Kikwete, kwa nini Ballali?
KAMA kuna jambo lililotushangaza kwa Rais Jakaya Kikwete tangu alipoingia madarakani, ni kumpa kisogo aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Ballali, tangu alipoanza kuugua, alipolazwa hospitalini hadi alipofariki dunia Ijumaa wiki iliyopita.
Si kawaida ya rais wetu kufanya kitendo kama hiki. Tunavyomjua sisi wa Tanzania Daima Jumapili, ni mtu anayewajali Watanzania wake, hasa wanapokuwa katika matatizo, bila kujali kama walimkosea yeye au serikali yake.
Maswali wanayojiuliza Watanzania wengi kwa sasa baada ya kupatikana kwa taarifa za kifo cha Dk. Ballali, ndiyo tunayojiuliza hata sisi, ingawa hatupati majibu. Tunajua wapo wanaoweza kuyajibu lakini kwa makusudi wameamua kukaa kimya.
Ukimya wao huo, ndio uliotufanya tufikirie mbali zaidi hadi kumfikia Rais Kikwete, ambaye ingawa ameonyesha kutenda tofauti na kawaida yake katika hili la Dk. Ballali, lakini tunaamini anaweza kuwaambia Watanzania sababu iliyomfanya yeye na serikali yake kujiweka mbali katika kipindi chote kigumu cha kuugua hadi kufariki dunia kwa Dk. Ballali.
Tunaamini kuwa kifo cha Dk. Ballali, iwe kilitokea kwa mipango ya watu fulani au kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, kinamuweka Rais Kikwete katika wakati mgumu, kwa sababu kadhaa, kubwa ikiwa kushindwa kwa serikali na timu aliyoiunda kuchunguza wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Aidha, picha waliyonayo sasa Watanzania dhidi ya Rais Kikwete, inazusha maswali mengi, likiwamo la kama huruma yake ni kwa Watanzania wote au wapo baadhi ambao hawaonei huruma hata wanapokuwa katika hatari ya kufa.
Picha hii inajitokeza kutokana na mlolongo wa matukio yasiyo kuwa ya kawaida aliyoyafanya dhidi ya Dk. Ballali.
Tangu aingie madarakani, Rais Kikwete amejiwekea rekodi ya kutokataa barua za kujiuzulu za wasaidizi wake.
Mifano ya hali hii ni kukubali kwake kujiuzulu kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, marehemu Ditopile Mzuzuri, aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, ambaye aliachia ngazi pamoja na mawaziri wawili, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, na hivi karibuni, Andrew Chenge.
Hawa wote waliandika barua za kujiuzulu baada ya kuandamwa na kashfa, kila mmoja kwa namna yake. Lakini kwa Dk. Ballali haikuwa hivyo, alikataa barua yake ya kujiuzulu baada ya kutolewa kwa taarifa ya uchunguzi wa kashfa ya EPA na siku chache baadaye alimtimua kazi.
Jambo jingine linaloleta utata ni kutopatikana kwa taarifa za kama Rais Kikwete alikwenda kumjulia hali Dk. Ballali wakati akiwa kitandani huko Marekani, akiugulia ugonjwa uliomuua. Rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa Rais Kikwete ni mwepesi kwenda kuwajulia hali watu wanaomgusa wanapokuwa wagonjwa au kuhudhuria mazishi yao.
Alifanya hivyo kwa marehemu Amina Chifupa, alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Lugalo na alikwenda Muhimbili kuwajulia hali waandishi wa habari wa MwanaHalisi, Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage, walipojeruhiwa wakiwa kazini, bila kujali kama watu hao ni wakosoaji wakubwa wa serikali yake.
Kwa Dk. Ballali haya yote hakuyafanya. Kwa roho ya ubinadamu ya kawaida sisi tunadhani ipo sababu ya kutokea kwa yote haya ambayo sasa yamezua picha tofauti kabisa miongoni mwa jamii ya Watanzania. Tunaamini kuwa Rais Kikwete anatambua Dk. Ballali alikuwa ni mmoja wa washirika wake wa karibu kikazi hadi alipougua na kwenda Marekani kutibiwa, hivyo kwa roho ya kibinadamu, anaweza kuwaeleza Watanzania walau kwa ufupi sababu ya ukimya wake kwa Ballali. Tunaamini rais anaweza kufanya hivyo kwa kumbukumbu tuliyonayo kutoka kwa swahiba wake, Lowassa, ambaye baada ya kulazimika kujiuzulu, rais alitumia mkutano wake na wazee wa Dar es Salaam kueleza jinsi alivyoumizwa na kujiuzulu huko kwa Lowassa, bila kuwajali watu wangemfikiliaje! Tunaomba afanye hivyo na kwa Dk. Ballali.