:jaw:Jaji Warioba avunja ukimya
Asema uongozi umebinafsishwa kwa wenye fedha
na Bertha Mwambela na Violet Tillya, Tanga
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amekemea matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi, akisema yameingiza sumu mbaya katika mchakato wa kuwapata viongozi na kulifanya taifa litawaliwe na wafadhili badala ya viongozi.
Jaji Warioba, alisema hayo jana wakati akifungua kongamano la mwaka la maadili ya waandishi wa habari mjini hapa, lililoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Alisema uongozi umebinafsishwa na kugeuzwa biashara ya wenye fedha na kwamba ndiyo chanzo cha siasa za chuki, kashfa, malumbano na mgawanyiko.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hali hii ndiyo imeleta mgawanyiko na hali tete ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hali hii ikiendelea nchi itafikishwa pabaya. Ni lazima kutafakari na kuchukua hatua. Nchi inahitaji viongozi badala ya wafadhili
uchaguzi, hasa uchaguzi wa kutumia fedha na kashfa, ndiyo umetufikisha hapa, alisema Jaji Warioba.
Akitoa mfano, Jaji Warioba alisema huko nyuma hali hiyo iliwahi kutokea.
Kumbukeni vizuri mwaka 1995 walijitokeza wanachama 19 waliopendekezwa kugombea urais, hata walipopunguzwa na kubaki watatu na hatimaye mmoja, chama hakikugawanyika maana hakukuwa na makundi, alisema Jaji Warioba.
Alisema, hata walipotolewa nje ya ukumbi na kuanza kujadiliwa na vikao vya juu, walikuwa wanacheka na kutaniana kwa maneno kama: Unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.
lakini hali ya sasa ni tofauti kwani ushindani wa kisiasa unaelekea kugeuzwa uadui.
Jaji Warioba aliwakejeli wanasiasa wanaotangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, wakidai wamechangiwa fedha na wananchi ili walipie fomu za kugombea, akisema fedha hizo ni zao wenyewe, si za wananchi maskini wanaosingiziwa kuchanga fedha hizo.
Kwa mujibu wa Warioba, fedha zimemaliza hata nguvu ya kamati za maadili ndani ya vyama, ambavyo badala ya kuwachukuliwa hatua wanachama kama ilivyokuwa zamani, vinaishia kuwashtaki Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kongamano hilo lililokuwa likijadili wajibu wa vyombo vya habari katika uchaguzi, lilishirikisha wahariri, wamiliki, viongozi wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Bara na Visiwani na wadau mbalimbali wa habari nchini.
Walijadili, pamoja na mambo mengine, Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambayo Jaji Warioba alisema ina madhumuni mazuri, lakini matendo ya viongozi yanaonyesha kuwa hayaendani na matakwa ya sheria hiyo.
Alisisitiza, hata Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa sheria hiyo, hana uwezo, hana zana za kutosha za kuitekeleza.
Ofisi yake iko Dar es Salaam, uchaguzi uko nchi nzima, ana wafanyakazi wachache, raslimali chache
ni mtumishi wa serikali
hana ubavu, alisema Jaji Warioba.
Alisema hata TAKUKURU, haiwajibiki kwa Msajili na Vyama vya Siasa, nayo haina uwezo wa kuwabana wanasiasa ambao tayari wanagawa pikipiki na baiskeli.
Ni vigumu kwa chombo cha umma kuwadhibiti viongozi walio madarakani, ndiyo maana hata katika mapamabano ya ufisadi, walio madarakani hawakuguswa, alisema Jaji Warioba.
Jaji Warioba alieleza kuwa katika miaka ya nyuma mgombea yeyote aliweza kupita bila kupingwa kutokana na kukubalika katika jamii tofauti na sasa ambapo wagombea wengi wanaonekana wamekuwa wakinunua uteuzi katika vyama vyao na kuwanunua wapinzani ili kuvuruga taratibu za uchaguzi.
Alisema, uteuzi wa mgombea ni hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi kwenye majimbo mengi ambapo uchaguzi unaishia kwenye uteuzi.
Akitoa mfano, alisema Tanzania Bara CCM ina nguvu kubwa katika majimbo yalio mengi, jambo ambalo linamfanya mteule wa CCM kwa nafasi ya Rais kuwa na uhakika wa kushinda.
Kwa sababu ya umuhimu wa uteuzi, fedha nyingi zinatumika, CCM imeamua kura za maoni iwashirikishe wanachama wake wote kwenye ngazi ya kijiji, kuna imani kuwa mgombea hawezi kuhonga wanachama wote ngazi ya kijiji. Imani hii ni potofu, kwani hivi sasa kuna watu wanatamba watatumia sh milioni 200 kwenye jimbo la uchaguzi, alisema Jaji Warioba.
Alisema wagombea hao wana uwezo wa kuhonga kila mwanachama hata sh 1,000 kila mtu na wana uwezo pia wa kununua mamluki. Alisisitiza kuwa tayari kadi za vyama vya siasa hasa CCM zinauzwa kwa madhumuni hayo.
Hakuna uchaguzi ambao hauna udanganyifu, kwani wanaogombea
uongozi hutumia kila mbinu ili kushinda na wakati mwingine mbinu zisizo halali hutumika; inawezekana udanganyifu ukaanzia kwenye zoezi zima la uandikishaji hadi kwenye hatua ya kupiga, kuhesabu na kujumlisha kura. Udanganyifu umekuwepo kila uchaguzi unapofanywa, alisema Jaji Warioba.
Alisema viongozi wamekuwa wakikiuka maagizo ya Rais na hawachukuliwi hatua yoyote. Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni na hasa baada ya kutungwa kwa sheria za gharama za uchaguzi, amekuwa akilaani vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, lakini viongozi walio chini yake ndani ya CCM na serikali kwa ujumla wao wako kimya badala yake wanagawa vitu majimboni, alisema Jaji Warioba.