Kikwete aapishwa rasmi
Rais Jakaya Kiwete akiwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania General Mwamunyange
Rais Jakaya Kiwete ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuwashinda wapinzani wake kwa asilimia 61 za kura zote zilizopigwa.
Akitoa hotuba mara baada ya kuapishwa alisema kuwa kipao mbele chake kwa hivi sasa ni kuhakikisha kuwa wanajenga umoja wa kitaifa na kurudisha amani iliyokuwepo awali kwani anaamini kuwa uchaguzi uliweza kuwagawa watanzania kwa namna moja ama nyingine
Alisema mchakato wa jinsi serikali yake itakavyofanya kazi ataitoa hivi karibuni wakati akilihutubia Bunge jipya
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Leon Bahati na Godfrey Nyang'oro
TUME ya Uchaguzi (Nec) jana ilimtangaza mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete kuwa mshindi wa nafasi ya rais baada ya kupata asilimia 61.17 ya kura zote zilizopigwa Oktoba 31.Mwenyekiti wa Nec, Jaji Lewis Makame alimtangaza mshindi huyo kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee iliyotawaliwa na ulinzi mkali huku mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa akiikosa hafla hiyo.
Kwa mujibu wa Jaji Makame, Kikwete alikusanya kura kura milioni 5.27 kati ya kura milioni 8.62 zilizopigwa na anafuatiwa na mgombea wa Chadema, Dk Willbrod Slaa aliyepata milioni 2.3 sawa na asilimia 26.34.
Lakini katibu huyo wa Chadema Dk. Slaa, ambaye alisema atayakataa matokeo hayo kutokana na taratibu nyingi kukiukwa, hakuhudhuria hafla hiyo.
"Nawapongeza wananchi, wanachama wa CCM na viongozi wa upinzani kwa kuonyesha ushirikiano," alisema Kikwete katika hotuba yake ya shukrani baada ya kutangazwa kuwa rais mteule.
"Napenda kuwathibitishia wananchi kwamba nitatekeleza ahadi zote nilizoahidi kwa mujibu wa ilani ya CCM; ahadi za papo kwa hapo nilizozitoa baada ya kutathmini matatizo ya wananchi na mambo mazuri ambayo yalielezwa na wapinzani.
"Katika yale waliyotoa wapinzani, yapo yanayoshabihiana na ya kwetu lakini kuna baadhi waliyoyatoa mazuri zaidi kuliko sisi. Tutayazingatia.
"Lengo la wagombea ni kuijenga nchi kimaendeleo na siyo kugombana. Tunajenga nyumba moja, hatugombei fito."
Lakini Kikwete, ambaye aliingia Ikulu kwa kuzoa asilimia 81 ya kura zote mwaka 2005, alionyesha kustushwa na ushindi mdogo wa mwaka huu wa asilimia 61.1.
Wakuu wa nchi wakifuatilia kwa makini kuapishwa kwa Rais Jakaya Kikwete
"Kuna changamoto nyingi zilijitokeza ambazo zitaifanya CCM ijiulize na kukaa chini ili kutafuta ufumbuzi wake... kutafuta nguvu mpya katika chaguzi zijazo," alisema Kikwete.
"Pamoja na wapinzani kuonyesha kuimarika, itabidi tukae kitako kuangalia ni namna gani tutafanya ili katika chaguzi zijazo tuweze kufanya vizuri zaidi."
Wagombea wengine watano walihudhuria hafla hiyo ambayo ilikuwa hitimisho la mtifuano wa kisiasa wa wagombea wote saba waliokuwa wakizunguka nchi nzima kwa takriban miezi mitatu wakiomba ridhaa ya kuongoza Watanzania.
Mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alishika nafasi ya tatu akiwa amepata kura 695,667 sawa na asilimia 8.06, akifiatiwa na Peter Mziray wa APPT-Maendeleo aliyepata kura 96,933 sawa na asilimia 1.12, Hashimu Rungwe wa NCCR-Mageuzi kura 26,388(0.31%), Muttamwega Mgahywa wa TLP kura 17,482(0.20%) na Fahmi Dovutwa wa UPDP 13,176 (0.15%).
Hata hivyo, ni asilimia 42.8 tu waliojiandikisha, ndio walioshiriki kupiga kura Oktoba 31, idadi ambayo ilikuwa gumzo miongoni mwa wengi walioshiriki hafla hiyo kutokana na kutofautiana sana na hamasa iliyoonekana wakati wa kampeni.
Takwimu za Nec zinaonyesha kuwa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa watu 20,137,303, lakini waliojitokeza kupiga kura ni watu 8,626,283 tu, kiwango ambacho hakifikii hata nusu ya walioandikishwa kwenye daftari la wapigakura.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Jaji Makame alisema kwa mujibu wa ibara ya 41(6) ya katiba, mshindi anapatikana kwa kupata kura nyingi zaidi ya wenzake.
"Kwa mujibu wa Ibara ya 41(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania... Namtangaza Jakaya Mrisho Kikwete wa Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 31 mwezi wa kumi (2010)," alisema Jaji Makame.
Tangazo hilo lilichafua utaratibu mzima wa hafla hiyo kutokana na wakereketwa wa CCM kuanza kushangilia na kuimba na kumfanya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Rajabu Kiravu awakemee.
"Kinachofanyika hapa ni kuiharibu hii hafla hii," alilalamika Kiravu, lakini wapenzi wa CCM waliendelea kuimba nyimbo, kushangilia huku wakipeperusha bendera ndogo za CCM.
Hali hiyo ilimlazimisha Kiravu kuchukua kipaza sauti na kuwataka viongozi wa CCM wawatulize wakereketwa hao.
