Na Mgaya Kingoba,
Ngorongoro
Mgombea urais wa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameonesha mfano katika kuhimiza ufugaji wa kisasa na usio wa kuhamahama kufuata malisho, akimiliki ng'ombe 400 ambao malisho yake yanalimwa katika shamba lake.
Amewaambia wafugaji nchini kwamba kama hawajui ng'ombe wao watakula nini, ni bora wasifuge.
Alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti mjini Rujewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya wiki hii na juzi alikuwa Loliondo wilayani hapa, kote akiomba kura kwa wananchi.
Rais Kikwete alieleza hayo wakati akifafanua kuhusu ilani ya Uchaguzi ya CCM, inavyoelekeza juu ya ufugaji wa kisasa na hasa kuhakikiksha wafugaji hawaendelei kuhamahama kwa nia ya kusaka malisho.
"Mimi pia nafuga, nina ng'ombe si haba. Sasa nimelima majani, nina ng'ombe 400 na ekari 600, na nimechimba kisima napata maji pale," alieleza Rais Kikwete bila kufafanua lilipo shamba lake.
"Katika kiangazi kikali cha mwaka, hakuna ng'ombe wangu hata mmoja aliyekufa. Sina ugomvi na jirani yangu. Ni kitu kinachowezekana tunaposema ufike wakati wafugaji wasihemeane na wawe na malisho ya mifugo yao.
Alisema kama mfugaji hajui ng'ombe wake watakula nini, ni bora asifuge kwa sababu kwa mwenendo wa sasa, ufugaji wa kuhamahama hauna muda mrefu……
Chanzo: HABARILEO Jumapili.