamuru serikali igharimie kuwasha mitambo yenye kutumia fedha takiribani shilingi bilioni 23 kwa mwezi (chanzo: Magazeti ya Tanzania Daima na Mwananchi). Hii ni sawa na sh bilioni 276 kwa mwaka. Hivi, Rais angeamuru kujengwa kwa mradi wa umeme utakaogharimu sh. Tirioni 1 na ukatekelezwa kwa miaka minne tangu 2006, tungeshindwa kuutekeleza jamani? Leo wapi hizo fedha zimetoka kama siyo kupitia vyanzo vya kawaida vya mapata ya serikali yetu!
Huwezi ukasema unajenga mazingira ya kukuza uzalishaji nchini ikiwa ni lengo la kukuza ongezeko la uchumi nchini halafu kusiwe na vyanzo vya kuaminika vya umeme. Bila uwendawazi tu hakuna tunachofanya na ni aibu kusema Tanzania tuna nia ya kubadilisha maisha ya wananchi hali hakuna hatua tunazozifanya za makusudi hayo. Kwenye uchaguzi wa 2005 kulingana na vyanzo mbalimbali vya taarifa juu ya CCM ilivyochota fedha zaidi ya Trilioni moja Benki kuu kwa lengo la kununua tisheti, kofia, kanga na takrima kwa wananchi ili wawachague. Hivi uchaguliwa ndiyo imekuwa msukumo wa kuendesha nchi yetu. Hebu tusukumwe na hali mbaya ya maisha ya watanzania hivyo tunagombea ili tuwe na maamuzi ya kiwendawazimu kwa kudhibiti myanya yote inayosababisha pato la taifa lipotee pasipo kuwekeshwa katika miradi ya uzalishaji mali. Tupunguze gharama/matumizi ya kuziendesha serikali zetu.
Hata tukiwa na wataalamu wa uchumi wa kiwango gani kama haya hayatazingatiwa tutaishia tu kuzima moto kila mara kama inavyotokea ukurupukaji katika suala la kutatua mgawo wa umeme unaoendelea kwa sasa. Nani alaumiwe hapa kama siyo serikali iliyokuwa inafahamu hali ya uzalishaji umeme tangu iingie madarakani. Nayasema haya, si kwa wana CCM tu bali ni kwa Watanzania wote, kwamba yeyote anayefikiria kuwatumikia watanzania wa sasa walio ndani ya matatizo mengi likiwepo kubwa la umasikini wa kipato, basi wawe na msukumo wa kuyaondoa haya na siyo vinginevyo. Wawe CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF, UDP, na vyama vingine, tuache ubabaishaji. Kama Rais alisema tatizo hilo la umeme halitatokea tena asingesubiri hali hii itokee ndipo aanze kutapatapa. Tukichezea muda hakika hatuwezi kuurudisha nyumba ili tuyafanye ambayo hatukuyafanya. Kama 2006 Rais alikuwa na dhamira ya kudhibiti tatizo lisitokee, hatua hiyo ilipaswa ianzie palepale kwa kutumia fedha ili fedha nyingi zije ziokolewe baadaye na kutumiwa kwenye miradi mingine ya kiuchumi.
NB: Naomba wasomaji wa habari hii waniwie radhi pengine lugha yangu si sanifu sana lakini ujumbe ni huo hapo!!!! Asanteni.