Jaji Makame alisema kwamba matokeo hayo yanatoka kwa wasimamizi wa majimbo 239 kote nchini.
Alisema majimbo saba hayakufanya uchaguzi wa wabunge na kata 23 hazikuchagua madiwani wao, lakini akasema chaguzi hizo zitafanyika mapema iwezekanavyo.
Baadaye Jaji Makame alimkabidhi Kikwete cheti cha ushindi na kufuatiwa na hotuba fupi iliyotolewa na Prof Lipumba kwa niaba ya wagombea urais walioshindwa.
Profesa Lipumba alisema katika hotuba yake kuwa alipewa nafasi hiyo kutokana na mshindi wa pili, Dk Slaa kutofika kwenye hafla hiyo.
"Salamu hizi zilikuwa zitolewe na Dk Slaa. Tulikuwa tumekubaliana mshindi wa pili ndiye atakayewawakilisha wenzake, lakini kwa kuwa hayupo, imenibidi nichukue nafasi hiyo," alisema Prof Lipumba.
Prof Lipumba alisema wote kwa pamoja wanampongeza Kikwete kwa ushindi alioupata.
Lakini alitoa lawama nyingi kwa Tume, akidai kuwa ilishindwa kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.
Alisema kuna watu wengi walioshindwa kupiga kura kwa sababu tu majina yao hayakuorodheshwa katika karatasi zilizobandikwa kwenye vituo mbalimbali vya wapiga kura nchini.
Alisema ushindi wa Kikwete si wa kujivunia kwa sababu alichaguliwa na asilimia 27 tu ya watu waliojiandikisha kupiga kura.
"Pamoja na kutambua Kikwete ni mshindi, waliomchagua ni asilimia 27 tu. Hili si jambo la kujivunia. Tume wametuangusha hawakuweza kuwahamasisha wengi wajitokeze kupiga kura," alisema Profesa Lipumba.
Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na baadhi ya maofisa wa Nec waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina gazetini.
Walisema kazi hiyo si ya Nec pekee, bali pamoja na vyama vya siasa kuhakikisha wafuasi wao wamejiandikisha na kujitokeza kupiga kura.
Profesa Lipumba alielezea pia kuwa vyama vya upinzani havina imani na Nec na vimekuwa na wasiwasi kama kweli wanauendesha kwa njia huru na ya haki kama wanavyojinadi.
Viongozi hao wa upinzani walipendekeza kuwa muundo wa tume hiyo ubadilishwe ili uweze kuwa na watu watakaoaminika pande zote.
Mwakilishi hiyo alisema suala la kukubali matokeo wamekuwa waklilichukulia kama ni moja ya njia za kutekeleza uvumilivu wa kisiasa.
Lipumba alimaliza kwa kumkabidhi Kikwete ilani ya CUF kwa tahadhari kwamba hakutumwa na wagombea wengine, bali ni kwa utashi wake ili kiongozi huyo aitumie katika kuleta maendeleo nchini.
Akitoa hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi, Kikwete alianza kwa kuwakemea wafuasi wa CCM waliokuwa wakishangilia kwenye hafla hiyo bila ya kujali utaratibu.
"Tafadhali shughuli hii inasimamiwa na Tume; tafadhali tutulie; tusubiri iishe kama ni kujimwaga, mfanye hivyo baadaye," alisema rais huyo mteule.
Rais huyo mteule alielezea tathmini ya uchaguzi huo akisema kuwa imeonyesha demokrasia nchini inaimarika.
Aliigeukia Nec akisema kuwa nao wajitathmini na kujipanga kukabili kasoro zilizojitokeza, akiwaasa kwamba kazi yao ni ya lawama.
Katika kuendelea kutathmini uchaguzi uliomalizika, alisema mambo mengi yenye madhara yanayoelekea kuligawa taifa kama vile siasa za udini, ukabila na kuchochea uhasama miongoni mwa wananchi yalijitokeza.
Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na vyombo vya habari kujitahidi kufuta chokochoko hizo ili Tanzania iendelee kuwa ya amani na utulivu.
Aliviasa vyombo vya habari kwamba vikitia chumvi chokochoko hizo vitakoleza moto na hata kulifanya taifa kuangukia kwenye matatizo ya ubaguzi.
Hata hivyo, alivisifu vyombo vya habari nchini kwamba vilifanya kazi nzuri wakati wa kipindi chote cha kampeni.
Katika hatua nyingine aliwataka waangalizi kutoka sehemu mbalimbali kutoa taarifa zao ili Tanzania izitumie kama njia ya kujitathmini na kurekebisha kasoro kwenye chaguzi zijazo.
Watu mbalimbali walialikwa kuhudhuria hafla hiyo na miongoni ni mabalozi wa nchi mbalimbali wanaowakilisha hapa nchini, wakurugenzi wa mashirika ya umma na binafsi, wahariri watendaji wa vyombo vya habari, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mawaziri wanaomaliza muda wao, wabunge wateule wa CCM na wanachama wakereketwa wa CCM.
Wengine ni marais wastaafu, Benjamin Mkapa wa awamu ya tatu na waziri mkuu mstaafu, Joseph Warioba na majaji wa Mahakama Kuu na wastaafu.
Kikwete ataapishwa leo.
Sherehe hizo zitahudhuriwa na marais kutoka Kenya, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya Nje pamoja na Ushirikiano wa Kimataifa, nchi nyingine zitakazotuma wawakilishi wake ni Burundi, Msumbiji, Algeria, Botswana na Uganda
Chanzo.
Gazeti la Mwananchi